Bila mapinduzi ya elimu, Tanzania tuitakayo ni ndoto ya mchana
Yapo mengi ninayoyataka nchini kwetu lakini, hatimaye, Tanzania tuitakayo itajengwa na watoto na vijana wetu na waitakayo wao. Na waitakayo wao itategemea aina ya elimu watakayoipata na kama ni elimu waitakayo kwa ajili yao, familia na jamii zao.
Hivyo, bila kukata mzizi wa fitina, mengi haya wanayoyataka hayawezi kupatikana bila kuwa na mfumo wa elimu unaoendana na hali halisi ya leo, kuanzia chekechea, elimu ya awali na ya msingi. Haiitwi ya msingi kwa makosa. Msingi ukiwa mbovu, nyumba haiwezi kukaa vizuri.
Kimsingi pia, kizazi hiki ni kizazi cha Tehama pamoja na akili mnemba, lakini bado tunaona tehama ni adui badala ya kuitumia na kuwafunza watoto wetu kuitumia vizuri. Si tu inaweza kuwapa watoto wetu fursa ya kuingia katika dunia ya leo, bali pia inaweza kuleta mapinduzi katika bajeti ya elimu ambayo, kwa mfumo huu, haiwezi kutoshelea hata kidogo. Hatutahitaji kujikita kwenye miundombinu kila siku kwenye majengo ya shule hasa kuanzia sekondari na labda hata chini ya hapo, na huenda hatutahitaji walimu wote hawa (ambao daima hatuwezi kuwaajiri wengi wa kutosha). Simu janja sasa zina bei ndogo kuliko hata mshahara wa mwalimu mmoja wa mwezi mzima.
Baada ya miaka mitatu au minne ya elimumsingi (na hata kabla) watoto watafikia elimu kupitia simu janja au kishikwambi kujisomea, kubadilishana mawazo na wenzie na kuandika kazi maalum kulingana na vipaji vyake na makubaliano na mwalimu. Halafu kila shule itageuzwa kuwa 'learning hub' ambapo inasimamia 'personalised learning' ya kila mwanafunzi badala ya kuwarundika wanafunzi wote darasa moja kwa kutegemea wako kwenye kiwango kimoja na vipaji vya aina moja.
Aidha, watoto watajifunza kutumia fikra tunduizi katika kutofautisha kati ya ukweli na mawazo na/au mihemko ya mtu, wapi mtu ametia chumvi au hata pilipili kichaa, wapi amesema uongo n.k. na kuweza kutoa hoja zake vizuri. Badala ya kupiga marufuku matumizi ya simu shuleni, wanafunzi watafundishwa jinsi ya kuzitumia vizuri.
Hadi sasa, tatizo kuu ni kwamba labda elimu ni kitu pekee duniani ambayo ni supply driven moja kwa moja. Kwa kuwa shule zimejengwa na mitaala imetengenezwa (hasa na watu wa kizazi cha juzi) basi ni lazima kila mtoto apitie humuhumu, bila kuzingatia kama chakula cha ubongo wanachokipata na mazingira wanamosoma vinafaa au la. Kwa kutumia tehama, itawezekana kuwa na unyumbufu katika kukidhi mahitaji na matakwa ya watoto.
Pamoja na hayo, inabidi kuwa na mfumo wa elimu unaozingatia kwamba miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto ni muhimu kuliko yote katika ukuaji wake kimwili, kiakili na kiroho. Upande wa kimwili, Tanzania bado ina kiasi kikubwa cha udumavu wa watoto unaowaathiri kimwili na kiakili maisha yao yote. Hali hii haisaidiwi na ukweli kwamba ingawa wanakaa katika chekechea na shule za awali saa nyingi, mara nyingi hawapati chakula. Pili, kama anavyotoa hoja Ken Robinson na wengine, watoto wanazaliwa na ubunifu wa hali ya juu unaowawezesha kuelewa na kuishi vema ndani ya mazingira yao. Wanaingia shule na ubunifu huu lakini kwa kiasi kikubwa sana, badala ya kuendeleza ubunifu, udadisi, furaha na akili za kudadisi na kuhoji, shule inaviua.
