Bunge la 12 Mkutano wa 16 Kikao cha 5, Septemba 2, 2024 Asubuhi

Bunge la 12 Mkutano wa 16 Kikao cha 5, Septemba 2, 2024 Asubuhi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Serikali imetenga shilingi Bilioni 31 ili kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo.

Amesema fedha hizo zitaiwezesha TARI kufanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu itakayowezesha kilimo cha kisasa kwa wakulima, kufanya ununuzi wa vifaa vya kisasa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa maabara na watafiti ili kuwawezesha kubuni teknolojia zitakazosaidia kakabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye afya ya udongo na mbegu zitakazostahimili ukame, wadudu na magonjwa.

Wizara ya habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Naibu Waziri wa habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari, MaryPrisca Mahundi amesema serikali inaendelea kutafuta njia bora zaidi ya kuruhusu watoa huduma za usajili wa laini za simu kuweza kuwafikia wananchi bila kuathiri viwango vya usalama na udhibiti.

Mahundi ametoa kauli hiyo leo bungeni Dodoma mara baada ya Mbunge wa Makete Festo Sanga kuhoji haja ya serikali kusitisha usajili wa laini za simu kiholela mitaani na badala yake watu wajisajili kwenye maduka maalum ya mitandao ya simu kama nchi jirani wanavyofanya ili kudhibiti utapeli ambao umekuwa ukiumiza na kugharimu watanzania.

"Lengo ni kuhakikisha usalama na uthibiti ubora wa huduma hizi. Tutaendelea kutafuta njia bora zaidi za kuwaruhusu watoa huduma kuwafikia wananchi bila kuathiri viwango vya usalama na uthibiti." Amesema

Hoja za Wabunge
Mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi (CCM) Noah Lemburis Saputi amesema ipo haja ya wataalamu wanaoandaa vigezo vya ajira kuangalia hali za Watanzania kwani kigezo hicho hakiko sawa huku akitaka serikali kujiridhisha umri wa Mtanzania mwenye uhalali wa kuajiriwa.

Saputi ameyasema hayo wakati akichangia hoja ya dharula iliyoombwa na mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ng’wasi Damasi.

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kushauriana na vyama vyote vya siasa, itaandaa kanuni za maadili ya uchaguzi kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

Nderiananga amesema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Neema Lugangira ambapo alitaka kufahamu ni lini kanuni za maadili ya uchaguzi zitakuwa tayari baada ya makosa ya ukatili wa kijinsia kuongezwa kwenye sheria za uchaguzi Februari, 2024.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 kinaeleza kuwa, Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa itaandaa kanuni za maadili ya uchaguzi; aidha, kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 1.2 ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za mwaka 2020, maadili ya uchaguzi yatatumika katika uchaguzi mkuu na katika chaguzi ndogo,” amesema Nderiananga.
 
Back
Top Bottom