Programu hiyo imepangwa kufanyika kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 12, 2026, kupitia vipindi saba. Mercy amesema inalenga wanawake wanaotaka kujenga ndoa yenye furaha na kufuata misingi ya imani yao.
Hata hivyo, tangazo hilo limeibua swali ambalo wengi wamekuwa wakijadili: Kwa nini wanawake wanafundishwa jinsi ya kuwa wake bora, lakini wanaume hawapewi msisitizo sawa kuhusu kuwa waume bora?
Janet Mbugua ameibua suala la ukatili dhidi ya wanawake.
Mwanahabari wa zamani wa Citizen TV Janet Mbugua amekosoa mpango huo, akihoji iwapo taasisi za kidini zinatoa uzito wa kutosha kwa masuala ya ukatili wa kijinsia, mauaji ya wanawake na dhuluma zinazowakumba wanawake na watoto.
Kwa Janet, mjadala hauhusu tu kama watu wanapaswa kufundishwa kuhusu ndoa. Anahoji pia vipaumbele vya taasisi za kidini wakati jamii inakabiliwa na changamoto hizo, pamoja na matarajio kwamba mara nyingi wanawake ndio wanaopaswa kufanya juhudi zaidi ili ndoa zidumu. Hoja yake kuu ni kwamba ndoa ni jukumu la watu wawili, na mwanamke mmoja hawezi kubeba jukumu lote la kuifanya ifanikiwe.
Mashirima Kapombe naye amtetea Mercy.
Kwa upande mwingine, mwandishi wa Citizen Tv Mashirima Kapombe amemtetea Mercy, akisema si sawa kumshambulia mwanamke kwa kuanzisha programu ambayo wengine hawaungi mkono.
Hoja ya wanaomtetea Mercy ni kwamba wanawake wanaotaka mwongozo wa ndoa kwa misingi ya imani yao wanapaswa kuwa na nafasi ya kupata elimu hiyo. Kwa mtazamo wao, kuwepo kwa programu ya kuwafundisha wanawake kuhusu ndoa hakumaanishi kwamba wanaume hawapaswi kuwajibishwa.
Katikati ya mvutano huo, waandaaji wameongeza kipindi cha Becoming a Husband, kitakachomshirikisha Kabi WaJesus, kufuatia wito wa kuwepo kwa mafunzo yanayowahusisha wanaume pia.
Je, mjadala ni kuhusu ndoa au namna tunavyoifundisha?
Kwa upande mmoja, watu wanaona hakuna ubaya kwa Mercy kushiriki uzoefu wake na kutoa mwongozo kwa wanawake wanaoutafuta. Kwa upande mwingine, wakosoaji wanataka wanaume wafundishwe kwa kiwango sawa kuhusu heshima, mawasiliano, uwajibikaji na kushiriki katika kujenga familia.
Pia kuna swali pana zaidi kuhusu nafasi ya kanisa: Je, Kanisa linaweza kuendelea kufundisha kuhusu ndoa huku likitoa sauti yenye nguvu dhidi ya ukatili, dhuluma na ukosefu wa haki?
Mjadala huu kwa hiyo hauishii kwa Mercy Masika pekee. Unagusa namna jamii inavyoelewa ndoa, majukumu ya wenza na matarajio yanayowekwa kwa wanawake.
Je, mnaona Mercy Masika anakosolewa visvyo kutoa mafunzo ambayo baadhi ya wanawake wanayahitaji, au wakosoaji wana hoja kwamba jamii imekuwa ikiwafundisha wanawake jinsi ya kuwa wake huku ikiwapa wanaume nafasi ndogo ya kuwajibishwa kama waume? Maoni yako ni yapi? Unaonaje wewe?