By Jenerali Ulimwengu
KATIKA makala za hivi karibuni nimekuwa nikijadili masuala yahusuyo elimu kwa sababu naamini kwamba elimu iliyoratibiwa vilivyo na yenye maudhui ya kimaendeleo ndiyo njia pekee ya kutuondoa katika umasikini ndani ya kizazi kimoja au vizazi viwili.
Elimu ya aina hiyo (pamoja na afya) ndiyo imekuwa tofauti baina ya nchi za Kiafrika na zile za Asia, ambazo wakati tunapata Uhuru zilikuwa sawa sawa na nchi zetu lakini leo zimetuacha mbali. Ukweli ni kwamba nchi kama Malaysia, Korea ya Kusini na Indonesia ziliwekeza katika maarifa na siha ya watu wake wakati sisi tuliwekeza, ama kwa kutokujua ama kutokujali, katika ujinga na maradhi.
Napenda kuamini kwamba hatujachelewa sana, ingawaje hata wakati huu tunaposherehekea miaka 47 ya Uhuru bado sioni mwelekeo wa wazi wa kujikosoa katika jinsi tunavyoenenda. Kwa jinsi tunavyoenenda tutatimiza miaka 50 tukiwa bado tunasuasua, na tusipoangalia nusu karne nyingine ya upuuzi itatukuta bado tupo hapa hapa tulipo au tumerudi nyuma.
Wakati tunaitafakari elimu yetu hatuna budi pia kufanya tafakuri ya dhati juu ya kipengele kingine ambacho kinaambatana na elimu katika kumjenga Mtanzania wa karne hii: Afya.
Miaka 47 iliyopita, wakati Tanganyika inapata Uhuru nilikuwa mtoto wa darasa la saba, na nakumbuka jinsi tulivyoelezwa na Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine wa wakati ule kwamba tulikuwa na maadui wakuu watatu: Umasikini, Ujinga na Maradhi.
Naamini maadui hawa bado tunao, na katika maeneo kadhaa wamekuwa wakali zaidi na wanazidi kututeketeza. Haielekei kama jitihada zetu zimezaa matunda ya kuridhisha, na mara nyingi watawala wetu wanaonekana kama watu wasiokuwa makini katika kuwashughulikia maadui hawa.
Watawala wetu, ama wanawatomasatomasa maadui juu ya magamba yao bila kuwaingia katika undani wao au wanatumia nguvu nyingi mno na maarifa kidogo mno katika kukabili matatizo ambayo yanahitaji tafakuri ya kina kabla ya harakati na mikurupuko.
Sina haja ya kurejea nilichoandika hivi karibuni kuhusu ‘madarasa' yasiyokuwa na waalimu, isipokuwa inawezekana pia kwamba tutajenga zahanati na vituo vya afya visivyo na waganga wala wauguzi.
Hebu tufikiri tena, na labda katika tafakuri yetu turejee misingi tuliyofundishwa, si tu na Mwalimu Nyerere, bali na ukweli unaojidhihirisha katika historia ya dunia katika karne iliyopita, historia ambayo hadi leo tunashuhudia ikiandikwa.
Nchi nilizozitaja hapo juu zilitambua yale yale aliyotufundisha Mwalimu: Maendeleo ya jamii huletwa si kwa kujenga vitu bali kwa kuwajenga watu, na kuwajenga watu ni kuwapa vitu viwili muhimu, elimu na afya. Ndivyo walivyofanya wenzetu wa zamani niliowataja hapo juu ambao leo tunashangaa jinsi walivyotuacha kimaendeleo.
Katika makala zangu za Aprili 1995 nilikumbushia msemo maarufu wa Kilatini, Mens sana in corpore sano (Akili Safi Ndani ya Mwili Imara). Msemo huu unaweza kutafsiriwa kwa maneno mawili: Elimu, Afya. Jamii inayoshindwa kulielewa hili haiendi ko kote.
Ndiyo maana nilishituka niliposoma mahojiano kati ya Rais Mteule wa Jamhuri Benjamin Mkapa na mwandishi (sasa marehemu) David Martin mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 kabla Mkapa hajaapishwa. Alipoulizwa ni katika sekta zipi angetoa kipaumbele, Mkapa alizitaja sekta za madini na utalii, jambo ambalo kwangu mimi lilidhihirisha kwamba tulikuwa na tatizo la msingi.
Dunia ya kisasa (na ya wakati ule), bila kujali mielekeo ya kisiasa na kiitikadi, inatambua (na ilikwisha kutambua wakati ule) hatari za nchi yo yote kutegemea uchumi wa ‘chimba-ondosha,' nikijaribu kupata tafsiri ya ‘extractive industry' ingawaje mbali na uchimbaji dhana hii inaweza kuhusishwa pia na ukataji wa magogo, uvuvi wa samaki na kadhalika.
Leo hii tunashuhudia malumbano makali miongoni mwetu kuhusu uchimbaji huo ambao wengi wanauona kama uwanja wa utapeli na uuzaji wa rasilimali za nchi unaofanywa na watu waliokabidhiwa madaraka kuitumikia nchi yao. Lawama hii Mkapa hawezi kuikwepa, hasa kwangu binafsi kwa sababu nilipata wasaa wa kumweleza na hakuwa na majibu ya kuridhisha isipokuwa tu kuniuliza hizo fedha za kuwekeza katika elimu na afya zingetoka wapi.
