Nimesoma sehemu kuwa ndege aina ya Bundi, licha ya kuhusishwa na imani za kichawi kama mikosi, mtu kufariki akionekana au kusikika akilia jirani, kutokea ghafla nk eti si kweli kwamba ni mchawi bali ana uwezo wa kunusa mtu aliyekaribia kufa.
Je, ukweli wake ni upi?
Je, ukweli wake ni upi?
- Tunachokijua
- Bundi ni nani?
Bundi ni moja ya aina ya ndege wawindao, huishi kwa kutegemea kula nyama, huwinda chakula chake wakati wa usiku hasa wakati wa giza ili kuepusha ushindani dhidi ya ndege wengine walao nyama kama vile mwewe na tai, pia hii humsaidia kukamata wanyama hawa kwa urahisi usiku wakiwa wamelala.
Mara nyingi bundi huutumia mchana kwa mapumziko.
Sifa za bundi na tabia zake
- Bundi huwinda wanyama wadogo wadogo kama vile: panya , mijusi, ndege na wadudu
- Bundi jike huwa na umbo kubwa zaidi, rangi yake imekoza zaidi na huwa mkali kuliko dume.
- Bundi jike huwa na uwezo wa kutaga mayai yapatayo 12, lakini kwa mara nyingi hutaga mayai 4 – 8 yakipishana siku moja hadi mbili.
- Bundi wana uwezo wa kuishi mabara yote isipokuwa bara la Antaktika, bundi waishio kwenye maeneo yenye baridi huwa na maumbo makubwa zaidi wakilinganishwa na wale wanaoishi kwenye maeneo yenye joto.
- Bundi mkubwa ana uwezo wa kumuwinda bundi mwenye umbo dogo wa aina(spices) nyingine, yaani cannibalism.
- Bundi ana uono wa mara saba (7) ya uono alionao binadamu, lakini pamoja na sifa hiyo hawezi kuona vitu vilivyo karibu, hivyo bundi hatumii macho kuvamia windo lake, ana uwezo wa kukamata windo lake akiwa amefumba macho
- Kichwa cha mviringo na macho yake yenye uwezo wa kuyafumba na kuyafumbua kama binadamu, umbo lake na rangi yake, mwonekano wa kichwa chake uwezo wa kugeuza kichwa chake pande zote kwa nyuzi 270° pasipo kuhusisha mwili mzima.
- Bundi hupaa kimyakimya bila ya mabawa yake kupiga kelele, hii ni kutokana na umbo la mabawa yake na mfumo wa manyoa, manyoa yaliyopo miguuni mwa bundi hufyonza kelele zitokanazo na upepo, hivyo kuzuia kelele akiwa anapaa. Zaidi soma Mfahamu Bundi
JamiiForums imepitia tafiti mbalimbali kuhusu maisha ya ndege aina ya bundi na imejiridhisha kuwa imani za uchawi au bundi kuhusishwa na vifo pamoja na mikosi ni imani potofu, bundi si mchawi wala hana mahusiano na mikosi wala vifo vya binadamu.
Moja ya tafiti imefanywa na mtafiti kutoka Taasisi ya Kudhibiti Viumbe hai Waharibifu katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Nicolaus Mwakalinga ambaye ameeleza kuwa imani zinazohusishwa na bundi ni uzushi na potofu na yeye amegundua bundi wana faida nyingi kwa binadamu ikiwemo ulinzi wa mazao shambani dhidi ya panya kutokana na uwezo wao wa kula panya saba hadi 12 kwa siku mbili hadi tatu. (Soma zaidi: Utafiti wa bundi wa chuo Kikuu SUA)
Baadhi ya maswali yanayozalisha imani Potofu kuhusu bundi
Kwa nini Bundi hutokea ghafla(kichawi)
Bundi hatokei ghafla ila huja bila kugundulika kirahisi kutokana na kupaa kimyakimya bila ya mabawa yake kupiga kelele, hii ni kutokana na umbo la mabawa yake na mfumo wa manyoa, manyoa yaliyopo miguuni mwa bundi hufyonza kelele zitokanazo na upepo, hivyo kuzuia kelele akiwa anapaa.
