Brazil inakuja Tanzania na inatarajiwa kucheza na timu ya taifa Taifa Stars katika Uwanja wa Taifa hapo Juni 7 wakati wa usiku. Brazil inapanga kutua Dar es salaam usiku wa Juni 6.
Mipango ya kuja Brazil pengine ni ya muda mrefu, kwa vile Tanzania ilikuwa na kiu ya kujiweka katika jukwaa la kimataifa la soka kwa kutumia fainali za Kombe la Dunia za huko Afrika Kusini.
Inaeleweka Tanzania imeunda kikosi kikubwa cha watu maarufu na wenye fedha ili kutafuta fursa mbali mbali za kuitangaza Tanzania. Katika hilo Tanzania imetengeneza machapisho yenye taarifa za vivutio vya kitalii ambayo yatasambazwa Afrika Kusini kuanzia wakati huu.
Lakini ilikuwa ni kiu ya Tanzania kupata timu ya kuja kucheza Dar es salaam au kufanya mazoezi. Zilijaribiwa nyingi, nyengine zikiwa zimewahi kucheza Dar es salaam kama Cameroon na Ivory Coast kwa upande wa Afrika na nyengine za Ulaya.
Ila hakuna aliyeitupia jicho kwa mfano Korea Kaskazini, ambao hadi sasa wanashikilia kwa kasi msimamo wao wa Ujamaa, kwa sababu ingawa ingekuwa rahisi kuwapata, lakini wasingeleta sifa na ujiko ambao Tanzania inautafuta.
Brazil, Brazil, Brazil ndio ikawa lengo, ila ingepatikana vipi. Kocha wa Tanzania Marcio Maximo akaruka mpaka nchini kwao katika likizo yake na akajaribu kuifanya kazi hiyo. Mguu hapa na mguu kule.
Akasema ingekuwa vigumu na haiwezekani hasa. Alitoa sababu za kiufundi ambazo sote tulikubali. Maana timu kama Brazil kwenda pahala hata urefu wa majani ya kiwanja cha mazoezi hupimwa seuze mahitaji mengine mengi.
Alichosema Maximo ni kuwa Brazil wasingeweza kuja maana hali ya hewa ya Dar es salaam haitafanana na ile ya kituo chao katika kundi lao huko Afrika Kusini.
Nikakutana na Maximo uso kwa uso, na akaniambia hay ohayo, na kunihakikishia kabisa haitawezekana.
Ila aliniambia jengine pia. Kuwaleta Brazil ni gharama kubwa sana na hakuwa na hakika kama Tanzania ingeweza kuthubutu kufanya hivyo.
Na mimi nilikubali hilo kwa sababu huko nyuma nilijaribu kuileta Brazil. Nina maajenti walioko Austria ambao wana viungo muhimu katika ulimwengu wa soka na walinipa ofa hiyo na mie nikaitupa kwa Shirikisho la Soka la Tanzania TFF.
Brazil walidai kulipwa dola milioni moja kwa kucheza mechi moja. Hiyo ni mbali ya tiketi za wachezaji na maafisa lakini pia watu wengine kadhaa. Kwa ujumla kawaida msafara wa Brazil huwa watu 60 hivi.
Leodgar Tenga Rais wa TFF akaanza kuhesabu vidole. La haitawezekana aliniambia. Kabisa haiwezekani. Maana kwa maana hiyo ya gharama zitazohusika basi ni wazi kuwa kiingilia cha chini kitabidi kiwe kikubwa kiasi ambacho cha kutisha na kiingilio cha juu kitakuwa kikubwa kiasi cha kuwa kufuru.
Na Tenga ameshaanza kusema hivyo hivi sasa. Kuwa wadau wa soka wajue kuileta Brazil ni gharama ambayo mzigo wake watabidi waubebe wao.
Huko nyuma Tenga na TFF pia walikataa ofa zangu kadhaa kuleta timu za Amerika Kusini hasa na sababu siku zote ikiwa ni gharama- yaani vipi mchezo utalipa. Nitakupeni mifano ya timu kama hizo.
