Ongezea na hii.... Hakuna kufatiliana kama umefunga kwani kufunga ni kati ya mtu na Mungu na siyo kuwindana nani anakula ili kuchapana viboko na kupeana majina ya ajabu ajabu.
Kati ya misingi muhimu sana ya dini ya kiislamu ni kuamrisha mema na kukataza mabaya:
Allaah ameamrisha jambo hili kwa kusema kati Suurat Aalu Imrani Aya ya 104 ya kwamba:.
{ وَلۡتَكُن مِّنكُمۡ أُمَّةٞ يَدۡعُونَ إِلَى ٱلۡخَيۡرِ وَيَأۡمُرُونَ بِٱلۡمَعۡرُوفِ وَيَنۡهَوۡنَ عَنِ ٱلۡمُنكَرِۚ وَأُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡمُفۡلِحُونَ }
Na liwepo miongoni mwenu kundi (ambalo) linalingania katika kheri na linaamrisha mema na linakataza mabaya.
Na hao ndio walio fanikiwa.
Na katika sura hiyohiyo aya ya 110 Allaah akasema:
{ كُنتُمۡ خَيۡرَ أُمَّةٍ أُخۡرِجَتۡ لِلنَّاسِ تَأۡمُرُونَ بِٱلۡمَعۡرُوفِ وَتَنۡهَوۡنَ عَنِ ٱلۡمُنكَرِ وَتُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِۗ
Nyinyi mmekuwa umma bora walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu".
Na mtume Muhammad
صلى الله عليه وآله وسلم
anasema katika hadithi aliyoipokea Imamu Muslim kutoka kwa swahaba Abuu Sai'yd Al khudry
رضي الله عنه.
Mtume amesema:
" مَنْ رَأَى مِنْكُمْ مُنْكَرًا فَلْيُغَيِّرْهُ بِيَدِهِ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِلِسَانِهِ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِقَلْبِهِ، وَذَلِكَ أَضْعَفُ الْإِيمَانِ ".
Atakayeona miongoni mwenu jambo ovu na alizuie kwa mkono wake, kama hawezi basi ( alikataze ) kwa ulimi wake , na kama hawezi basi ( alichukie ) kwa moyo wake na huyo ni mdhaifu mno wa imani"
Sasa Allaah ameamrisha waislamu wote ambao hawana dharura za kisheria wafunge mwezi wa Ramadhani pale aliposema katika Suuratul Baqara Aya ya 183 ya kwamba :
{ يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡكُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ }
"Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, ( mumefaradhishiwa kufunga )
kama waliyo andikiwa (walivyofaradhishiwa ) walio kuwa kabla yenu ili mpate kumchamungu."
Na katika Aya ya 185 Allaah akasema:
" { شَهۡرُ رَمَضَانَ ٱلَّذِيٓ أُنزِلَ فِيهِ ٱلۡقُرۡءَانُ هُدٗى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَٰتٖ مِّنَ ٱلۡهُدَىٰ وَٱلۡفُرۡقَانِۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ ٱلشَّهۡرَ فَلۡيَصُمۡهُۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوۡ عَلَىٰ سَفَرٖ فَعِدَّةٞ مِّنۡ أَيَّامٍ أُخَرَۗ يُرِيدُ ٱللَّهُ بِكُمُ ٱلۡيُسۡرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ ٱلۡعُسۡرَ وَلِتُكۡمِلُواْ ٱلۡعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ ٱللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَىٰكُمۡ وَلَعَلَّكُمۡ تَشۡكُرُونَ }
Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo (ndani yake ) Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru."
Kwakuwa Allaah kaamrisha waislamu wasiokuwa na dharura za kisheria kufunga, basi ni dhambi na maasi kwa mwislamu asiyekuwa na dharura kula mchana wa Ramadhani na anapoonekana akifanya hivyo katika jamii ya waislamu wengi lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake.!
Ama wakristo na wapagani hakuna mahala wamekatazwa kula kwakuwa tukifanya hivyo hata mbwa, nguruwe,paka ,mbuzi na ng'ombe tutawalazimisha kufunga wakati wao Allaah hajawawekea sheria ya kufunga.