Hasa hapa Tanzania, tofauti na nchi nyingine kama Finland na Japan zinazojali ukuaji wa mtoto badala ya kulazimisha taaluma toka mwanzo, shule zetu za awali zinaanza kuzingatia taaluma na nidhamu ya watoto wakubwa sana hata kabla hawajawa tayari. Nafasi ya kucheza, kushirikiana na wenzao na kujifunza mahusiano na maadili kwa njia hii ziko haba sana.
Ndiyo maana ubunifu wao, kujiamini kwao vinafinywa sana. Hivyo, kwanza nataka kuona mapinduzi katika elimu ya awali inayozingatia ubunifu na vipaji anuwai vya kila mtoto badala ya kulazimisha usare. Na kipaumbele kitolewe kwa elimu hii ya awali kama msingi wa kupata Watanzania wenye stadi za ubunifu na fikra tunduizi.
Hali hii inapaswa kuendelea katika shule za msingi, hasa miaka ya mwanzo. Na ili kufanya hivyo, tunahitaji kuondoa udikteta wa mitihani ambao unaua moja kwa moja uwezo wa watoto walio wengi kuendeleza vipaji vyao na stadi zao za karne ya ishirini na moja. Inasikitisha kwamba wengi wanaamini kwamba bila mitihani mtoto hatasoma. Hii inaonesha jinsi tulivyoharibu elimu maana watoto wanapenda kujifunza, kuelewa vizuri mazingira yao na kupanua mawazo yao.
Iwapo inabidi tuwalazimishe kusoma kwa vitisho vya mitihani na kuwahukumu wengi kuwa wamefeli, ina maana kwamba elimu yetu ina kasoro kubwa sana. Si kwamba tathmini haihitajiki lakini itafanywa na walimu wenyewe ili wajue watoto wao wanataka nini lakini, sawa na nchi nyingine, mitihani ya taifa haihitajiki kwa umri huu hadi baadaye kabisa.
Tatu, hatuwezi kupata Tanzania tuitakayo kwa kuwalazimisha watoto wetu wasome kwa lugha wasiyoijua. Nataka kuona watoto wote waweze kusoma angalau hadi mwisho wa sekondari ya chini, ni upumbavu kuendelea kung'ang'ania kuwafundisha kwa lugha wasiyoijua. Kufikia elimu si tu kukaa darasani bali ni kuweza kuelewa wanachofundishwa, elimu kwanza si lugha kwanza. Wakifundishwa na kutahiniwa kwa lugha wanayoilewa, watajifunza mengi zaidi, na kujiamini zaidi kutumia walichofundishwa huku wakifundishwa lugha nyingine kama somo, kama wafanyavyo katika karibu nchi zote duniani.
Hayo yote hayawezekani bila kuwa na walimu wa aina mpya, walimu wanaojua kwamba si kazi yao kuwajaza na kuwakaririsha watoto taarifa nyingi za masomo yao, bali kazi yao ni kuwachokoza na kuwawezesha kutafuta wanachokitaka na kukihitaji katika kupanua uelewa, ubunifu na fikra tunduizi zao. Hivyo inabidi wanaojifunza ualimu nao wapewe kozi maalum kwa ajili yao kujenga stadi zao za karne ya 21.
Aidha, kwa kutumia akili mnemba, kazi za kiutawala, na kutathmini watoto itarahishwa sana ili walimu waweze kujikita moja kwa moja kujifunza pamoja na wanafunzi wake. Wanafunzi nao wataweza kuchagua walimu, au kozi mtandaoni vinavyomfaa. Hii nayo itakuwa ni motisha kubwa kwa walimu kuwa bora zaidi, maana bila hivyo watajikuta hawana wanafunzi. Walimu daima watahitajika kusaidia lakini kwa nini wanafunzi wakubali kukaa darasani na mwalimu asiyejua vizuri somo lake, wala mbinu bora za kufundisha wakati anaweza kufuata kozi mtandaoni zilizoandaliwa na walimu bora kabisa?
Hatimaye elimu itakuwa demand driven badala ya supply driven, yenye kuwawezesha watoto kusoma vizuri, kwa mwendo wao na kutumia elimu yao kujenga Tanzania waitakayo.
Upvote
4