SoC02 Bidhaa ya mawazo

Stories of Change - 2022 Competition

Tibaiwa

Member
Joined
Sep 8, 2021
Posts
51
Reaction score
38
Ninayoimani kubwa kuwa Tanzania tumepoteza hazina kubwa ya ubunifu, maarifa na mapato kwa kukosa watu sahihi wa kuyaibua na kuyaendeleza mawazo ya kibunifu.

"Siku neema ya kuweka alama kwenye makaburi ya watu waliokuwa na mawazo bunilizi na yenye tija kwa taifa ikishuka wengi wetu tutatoa machozi kwa kupoteza hazina kubwa hapa nchini.

Tunao wabunifu wa mavazi, majengo, mitambo na mawazo mbalimbali yenye tija kwa kumsaidia mtu mmoja mmoja hadi ngazi ya taifa kupitia mapato/kodi, je? Kupitia Mtu mmoja mmoja, Serikali au watu binafsi (kampuni) ni nani anampango na watu hawa? (Ni hapa tunapokosea).

Kwanini nayasema haya;
Tumekuwa waumini wa ajira za moja kwa moja kutoka serikalini au kwenye taasisi binafsi kuliko kuheshimisha ubunifu na ndio maana nchi za wenzetu zimekuwa zikitupiga vikumbo kwenye nyanja za kiuchumi.

Tumeamini kazi ni ile inayoonekana kupitia macho na matumizi ya nguvu kama vile kilimo, kazi za viwandani nk. huku tukibeza matumizi ya akili kwenye ubunifu na kuwaza mawazo ya kuwekwa kwenye matendo ya utendaji.

Kama Wenzetu wangelijikita tu kwenye kuwaza shibe pekee kupitia kilimo na ufugaji au kazi za kuajiriwa moja kwa moja, leo tusingelikuwa na zana bora utendaji, mifumo ya fedha kwa njia ya mitandao, mawasiliano na vyombo vya usafiri kupitia anga, majini na nchi kavu huku wakiendelea kukuza uchumi wao.

Wenzetu mbali na kutowaza vitu vipya wamejikita kwenye "Uboreshaji" wa kilichowazwa na wabunifu wa zamani.

Mfano Uboreshaji/ Ubadilishaji wa magari na pikipiki zenye kutumia nishati ya mafuta kwenda kwenye mfumo wa nishati ya nguvu za jua na kuchaji kupitia umeme.

Mfano mwingine kwenye simu kumekuwepo ongezeko la vipengele mbalimbali kama vile Bluetooth, tochi camera, wireless nk. ( Huu nao ni ubunifu) unaotokana na uboreshaji wa zana za kizamani na kuelekea kwenye usasa tunao uhitaji).

VISABABISHI VYA KUKOSEKANA KWA UBUNIFU HUU HAPA NCHINI. (kwanini tumezika watu na mawazo yao badala ya miili tu, huku familia na nchi zikinufaika na mawazo hayo yaliyoachwa).

1. Ubinafsi; Ubinafsi huu huko kwa pande mbili ambapo mtu anaweza kukataa kutoa Wazo la kibunifu sababu tu atanufaisha kampuni fulani na yeye kutoka kapa. Mfano halisi mtu anaweza kuona shindano la kukusanya mawazo chanya, badala ya kufurahi kuona amepata sehemu sahihi ya kutua mzigo wa wazo la kibunifu lilokuwa likimkereketa ndani yake yeye anawaza kwanza hatimiliki bila hata kuangalia zawadi kwa washindi, sawa anakuwa na hoja ya kulinda kazi yake bunilizi lakini kinacholeta dukuduku ni pale anapoanza kuhoji hivi bila hata kusoma vigezo na masharti (huu ni mfano wa ubinafsi) "Tumezika watu na mawazo".

