Bosi wa WADA Atua Kenya - Je, Riadha Zetu Zitaondolewa Kabisa Kwenye Doa la Doping?

Bosi wa WADA Atua Kenya - Je, Riadha Zetu Zitaondolewa Kabisa Kwenye Doa la Doping?

Ikariiah

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
287
Reaction score
314
Rais wa World Anti-Doping Agency (WADA), Witold Bańka, yuko Kenya kwa ziara rasmi ya siku 3, huku vita dhidi ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku katika michezo ikiwa kileleni mwa ajenda yake.

Bańka aliwasili Nairobi Jumapili na kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na Katibu wa Wizara ya Michezo, Elijah Mwangi, pamoja na Maafisa wa Anti-Doping Agency of Kenya (ADAK) na WADA Africa Office.

Hii ni ziara yake ya kwanza nchini Kenya tangu achaguliwe kuwa Rais wa WADA, na Bańka ameielezea Kenya kama “home of champions” huku akisema lengo kuu ni kuangalia namna ya kuimarisha mifumo na sera za kupambana na doping nchini.

Katika ziara hiyo, Bańka anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais William Ruto, Waziri wa Michezo Salim Mvurya, Viongozi wa National Olympic Committee of Kenya (NOCK), ADAK, Mashirikisho ya Michezo pamoja na Wanariadha wenyewe. Aidha anatarajiwa kuzungumza na Vyombo vya Habari Jumanne baada ya kukamilisha Mikutano yake.

Lakini kwa nini ziara hii ni muhimu kwa Kenya?

Kenya imekuwa na historia ndefu ya changamoto katika vita dhidi ya doping, hasa katika riadha. Mwaka huu, hata hivyo, kulikuwa na hatua muhimu: WADA ilithibitisha kuwa Kenya ilikuwa imetekeleza hatua zilizohitajika za kurekebisha mapungufu yake na hivyo suala la compliance likafungwa bila vikwazo vilivyokuwa vikitishia nchi.

Lakini hiyo haimaanishi mjadala wa doping umeisha. Hapana! Kenya bado ipo kwenye Category A chini ya Athletics Integrity Unit (AIU), hali inayoonyesha kuwa riadha ya Kenya bado iko katika kundi linalofuatiliwa kwa karibu kutokana na historia na kiwango cha hatari ya doping.

Na hapo ndipo ziara ya Bańka inakuwa ya kuvutia zaidi. Je, Kenya imebadilisha mifumo tu ili kukidhi masharti ya kimataifa, au imefanya mabadiliko yatakayoweza kuondoa kabisa mazingira yanayowafanya baadhi ya wanariadha kuingia kwenye kashfa za doping?

Kwa sababu mwisho wa siku, suala si jina la Kenya pekee. Ni kuhusu Wanariadha wanaoshindana kwa uaminifu, rekodi zinazowekwa, medali zinazoshinda na imani ambayo mashabiki duniani wanaweka kwa “Home of Champions.”

ADAK yenyewe imeendelea kuchapisha orodha ya wanamichezo waliowahi kupewa adhabu kwa ukiukaji wa kanuni za doping, ikiwemo kesi zinazohusisha uwepo au matumizi ya vitu vilivyopigwa marufuku, kukwepa vipimo na kuvuruga mchakato wa doping control.

Kwa hiyo, wakati WADA boss akiwa Nairobi, swali kubwa si “Kenya iko clean?” hilo haliwezi kujibiwa kwa kuangalia taifa lote kama kundi moja. Swali ni:

Je, mifumo ya Kenya sasa inaweza kuhakikisha mwanariadha anayeshinda kwa usafi analindwa, anayekiuka sheria anakamatwa, na hakuna mianya inayoruhusu doping kufichwa?

Ikumbukwe Kenya ilichaguliwa kuandaa World Athletics Championships 2029, na hivyo basi kiwango cha uaminifu katika mfumo huu kitakuwa muhimu zaidi.

Je, unadhani Kenya imefanya maendeleo ya kutosha katika vita dhidi ya doping, au bado kuna kazi kubwa kufanywa?

Na muhimu zaidi: WADA ikiondoka Nairobi, ungependa kuona mabadiliko gani yakifanyika ili “Home of Champions” iwe pia “Home of Clean Champions?"
 
Back
Top Bottom