Pia rangi za manyoya ya bundi hufanana Sana na mazingira yake hivyo kumfanya bundi asionekane kwa urahisi hasa wakati wamchana, na ikitokea mtu kamuona hudhani katokea ghafla hali ya kuwa anaweza kuwa alikuwepo hapo kwa muda mrefu nyuma.
Pia bundi huweza hukaa kwenye tawi la mti au sehemu nyingine bila kutingishika hivyo kuonekana kama kiumbe kisicho na uhai kama vile jani la mti au kisiki hali ambayo hufanya watu wasimuone kwa wepesi na ikitokea kahisi hatari huweza kutikisika au kutoa mlio ambao huwaogopesha binadamu na kuhisi katokea kichawi wakati huo.
Bundi hulia usiku na kuleta mikosi
Mlio wa bundi usikikapo usiku sio mkosi kama wasemavyo watu wengi, kama ilivyo kwa ndege wengine bundi hutoa mlio kwa ajili ya mawasiliano baina yao hii inaweza kuwa; kuitana, kuogopa, kumtishia au kumkimbiza adui na sababu nyingine ziwafanyao ndege wote kutoa milio.
Bundi hulia usiku kwa kuwa ndio muda ambao yeye huutumia kufanya shughuli zake za uwindaji, hasikiki mchana kwa kuwa mchana huutumia kama muda wake wa kupumzika(kulala) ivyo kulia kwake hakuna mahusinao na imani hizo potofu bali ni maisha yake ya kawaida kama ndege wengine.
Kwa nini bundi akionekana mara nyingi mtu hufariki eneo hilo?
Bundi ana uwezo mkubwa sana wa kuvuta harufu ya mzoga kutoka mbali. Uwezo huu wa kunusa harufu unapita uwezo walionao binadamu.
Hivyo inapotokea katika nyumba fulani kuna mgonjwa mahututi ambaye seli za mwili wake zimeshaanza kufa lakini mapigo ya moyo bado yanafanya kazi; Bundi huweza kunusa harufu ya seli hizo, harufu ambayo binadamu hawawezi kuihisi, na hivyo huvutiwa kuisogelea kwa ajili ya kujipatia chakula, ila hataweza kuingia ndani kwa kuhofia binadamu.
Aidha, maneno ya Makheya, Afisa kutoka Taasisi ya TAWA wakati akizungumza na Nipashe kwenye maonesho ya Sabasaba, Julai 5, 2023 yanayosema "Huyu ndege ni ndege kama walivyo ndege wengine, kama nilivyosema ana uwezo wa kunusa seli zilizokufa kwa maana ya chakula, wakati anatafuta chakula......Kama kuna mgonjwa au mgonjwa ambaye yupo kwenye hatua za mwisho anauwezo wa kunusa harufu ya seli zilizokufa" yana ukweli.
Kwa kawaida binadamu hafi mara moja, bali hufa hatua kwa hatua (mchakato).
Huwa zinaanza kwanza kufa seli za mwili, baadaye ogani mbalimbali za mwili. Ogani za mwisho kufa ni moyo ikifuatiwa na ubongo. Hivyo bundi anapoonekana kwenye nyumba yenye mgonjwa mahututi ni dalili kwamba mgonjwa huyo ameshaanza hatua za kufariki, na hivyo uwezekano wa mgonjwa huyo kufariki siku za karibuni ni mkubwa sana.
Inapotokea kwamba mgonjwa amekufa baada ya bundi kuonekana, tafsiri sahihi siyo kwamba kifo kimesababishwa na bundi bali ni kwamba dalili za kifo cha mgonjwa huyo zimetambuliwa na bundi.
Hivyo cha kufanya siyo kumtafuta mchawi.
Pia soma: Bundi hunusa seli za aliyeanza kufariki