UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
Kilimo cha migomba ni tegemeo muhimu la kiuchumi na chakula kwa kaya nyingi nchini, lakini kwa sasa, ugonjwa wa Fungashada umegeuka kuwa tishio kubwa linalotafuna jasho la wakulima huku mamlaka zinazohusika zikiwa zimenyamaza kimya. Katika mfululizo wa makala hizi, tunaanza kueleza ukubwa wa tatizo hili na athari zake za kusikitisha kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Maisha ya Steven Mwita, mkulima na mkazi wa Mtaa wa Konga A, Kata ya Mzinga iliyopo nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, yamebadilika ghafla baada ya shamba lake la migomba lenye ukubwa wa ekari nne kukumbwa na ugonjwa hatari wa Fungashada ya Migomba.
Kila mwezi alikuwa na uhakika wa kuvuna kati ya mikungu ya ndizi 100 hadi 80. Kwa sasa, yote hayo yamebaki kuwa historia, Mwita hana uwezo hata wa kuvuna mkungu mmoja wa ndizi kwani ugonjwa huo umezika ndoto zake. Zaidi ya shilingi 500,000 alizowekeza kwenye shamba lake katika msimu wa kilimo wa 2023/24 zimeyeyuka mithili ya moto wa mabua kwenye upepo mkali.
Migomba iliyoathirika na ugonjwa wa fungashada.Kwa sasa hana mbele wala nyuma, kwani ekari nne za shamba la migomba ndilo lilikuwa tegemeo lake kuu katika kuendesha maisha yake, ikiwemo kulipia ada za shule za watoto. Chanzo cha hali hii ilikuwa ni miche aliyonunua kutoka kwa mkulima mwenzake bila kujua kuwa ilikuwa imeambukizwa.
"Nilipewa miche na jirani. Sikujua kama ilikuwa na ugonjwa. Leo migomba yote imekufa, nashindwa kupata mahitaji yangu ya msingi kama zamani," anasema kwa huzuni.
Kisa cha Mwita kinawakilisha kilio cha wakulima wengi wa migomba katika wilaya ya Morogoro, hasa Manispaa ya Morogoro, wanaoendelea kupoteza matumaini kutokana na kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa huo bila kuwepo kwa mkakati thabiti wa kuudhibiti kutoka kwa mamlaka zinazohusika.
Ukubwa wa tatizo
Bi. Zainabu Salum, mkulima wa Kata ya Kauzeni, Manispaa ya Morogoro, anasema kuwa kabla ya ugonjwa wa fungashada kuingia shambani kwake, alikuwa akiuza mikungu 130 hadi 150 ya ndizi kwa msimu kupitia shamba lake la nyumbani. Leo hii, hana hata mkungu mmoja wa kutegemea.
Utafiti unaonyesha jinsi hali ilivyobadilika kuwa janga la kitaifa. Ripoti ya Utafiti uliofanywa mwaka 2023 kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda (TAHA), kuhusu ugonjwa huo ilionyesha kuwa katika Wilaya ya Morogoro, ni Kata ya Mzinga pekee ndiyo iliyokuwa imeripotiwa kuwa na ugonjwa huo, ukiwa umeathiri asilimia 90 ya mashamba ya migomba.
Leo hii, sauti za vilio zimevuka mipaka ya Kata ya Mzinga na kuenea katika maeneo mengine. Afisa Kilimo wa Manispaa ya Morogoro, Shabani Charles, anakiri kuwepo kwa ugonjwa huo na kubainisha kuwa hadi kufikia Julai 31, 2026, umeenea katika Kata za Kauzeni, na Bigwa, ndani ya halmashauri hiyo.
"Kwa sasa idara yetu inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara wa miche ya migomba kuchukua tahadhari na kutambua hatari iliyopo," anasema Charles.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Konga A, Kata ya Mzinga Ally Abdu Kondo, anatoa takwimu za kutisha akieleza kuwa zaidi ya ekari 600 za migomba zimeathirika katika mtaa wake pekee kutokana na biashara holela ya miche (machipukizi) ya migomba hali inayochangia kuenea kwa ugonjwa wa Funga shada, huku ukiwaacha wakulima wakiwa njia panda bila msaada.
Sheria na ukimya wa mamlaka
Licha ya sheria kuwepo wazi, utekelezaji wake umekuwa kitendawili kinachogharimu wakulima. Kifungu cha 5 cha Sheria ya Afya ya Mimea na Viuatilifu ya Mwaka 2020 kinaipa TPHPA wajibu wa kusimamia afya ya mimea nchini, kufanya ufuatiliaji (surveillance), na kutoa vyeti vya afya ya mimea.
Aidha, vifungu vya 21 hadi 35 vya sheria hiyo vinaweka masharti makali ya vibali vya kuingiza na kusafirisha mimea, wakati Kifungu cha 45(1) kinatoa mamlaka ya kutangaza maeneo ya yaliyoathiriwa na mlipuko wa magonjwa ya mimea kuwekwa chini ya karantini ya muda.
Hata hivyo, wakulima kama bigwa kisiwani wa Kata ya Bigwa manispaa ya Morogoro anainyooshea kidole Tassisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) kwa kushindwa kuchukua hatua kudhibiti biashara holela ya michipukizi ya migomba.
"Biashara holela ya machipukizi ya migomba ndiyo chanzo kikuu cha kusambaa kwa ugonjwa huu. Mbali na kutodhibitiwa kwa biashara hii, Idara ya Kilimo, TOSCI na TPHPA zimeshindwa kuchukua hatua madhubuti zikiwemo kuweka karantini rasmi," anasema Farida.
