Msingi mkuu wa imani yetu ya Kikristo ni katika Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wetu; kama njia pekee ya uzima kuufikia ufalme wa milele. Viongozi wetu wa kiroho ni binadamu wenzetu waliojaliwa karama mbalimbali na Mwenyenzi Mungu ili watusaidie katika safari hiyo. Hata kama tunabarikiwa sana na huduma za viongozi wa kiroho, itakuwa kosa kubwa kama nguvu ya Ukristo wetu itajikita katika binadamu wenzetu badala ya Kristo pekee kwani nao (viongozi) wanahitaji kuitafuta ile Nuru katika maisha yao siku zote. Hata Mitume pamoja na kazi ngumu sana walizofanya ikiwa ni pamoja na kujitoa mhanga hawakuwahi kuchukua nafasi ya Kristo.
Ninachokiona nyakati hizi ni kuwa viongozi wa kiroho wamekuwa na umaarufu mkubwa ambao wakati mwingine hufunika jina Kuu la Kristo kiasi kwamba uono wa wakristo huishia kwao. Wakipata matatizo basi utasikia maelfu wakitetereka katika imani. Wakipotoka na kwenda nje ya Maandiko ndio taabu kabisa maana wengi watawafuata hukohuko bila wenyewe kutafuta kweli imesimamia wapi.
Kwa hili la Benny Hinn na wahubiri wengine wanaopatwa na matatizo, turudi kwenye Biblia ili kuimarisha u-Kristo wetu, tuweze hata kuwasaidia (kuwaombea) wote wenye matatizo (ikiwa ni pamoja na sisi wenyewe) tusijejikuta tukiingia kwenye ushabiki usiokuwa na tija kiroho.