Uwekezaji ni uwekezaji, na una gharama zake. Kuwaruhusu wageni waje wachimbe-waondoshe huku wakituachia mashimo matupu na ardhi iliyochuja si uwekezaji ni wendawazimu. Hata mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa uchumi atakwambia hivyo.
Uwekezaji katika elimu na afya ya watu wetu ni uwekezaji wa kweli kwa sababu kilichowekezwa kinabaki nchini na kinakuwa kimeongezwa thamani kubwa na isiyoondosheka. Raia wenye elimu bora na siha imara ni vito vya thamani ambavyo haviwezi kulinganishwa na dhahabu, almasi wala mafuta ya peteroli, vitu ambavyo wakati mwingine vinakuwa chanzo cha vita miongoni mwa wananchi wajinga chini ya watawala walafi.
Hebu tuangalie mifano ya nchi mbili katika eneo letu. Zimbawe inakiona cha mtema-kuni kutokana na ufisadi wa ajabu wa mzee mwenye ugonjwa wa akili. Lakini siku moja ataondoka kwa sababu hata wendawazimu hawaishi daima. Zambia imekuwa na uchumi ‘mzuri' kwa miaka kadhaa sasa lakini wakati ninaandika makala hii habari ni kwamba bei ya shaba imeshuka vibaya mno na kwamba Zambia na DRC zinalazimika kuwaachisha kazi maelfu na maelfu ya wafanyakazi.
Utabiri wngu? Mara yule mzee mwendawazimu atakapoondoka (kwa hiari au kifo) na Wazimbabwe wakajipanga upya wataiponya nchi yao na kuirudishia neema haraka zaidi kuliko watakavyoweza kufanya Wazambia. Sababu? Pamoja na mambo mengine yote, Zimbabwe iliwekeza katika rasili-mali watu, ambao wanachohitaji pekee ni fursa ya kurejea nyumbani. Zambia watakuwa na mashimo mengi, makubwa.
Kama tutakubali kwamba uwekezaji katika elimu na afya ni wa msingi, basi tuikubali ankara yake tukijua kwamba matunda yake yatakuja, na hatuhitaji kusubiri zaidi ya vizazi viwili kabla hatujaona matokeo yake.
Hata tungekopa matrilioni ya dola za Marekani na tukaziwekeza zote katika elimu na afya ya watoto wa nchi hii, hao watoto watakaonufaika na programu hiyo watawezaje kutulaumu kwa kuwaachia deni ambalo linatokana na maendeleo yao ambayo watakuwa wanayaona?
Sasa, nini ni bora kati ya deni la aina hiyo na yale mashimo tunayoyaona huko tulikoruhusu ‘uwekezaji' wa kijuha. Ningependa iwepo fursa kwa watoto wa maeneo hayo kuwauliza watawala wao walikuwa wanafikiri nini wakati wakiwaleta ‘wawekezaji' hao.
Lakini bahati ya watawala wetu ni kwamba wakati maswali hayo yanaulizwa watakuwa wamekufa au wameikimbia nchi. Hapa ndipo itabidi lifanyike zoezi alilolieleza Mwalimu Nyerere, la kufukua maiti zao na kuzichunguza bongo zao ili kujua kama kweli walikuwa na akili timamu.
Kilicho dhahiri ni kwamba watawala wetu wanapenda kufanya ‘uwekezaji' katika mambo ya haraka haraka, yatakayoonyesha faida kubwa mara moja, kimsingi kwa sababu, moja, hawana ‘vision' ya muda mrefu, na pili, wanataka matokeo ya papo kwa papo kwa sababu watanufaika binafsi, kisiasa na kimali.
Tumegeuka nchi isiyoweza kufikiri nje ya vipindi vya miaka mitano kwa wakati mmoja, kwa sababu kinachotafutwa ni madaraka ya kisiasa ambayo yanampa aliyenayo nafasi ya kuiba. Kwa hiyo kila aina ya juhudi, halali na haramu, inaelekezwa katika uchaguzi, na baada ya uchaguzi mmoja yanaanza maandalizi ya uchaguzi unaokuja.
Kwa chama-tawala ndiyo kabisaa, na wala si miaka mitano. Angalia hii: 85 uchaguzi; 87 uchaguzi; 90 uchaguzi; 92 uchaguzi; 95 uchaguzi; 97 uchaguzi; 2000 uchaguzi; 2002 uchaguzi; 05 uchaguzi; 07 uchaguzi; 010 uchaguzi; 012 uchaguzi; 015 uchaguzi; 017 uchaguzi; 020 uchaguzi…
Laiti kama nusu ya muda, nishati na fedha zinazowekezwa katika chaguzi hizi zisizo na mwisho zingeelekezwa katika elimu na afya ya watoto wa nchi hii Tanzania ingekuwa nchi tofauti kabisa. Lakini huko siko yaliko maslahi ya wakubwa.
Itaendelea