Blasio Kachuchu
JF-Expert Member
- Sep 7, 2016
- 721
- 438

Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, akiwa katika hatua moja wapo ya uchunguzi wa saratani ya matiti wakati wa zoezi la uhamasishaji lililoandaliwa na benki hiyo kupitia programu ya Exim Cares kwa kutumia wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, jijini Dar es Salaam, tarehe 23 Oktoba 2026.
Zoezi hilo liliwapa wafanyakazi wa benki na wanajamii inayowazunguka kupata elimu na huduma ya uchunguzi bure, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwezi wa Uhamasishaji kuhusu Saratani ya Matiti, unaoadhimishwa kila Oktoba, kwa lengo la kuhamasisha utambuzi wa mapema na matumizi ya taarifa sahihi za afya.
BENKI ya Exim Tanzania kupitia programu yake ya uwajibikaji kwa jamii ya Exim Cares, imetoa elimu na huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti bila malipo kwa wafanyakazi wake na wanajamii wanaoizunguka, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Mwezi wa Uhamasishaji kuhusu Saratani ya Matiti.
Zoezi hilo lililofanyika Oktoba 23, 2026, katika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, lilishirikisha wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road waliotoa elimu kuhusu dalili za ugonjwa huo, mabadiliko yasiyo ya kawaida mwilini na umuhimu wa kutafuta huduma za afya mapema.
Kupitia kampeni hiyo, washiriki walielimishwa kuhusu umuhimu wa tathmini ya kitabibu wanapobaini mabadiliko kwenye matiti, huku juhudi zikilenga kupunguza hofu na dhana potofu zinazoweza kuwafanya watu kuchelewa kupata huduma.Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, alisema afya na ustawi wa wafanyakazi pamoja na jamii ni sehemu muhimu ya mchango wa benki hiyo kupitia programu ya Exim Cares.
Alisema benki inaunga mkono juhudi zinazowezesha jamii kupata taarifa sahihi za afya na kuelewa umuhimu wa kuchukua hatua kwa wakati, akisisitiza kuwa uhamasishaji kuhusu saratani ya matiti ni hatua muhimu katika kuimarisha utunzaji wa afya na upatikanaji wa huduma zinazofaa.
D’souza aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani asilimia 80 ya saratani ya matiti hutokea kwa wanawake wasio na vihatarishi maalumu vinavyojulikana, isipokuwa kuwa mwanamke na kuongezeka kwa umri. Alisema hali hiyo inaonesha kuwa kutokuwa na historia ya ugonjwa huo katika familia hakumaanishi kuwa mtu hawezi kuupata.Kwa upande wake, Daktari Maguha Stephano, mwakilishi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, alisema utoaji wa taarifa sahihi na kuhamasisha jamii kutafuta huduma za afya mapema ni muhimu katika kukabiliana na saratani ya matiti.
Alitaja baadhi ya dalili zinazopaswa kupewa kipaumbele kuwa ni uvimbe kwenye titi au kwapani, pamoja na mabadiliko kwenye ngozi ya titi au chuchu, akiwataka watu wanaobaini mabadiliko hayo kutafuta ushauri wa kitaalamu bila kuchelewa.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC), makadirio ya mwaka 2024 yanaonesha kuwa kulikuwa na visa vipya takribani milioni 2.43 vya saratani ya matiti duniani. Nchini Tanzania, wanawake takribani 3,024 walikadiriwa kugundulika na ugonjwa huo, huku vifo 1,492 vikikadiriwa kutokana na saratani hiyo katika mwaka huo.Takwimu za WHO pia zinaonesha kuwa kiwango cha kuishi kwa angalau miaka mitano baada ya kugundulika na saratani ya matiti kilikadiriwa kuwa asilimia 77.8 duniani, ikilinganishwa na asilimia 39.1 katika Kanda ya Afrika ya WHO kwa wanawake waliogundulika kati ya mwaka 2017 na 2021. Hali hiyo inasisitiza umuhimu wa utambuzi wa mapema na upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wakati.
Benki ya Exim Tanzania imewahimiza wafanyakazi wake na jamii kwa ujumla kuweka utunzaji wa afya kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu uchunguzi unaofaa na kutochelewa kutafuta huduma za afya wanapobaini mabadiliko yasiyo ya kawaida.