Anataja maeneo yanayozunguka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuwa kinara wa biashara hiyo holela, ambapo wakulima huingia mtegoni wakiamini miche hiyo imezalishwa na wataalamu na ni salama, jambo ambalo si ukweli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Nyasebwa Chimagu, anasema taasisi hiyo kwa kushirikiana na TARI imeanza kusajili aina mpya za mbegu bora za migomba ili kuwasaidia wakulima kupata miche yenye afya na kupunguza matumizi ya miche ya asili ambayo mara nyingi hubeba magonjwa.
Fungashada ni nini na inaenezwaje?
Akifafanua kuhusu ugonjwa huo, Dkt. Beatrice Mwaipopo, mtafiti kutoka Idara ya Sayansi ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), anasema kuwa Fungashada au Banana Bunchy Top Virus (BBTV) hushambulia migomba na kuzuia ukuaji wake.
"Majani ya mgomba yenye ugonjwa huu yanapoota hushindwa kutanuka vizuri, hujikusanya na kujifunga pamoja yakifanana na ua, jambo linalofanya mgomba ushindwe kuzaa kabisa," anaeleza Dkt. Mwaipopo.
Kwa mujibu wa Hamad Lyimo, Afisa Kilimo Mkuu wa TPHPA, virusi hivi havisambai kwa hewa au maji ya mvua, bali huenea kwa njia kuu mbili.
Anaitaja njia ya kwanza ni kupitia wadudu wanaoitwa viwavi wapepevu (Aphids) wa aina ya Pentalonia nigronervosa, ambao hufyonza utomvu wenye virusi na kuviambukiza kwa migomba mizima; na pili, kupitia usafirishaji na upandaji wa machipukizi yaliyoambukizwa.
Lyimo anabainisha kuwa tangu mwaka 2020, ugonjwa huo umezidi kusambaa na hadi kufikia Mei 2026 ulikuwa umethibitishwa katika mikoa tisa ikiwemo Morogoro, Pwani, Mbeya, Arusha, Dodoma, Geita, Katavi, Kilimanjaro, na Mwanza. Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ya mwaka 2024 ilionyesha kuwa hadi Machi 2024, ugonjwa huo ulikuwa umeenea katika mikoa 9 nchini.
"Tanzania bado haijaukubali ugonjwa huu kuwa dharura ya kitaifa, na kuna uhaba wa rasilimali za kutosha za kuudhibiti," anakiri Lyimo.
Athari za kiuchumi
Madhara ya ugonjwa huu ni makubwa na yanatishia usalama wa chakula na uchumi wa taifa. Afisa Kilimo Mkuu wa TPHPA, Hamad Lyimo, alithibitisha kuwa ugonjwa wa Fungashada una madhara makubwa kwa wakulima na walaji; kwa wakulima hupunguza uzalishaji na kupunguza au kupoteza mapato yao, na kwa walaji huchangia kupanda kwa bei ya ndizi sokoni.
Ripoti ya mradi wa Mbinu za Kikanda Kudhibiti Ugonjwa wa Fungashada kwa Migomba barani Afrika ya taasisi ya Standards and Trade Development Facility (STDF) unaotekelezwa na Baraza la Afya ya Mimea la Umoja wa Afrika (AU-IAPSC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) yam waka 2023, inaonyesha kuwa nchi za Afrika zilizokusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania, zinapoteza dola za Marekani milioni 200 hadi 600 kwa mwaka kutokana na janga hili.
Hali hii inazua swali kubwa kwa Wizara ya Kilimo, TPHPA, TOSCI, na Idara ya Kilimo Manispaa ya Morogoro: Wakati sheria zipo na mamlaka zimeainishwa wazi, kwa nini hatua madhubuti hazichukuliwa mapema kuokoa mamilioni ya ekari za migomba nchini? Wakulima kama Steven Mwita na Zainabu Salum wanaendelea kulia peke yao huku mashamba yao yakiteketea.
Pia soma:
~ Mamilioni yanapotea Shambani Serikali Inasubiri ‘Dharura’ Itangazwe
~ Kutokuchukua hatua kunavyoeneza fungashada Morogoro
Wakulima kama Steven Mwita na Zainabu Salum hawaitaji tena semina za kinadharia; wanahitaji sera thabiti, udhibiti mkali wa miche holela, uwekaji wa kanda za karantini, na fidia au ruzuku ya kurejesha matumaini yao. Ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa sasa, zao la ndizi litabaki kuwa historia inayofuta uchumi wa familia nyingi nchini.
Katika sehemu ijayo ya mfululizo wa makala hizi itaangalia chanzo cha kusambaa kwa ugonjwa wa Fungashada katika manispaa ya Morogoro nana ni wanahusika na tatizo hilo.
ANDIKO LA: Farida Mangube, Morogoro
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
Maisha ya Steven Mwita, mkulima na mkazi wa Mtaa wa Konga A, Kata ya Mzinga iliyopo nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, yamebadilika ghafla baada ya shamba lake la migomba lenye ukubwa wa ekari nne kukumbwa na ugonjwa hatari wa Fungashada ya Migomba.
Kila mwezi alikuwa na uhakika wa kuvuna kati ya mikungu ya ndizi 100 hadi 80. Kwa sasa, yote hayo yamebaki kuwa historia, Mwita hana uwezo hata wa kuvuna mkungu mmoja wa ndizi kwani ugonjwa huo umezika ndoto zake. Zaidi ya shilingi 500,000 alizowekeza kwenye shamba lake katika msimu wa kilimo wa 2023/24 zimeyeyuka mithili ya moto wa mabua kwenye upepo mkali.
Migomba iliyoathirika na ugonjwa wa fungashada.