Pia ubinafsi kwenye taasisi zenye kupokea mawazo, nao unaweza kuwa shida kwani mtu anaweza kutoa wazo bora lakini wakashindwa kumtambua au kumpa stahiki mbunifu hadi kukatisha wengine tamaa, pale atakapo toa wazo kwa muda usio hitajika yaani kuendana na uhitaji uliopo lakini likaja kufaa miaka kumi mbeleni na taasisi ikalitumia yenyewe bila kumfikiria aliyelibuni kwa hiyo miaka kumi iliyopita.

2. Ukosefu wa mitaji na kukatishana tamaa.
Sawa kuwaza mawazo makubwa kunahitaji mtaji mkubwa, mbali na hili kuna baadhi ya watu wanao katisha wenzao tamaa kwa kusema mawazo haya niyawazungu hapa kwetu sisi bado. (kauli hizi ni hasi) kwani mawazo hayo yanaweza kuuzwa hata kwa wazungu na yakaleta faida kwa dunia nzima pia wazazi wamekuwa na msukumo wa kuwakatisha tamaa watoto kwa kuwasukuma zaidi kwenye kufanya kile wanachokiamini wao na kufisha mawazo makubwa ya kibunifu na ndoto za watoto.

NINI KIFANYIKE?
Hapa nchini kunapaswa kuwepo na vitengo/taasisi za kupokea na kuthaminisha kazi za kibunifu kulingana na nyanja husika.

Mfano ubunifu kwenye sanaa na burudani
Michezo;

Kupitia bajeti inayotoka serikalini, Wizara itoe tamko la wazi kila mwaka kuwa kupitia fedha iliyoipata nayo inafungua dirisha la kupokea wazo la kibunifu linaloweza kubadilishwa na kuwa fedha iwe kwa kukuza uchumi wa mtu mmoja au kikundi.

Mfano; Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia
Wao waseme mwaka huu tunamaliza tatizo la upatikanaji wa zana za kufundishia na kujifunzia. Mfano kwa upande wa vitabu.

Hapa watangaze neema kwa vijana wenye vipawa/ Ubunifu wa kuandaa vitabu vya ziada na kiada "waandishi" na waelekeze ni wapi watu hawa watawasilisha kazi zao ili ziweze kupatikana kwa urahisi au hata kuziweka kwenye mfumo wa kimtandao utakao mwezesha mwanafunzi kuzisoma huko huku vikimjenga juu ya kutumia teknolojia na kunumfaishi mwandaaji wa hayo matini kwa zile zitakazo kidhi vigezo.

Vivyo hivyo hata kwenye sekta za Usafirishaji na uchukuzi pamoja na Siasa.

Yaani kila taasisi kila mwaka itenge bajeti ya kukusanya mawazo shindani ya kibunufu yatakayo badilishwa papo kwa papo na kuwa sehemu ya kujiingizia kipato.

"Uwepo wa fursa ya bidhaa ya mawazo" itamfanya kila mtu kuwaza kile anachokiona au kukitumia kwa wakati huo anawezaje kukiongezea manjonjo yapi ili kionekane kama kitu kipya kwenye uso wa dunia.

Maana yangu ni kuwa Tanzania tumefungua maduka mengi kununua bidhaa zinazotoka viwandani tena nje ya nchi.

Leo na sisi tuwe na duka linalotambulika na kuonekana wazi wazi kwa kununua mawazo yatakayozalisha bidhaa yaani tuwe na duka la kununua “AKILI”.

Anayebuni kwenye Elimu amuone nani?

Anayewaza mazuri ya sanaa amuone nani?

Anayewaza mema ya Teknolojia na sanyansi ampelekee nani hayo mawazo ya kiteknolojia.

Ninayo imani kubwa Maduka haya yakiwa wazi kwa kuonekana tutapunguza Makaburi mengi yaliyozika mawazo mazuri yaliyozagaa huku mtaani labda yakibadilishwa na kuzikwa kwenye ofisi ndani ya kanzidata.
 
Upvote 0
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…