Kulikuwa na jaribio nilofanya ya kuileta timu ya Paraguay ikashindikana. Nikajaribu Bolivia ikawa hivyo hivyo. Pia nimejaribu timu za Ulaya Mashariki.
Niliwahi kuwaambia TFF kuwa hata siku moja hatutaweza kuipata timu ya Ulaya kuja kucheza bila ya mchango wa makampuni. Kwa kutarajia viingilio tu hatutaweza kupata fedha za kutosha kulileta kundi la nyota ambao huunda timu za taifa za Ulaya.
Wakati huo pengine walikuwa na sababu kwa pembeni kukataa ofa hizo kwa kuwa sikuwa wakala rasmi wa mambo ya soka. lakini sasa nina kibali rasmi cha fifa kufanya kazi kama hizo.
Sasa tunaambiwa Brazil inakuja. Inakuja kwa kupitia Afrika Kusini.Hapa inabidi tujiulize suala moja kubwa sana. Inakuaje timu ishafika Afrika Kusini ambako ndio lengo lake kisha tuitoe huko na kuileta huku.
Tunaambiwa Brazil inakusudia kucheza Tanzania na baadae Zimbabwe katika programu ambayo hatukuwa tumeisikia mapema. Timu zote takriban tumejua mapema zinacheza mechi gani, na hakuna hata timu moja iliyopanga kwenda Afrika Kusini kisha ndio itoke kwenda kucheza mechi za kirafiki.
Lakini hayo ni maalesh
tuseme naiwe hivyo. Hebu tutizame basi imekwendaje mpaka Brazil ikaja Tanzania? Hilo limetokezea baada ya Tanzania kwa njia moja au nyengine kukutana au kuijua kampuni inayoitwa kentaro na tembelea
Kentaro - Home utapata mengi.
Kwa ufupi tu Kentaro ni kampuni ya mawasiliano au public relations na ni moja ya zile kubwa duniani na wateja wake ni wale wenye fedha za kupukutika.
Na mimi sikujajua hayo mpaka nilipoona Philippe Huber ndipo akili ilionigonga kwa sababu huyu bwana niliwahi kusoma habari zake kadhaa wa kadhaa katika medani ya soka na ni mmoja ya watu maarufu kama vile wakala wa Kiisrael Pini Zahavi.
Sifa za watu hawa katika mipango ni kubwa sana. Marafiki zao ni marais, mawaziri wakuu na wanasiasa wakubwa wakubwa. Hunywa chai Ikulu na kwenye majumba ya watu wenye ulwa na vyao.
Mwili wangu unatetemeka kama tumba la uvi nikifikiri kiasi gani Phillipe Huber na kampuni yake wamelipwa ili kuwezesha kuipata Brazil kuja kucheza Dar es salaam? Kiasi gani nasubiri watu wengine waniambie kama angalau wanaweza kukisia?
Inaaminika katika dunia ya soka haiwezekani kitu akitake Phillepe Huber Mswisi anayemiliki makampuni kadhaa au huyu Zahavi na kitu hicho kishindikane. Na Huber alipewa kazi na Tanzania na haingewezekana kabisa kushinda kuileta Brazil ukitizama kazi ambazo kampuni yake imezifanya.
Sawa Brazil itakuja itacheza. Mpira wa Tanzania hautapanda kwa kuwa imecheza na Brazil. Wala wachezaji wa Bongo hawatachukuliwa kwenye timu za Ulaya kwa kuwa usiku mmoja wamecheza na Brazil. Wala mimi siamini kuwa Tanzania itakuwa imejitangaza hivyo kwa mechi ya siku moja ambayo nayo imekuja mwishoni mwishoni.
Pengine mtu angejiuliza lipi lingekuwa bora. Kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye soka yetu au kuwaalika watu kuja kucheza usiku mmoja. Hapa ndipo ninapopiga jicho katika sababu halisi ya kuileta Brazil.
Jee si kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi?
makala na Ally Saleh "Alberto" wa BBC