Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania iliyokutana tarehe 8 Mei 2020 imepitisha hatua mbalimbali za kisera zinazolenga kukabiliana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona (COVID-19) katika uchumi. Lengo la hatua hizi ni kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha na upatikanaji wa huduma za fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Hatua za kisera zilizopitishwa ni:
1. Benki Kuu kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania, kutoka asilimia 7 hadi asilimia 6, kuanzia tarehe 8 Juni 2020. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ukwasi katika sekta ya benki.
2. Benki Kuu kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5, kuanzia tarehe 12 Mei 2020. Hatua hii itawezesha kuongeza wigo wa benki kukopa kutoka Benki Kuu kwa riba nafuu, na hivyo kupunguza riba ya mikopo kwa wateja.
3. Benki Kuu kuongeza unafuu kwenye dhamana na hati fungani za serikali zinazotumika na benki kama dhamana wakati wa kukopa kutoka Benki Kuu. Unafuu huo unapatikana kwa kupunguza kiwango cha dhamana kutoka asilimia 10 hadi asilimia 5 kwa dhamana za muda mfupi, na kutoka asilirnia 40 hadi 20 kwa hati fungani, kuanzia tarehe 12 Mei 2020. Hatua hii itaongeza uwezo wa benki kukopa kutoka Benki Kuu kwa unafuu zaidi kultko ilivyokuwa awali.
4. Mabenki na taasisi za fedha kutathmini kwa kina athari zinazotokana na mlipuko wa COVID-19 kwenye urejeshaji wa mikopo, kujadiliana na wakopaji namna ya kurejesha mikopo, na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo itakavyoonekana inafaa. Benki Kuu itatoa unafuu kwa mabenki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi na bila upendeleo
5. Makampuni yanayotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka Shilingi 3,000,000 hadi shilingi 5,000,000, ma kiwango cha akiba kwa siku kwa mteja kutoka shilingi 5,000,000 hadi shilingi 10,000,000. hatua hii inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha za kidigitali katika kufanya miamala mbalimbali, na hivyo kupunguza ulazima wa wateja kwenda katika Mabenki. Aldlia, Mabenki yamehimizwa kuongeza matumizi ya mifumo ya kufanya miamala kwa njia ya kidigitali, ikiwemo matumizi ya mashine za kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki.
6. Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kufanya tathimini ya athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona katika sekta mbalimbali za uchumi na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza madhara ya athari hizo.
Aidha, Benki Kuu inapenda kuufahamisha urnma kwamba nchi yetu ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kuwezesha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Vilevile, wananchi wanahimizwa kuendelea kufanya miamala mbalimbali nchini kwa kutumia Shilingi badala ya fedha za kigeni.
Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kuwashauri wananchi kuchukua hatua na taadhari ili kuepusha kuenea kwa ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona nchini.
Prof. Florens D."A. M. Luoga
Gavana, BENKI KUU YA TANZANIA
12 Mei 2020