Nami naona nijadili machache juu ya bajeti:
"Mheshimiwa Spika, ili kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta nchini, Serikali imeamua kufanya mapitio ya namna ya kukokotoa tozo zinazotozwa na Mamlaka mbalimbali kwa lengo la kuzipunguza na zoezi hili litakamilika katika mwaka wa fedha 2011/12."
Hizi ni blabla za kisiasa tu. Yaani mapitio na namna ya kukotoa ndiyo yatakamilika 2011/2012, siyo urekebishaji wa tozo hizo! Hivyo bei ya mafuta uko pale pale
".kuingiza sekta isiyo rasmi kwenye mfumo wa kodi;"
Hata kwa tafsiri ya neno lenyewe (sekta isiyo rasmi) ina maana ya sekta isiyo na utaratibu rasmi. Hawana kumbukumbu, leo wapo kwenye biashara kesho hawapo, hawana maeneo maalum nk. Kwa vyovyote kodi za sekta hii zitakuwa ni za kukadiria tu – hapo ndipo rushwa itakapokithiri. Ebu fikiria unamtozaje kodi mama-ntilie!
Je hatua hii inapunguza ukali wa maisha?
"Maslahi ya Watumishi
68. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kulingana na uwezo wa mapato yake kwa lengo la kuwawezesha kumudu gharama za maisha. Maeneo ambayo yatatiliwa mkazo ni pamoja na malipo ya mshahara na likizo kwa wakati, kuhakikisha watumishi wanalipwa mafao yao mara baada ya kustaafu, pamoja na pensheni zao za kila mwezi. Sambamba na hayo, Serikali itatoa mafunzo kwa maafisa wa Hazina ndogo na wa mahakama zote zinazoshughulikia mirathi, na kuweka mikakati ya pamoja kuwaondolea kero wasimamizi na warithi wa mali ya marehemu."
Watumishi hapa mmepigwa changa la macho. Serikali itaendelea kuboresha maslahi, lakini maeneo yatakayotiliwa mkazo si kuongeza mishahara! Poleni sana. Silaha ya mfanyakazi kuongezewa mshahara si kumbembeleza mwajiri bali kumshinikiza!
"Baadhi ya hatua zitakazochukuliwa, ni pamoja na: kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri; kupitia upya vyanzo vya Halmashauri vilivyofutwa; kupitia mfumo wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo; na kuainisha mianya ya upotevu wa mapato na vyanzo mbadala vya kuongeza mapato ya Serikali za Mitaa."
Hapa waziri anataka baadhi ya vyanzo vilivyofutwa sasa virudishwe. Hii yaweza kuwa kodi ya maendeleo, gharama za leseni nk. Je ametafakari sababu zilizopelekea kuondolewa kwake. Je kuna mabadiliko ya mazingira kwamba zilipofutwa hali ilikuwa hivi na sasa imeboreka kiasi cha kurudisha kodi hizo? Je hii itapunguzaje ukali wa maisha? Kumbuka hapa inaongelewa kodi kwenye halmashauri ambako ndiko wananchi wanaishi!
"Kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa Serikali na wanaofanya kazi kwenye Taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya Serikali.."
Huu ni ubaguzi wa wazi katika bajeti. Fikiria wewe ni mtumishi wa sekta isiyopata ruzuku ya serikali, unakwenda katika semina au warsha au mkutano ambao pia unahudhuriwa na watumishi wa serikali na mashirika yanayopata ruzuku ya serikali. Nyote mnalipwa posho ya Tshs 50,000 kwa siku. Wewe posho yako ihesabiwe kama sehemu ya mapato yako wakati wa kukokotoa kodi ya mapato lakini kwa hao wengine isihesabiwe hivyo! Nyote ni watanzania, mnakula chakula kile kile, mnalala sehemu ile ile. Huu si ubaguzi wa hatari?
"b)Halmashauri za Wilaya zitoze na kukusanya Ada ya leseni ya biashara ya shilingi 30,000 kwa mwaka kwa biashara zinazoendeshwa katika maeneo ya miji midogo na vituo vya biashara."
"c)Halmashauri za vijiji zitoze na kukusanya shilingi 10,000 kwa mwaka kwa kila biashara inayoendeshwa katika maeneo yake."
Ada ya leseni hizi ilifutwa huko nyuma baada ya kuonekana ni kero kwa wananchi. Je sasa sababu za kuifuta zimekwisha? Waziri anaweza kutueleza sababu hizo zimekwisha vipi? Halafu hizi ni flat rate – yaani kwa kila biashara, kana kwamba biashara zote zinafanana! Halafu hapo umepunguza ukali wa maisha!
"84. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura, 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati wa uendeshaji gari barabarani (Traffic Notification Fee) kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 300,000."
Fursa za rushwa zimeongezwa! Hata kama itakuwa ni hiyo 50,000 aliyotamka waziri. Ni vizuri ikawa kila kosa na fee yake badala ya kujumuisha makosa yote. Fikiria mtu ambaye anaendesha pikipiki lakini kwa bahati mbaya amesahau kadi ya pikipiki au leseni nyumbani – fee 300,000! (maana sheria inasema lazima uwe navyo wakati wote iwe mvua au jua) Nadhani pia kuna kasoro kubwa katika utungaji wa sheria. Wanatunga sheria za magari halafu wanazihusisha na pikipiki. Kwa mfano road licence (kwa sheria) inatakiwa ibandikwe kwa ndani kwenye kioo cha mbele! Mwenye pikipiki kioo hicho ni kipi?
Kwa sasa naishia hapo; nitaendelea na uchambuzi kadri muda utakavyoruhusu.