Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Bongo Hapo Zamani:
NYERERE ALIPOONGOZA KIKAO KILICHOIUA TAA NA KUZAA TANU
NYERERE ALIPOONGOZA KIKAO KILICHOIUA TAA NA KUZAA TANU
Kwenye kichumba kidogo kisichokuwa na hewa ya kutosha, Julius Nyerere alikaa kwenye kiti chenye meza. John Rupia alikaa kwenye kiti kingine.
Akina Sykes, mtu na nduguye, wakiwa na Dossa Aziz walihangaika na vilivyomo kwenye mikoba walioingia nayo kwenye chumba hicho.
Julius Nyerere akafungua kikao kwa kusema ametafakari sana kuhusu T.A.A. , lakini, imekuwa vigumu kukibadilisha kuwa Chama cha siasa.
Kwa kauli hiyo, ilimaanisha kuwa T. A. A ilishachimbiwa kaburi. Mwisho wa T. A. A ukawa hapo na T. A. N. U ikawa njiani kuzaliwa.
Siku ya tukio hilo ilikuwa Oktoba 10, 1953. Kikao kilikuwa ni cha T. A. A kwenye nyumba moja pale New Street ( Mtaa Mpya) ambao sasa unaitwa Mtaa Lumumba.
Haya yamo kwenye kitabu ninachokisoma sasa cha ‘ The Making of Tanganyika ‘ kilichoandikwa na mwanamama Judith Listowel.
Maggid,
Zanzibar.
Mwenyekiti Maggid,
Hayo hapo juu yanatokana na mahojiano kati ya Judith Listowel na Mwalimu Nyerere.
Nyumba hii ya New Street ambayo ilikuwa ofisi ya African Association ilijengwa kati ya mwaka wa 1929 hadi 1933 kwa kujitolea wanachama wenyewe kuja kufanya kazi za ujenzi kila Jumapili.
Abdu Sykes anaeleza kuwa yeye akiwa mtoto mdogo alikuwa akifuatana na baba yake kuja pale kila Jumapili.
Haikumpitikia kuwa iko siku yeye na mdogo wake watakuja kuwa viongozi wa chama hiki na watashiriki katika kuasisi TANU kudai uhuru wa Tanganyika.
Katika kitabu cha Abdul Sykes ipo picha ya ufunguzi wa ofisi hii na baadhi ya majina ya waliohudhuria sherehe hiyo iliyoongozwa na Gavanà Donald Cameron.
Katika hii picha waliokaa wa pili kushoto ni Ramadhani Mashado Plantan
Yeye ni kati ya watoto wa Chief Mohosh Mkuu wa Jeshi la Wazulu lililoingia Tanganyika na Herman von Wissman kuja kupigana na Abushiri bin Salim Al Harith na Mtwa Mkwawa.
Mohosh akajajulikana kwa jina la Affande Plantan Tanganyika wakati huu akiwa Mkuu wa Germany Constabulary.
Kaka yake, Thomas Plantan ndiye alikuwa Rais wa TAA aliyepinduliwa na Abdul Sykes na Dr. Vedasto Kyaruzi kuingia madarakani ili kugeuza TAA kiwe chama cha siasa kudai uhuru.
Thomas Plantan
Aliyekuwa akitia shinikizo la kumtoa Thomas Plantan alikuwa mdogo wake Abdillah Schneider Plantan.
Msimamo wa Schneider ilikuwa wakati umefika chama kiongozwe na vijana.
Listowel kawapa jina hawa vijana kawaita "Makerere Intellectuals."
Hawa akina Plantan na Sykes ni ndugu.
Dr. Kyaruzi kwenye mswada wake "The Muhaya Doctor," kaeleza mchango wa Schneider katika kuwaingiza vijana katika uongozi wa TAA.
Hizi koo mbili za Kizulu wazee wao wakitokea Mozambique zilikuwa na nguvu sana katika siasa za Dar es Salaam.
Schneider baada ya uhuru na Mufti Sheikh Hassan bin Ameir kutangaza kujiuzylu siasa ili ashughulike na suala la elimu kwq Waislam alianzisha taasisi inaitwa Daawat Islamiyya (Mwito Kwa Waislam) akiwa Mudir yaani Kiongozi Mkuu, Schneider akachaguliwa kuwa Katibu.
Mashado Plantan ni Mwafrika wa pili kuwa na gazeti "Zuhra," na ndiyo lilikuwa sauti ya TAA na TANU hadi TANU ilipoanzisha gazeti lake, ''Sauti ya TANU,'' mwaka wa 1956.
Yapo mengi.
Historia ya TAA, TANU na historia ya Julius Nyerere inahitaji utulivu kuieleza kwa pande zote za mazingira aliyoyakuta Dar es Salaam 1952 pale alipopokelewa ndani ya TAA na Abdulwahid Sykes.
Kinyume cha haya haitakuwa historia ya TANU kama TANU ilivyokuwa.
Listowel hakupata haya ninayokuelezeni kutoka kwa Abdul sababu ya Abdul kukataa kueleza historia kwa dhahiri yake nimeshaeleza hapa.