Uchaguzi 2020 Buberwa Kaiza: Vituko na makosa kwenye kampeni za uchaguzi jana Jumatatu 7/9/2020

Uchaguzi 2020 Buberwa Kaiza: Vituko na makosa kwenye kampeni za uchaguzi jana Jumatatu 7/9/2020

M-mbabe

JF-Expert Member
Joined
Oct 29, 2009
Posts
13,203
Reaction score
23,027
Vituko na Makosa kwenye kampeini za Uchaguzi jana Jumatatu 7/9/2020
Kituko: Jana Jumatatu, Septemba 7, maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), walikuwa wanatembelea baadhi ya NGOs ambazo NEC ilizipatia vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura, kutathmini jinsi NGOs hizo zinavyotekeleza majukumu ya kutoa elimu kwa wapiga kura.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Elimu kwa Mpiga Kura namba 13 ya mwaka 2004 kama ilivyonukuiwa kwenye kifungu cha 4C cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343 kama ilivyopitiwa mwaka 2015, NEC inawajibika kwa mujibu wa sheria kutoa elimu kwa wapiga kura.

Kwa hiyo, NEC inapaswa kuwa na uwezo kibajeti, kiutaalamu, ki-organazesheni na ki-operesheni kutimiza wajibu huo wa kuelimisha wapiga kura. NGOs zinapofanya kazi hii huwa zinajitolea kutimiza wajibu huo kwa taifa kwa niaba ya/kuisaidia NEC kutimiza wajibu huo.

Kwa lugha nyingine, NEC inatakiwa kuwa na bajeti kisha kutoa kandarasi kwa NGOs ili ziweze kusaidia kutoa elimu kwa wapiga kura nyakati za uchaguzi au kuboresha Daftari la Kudumu la wapiga Kura.

Sasa jambo la kushangaza, NEC ilitoa vibali kwa NGOs ambazo hazina utaalamu, uzoefu wala bajeti za kuandaa na kutoa elimu kwa wapiga kura. Kwa makusudi kabisa NEC ilizinyima vibali NGOs zenye uzoefu, utaalamu na bajeti ya kutimiza wajibu huo.

Kama hiyo haitoshi, NEC ilizionya vikali na kuziasa NGOs ilizozipatia vibali kutoshirikiana kwa namna yoyote ile na NGOs zenye ujuzi, utaalam, uzoefu na bajeti ya kuandaa na kutoa elimu kwa wapiga kura.

Hadi sasa NGOs zenye vibali zimeshindwa kutimiza wajibu wake kutokana na kukosa ujuzi, utaalamu, uzoefu na bajeti. Sasa katika ziara za maofisa wa NEC 'kukagua' NGOs walizozipatia vibali, wamekuta NGOs hizo hazijafanya kitu chochote. Ni dhahiri maofisa hao wa NEC watakuwa wamelipwa posho kwenda kukagua shughuli za NGOs ilhali wakijua walikwenda kukagua/kuona kisichokuwepo.

Ajabu: maofisa na viongozi wa NGOs hizo walipowaeleza maofisa wa NEC kuwa NGOs zao zimeshindwa kutimiza wajibu wa kuandaa na kutoa elimu kwa mpiga kura, maofisa hao walitishia NGOs hizo kuwa NEC itazichukulia hatua za kisheria (kuzishitaki mahakamani) kwa kushindwa kutumia vibali vya NEC kuandaa na kutoa elimu kwa wapiga kura!

Kwa wanaojua nadharia ya 'reverse dependence' ndio hiyo imeonekana mubashara.

Makosa ya Kimaadili (rushwa) kenye mchakato wa uchaguzi

Jana nilipata bahati ya kuwasikiliza viongozi wawili wa kitaifa wakifanya kampeini za chama chao, kuomba wananchi wawapigie kura wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia chama chao.

Kuna jambo moja, kosa la kimaadili (rushwa) limejitokeza kwenye kauli za wawili hao. Wametaka wananchi kuchagua wagombea kupitia chama chao kwa kuwa mwaka huu wa fedha (2020/21) serikali tayari imetenga bajeti ya kujenga daraja refu (kiranja mmoja amesema hivyo), na mwingine akasema kuwa serikali imetenga bajeti ya shilingi za Tanzania zaidi ya bilioni moja kumlipa mtaalam mshauri (mkandarasi) kutathnini/kupembua na kushauri Serikali namna ya kusambaza maji katika vijiji vyote vya wialaya/jimbo husika.

Tafsiri ya kauli hizi ni kwamba mipango na fedha za bajeti si mali ya umma bali ni mali zao binafsi au chama chao. Kwa hiyo wanashawishi wananchi wapigie kura wagombea wa chama chao ili viongozi hao 'wawasidie' wananchi kwa kuwajengea daraja refu au kusambaza maji kwenye vijiji vya jimbo/wilaya husika.
Hili ni kosa la kimaadili kwa sababu:

1. Bajeti ya Serikali ni mali ya umma siyo ya chama fulani au wagombea binafsi.

2. Sheria ya Uchaguzi, Maadili ya Vyama vya Siasa na wagombea vinaharamisha vitendo vya aina/namna hii vya kubinafsisha na kutumia rasilimali za umma kwa manufaa binafsi wakati wa kampeini za uchaguzi.

3. Matamshi ya mabwana na mabibi hawa ni vitendo vya rushwa katika uchaguzi.

4. NEC ina wajibu na mamlaka chini ya sheria kuchukua hatua za kuwajibisha wahusika.

5. Sisi wananchi ndio wenye mamlaka ya kuchagua na kukasimu madaraka ya kuongoza nchi kwa viongozi. Wagombea wasipowajibika au NEC kuwawajibisha, wananchi tunawajibika kuwawajibisha moja kwa moja. Makala haya ni hatua mojawapo.

Ahadi ya 6 ya mwana TANU : Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.

Ninakutakieni kampeini njema na uchaguzi wenye haki, amani na usalama.

Buberwa Kaiza (ForDIA)
 
Hii waione wanaoitwaga "mabeberu"!
 
Back
Top Bottom