Waungwana, salama!
Kwa mujibu wa hii sheria mpya, unaweza kununua na kuhifadhi vipimio vya ‘HIV’ ndani kwako kwa ajili ya matumizi binafsi na ya kifamilia, wapo wanaopongeza hatua hiyo na wengine kusimama kinyume.
Pamoja na ukweli kwamba suala la maambukizi ya virusi ‘vinavyoweza’ kusababisha UKIMWI (VVU) ni tatizo kubwa, elimu ya kujikinga na kujiepusha na maambukizi mapya bado haipewi uzito unaostahili, hivyo kupelekea kasi ya maambukizi kuendelea kupanda kila kukicha.
Elimu inayotolewa bado haijawafikia walio wengi ukiacha ile kidogo ya awali ambayo wengi tumeipata tungali wadogo sana shule ya msingi, kwa wakati huo tuliamini na kuogopa kweli kweli lakini kumbe ni kwa vile tu tulikuwa hatujaonja asali. Waathirika wakubwa ni ‘watu wazima’ ambao kwa asilimia kubwa hawana tena muda wa kuendelea kupatiwa elimu sahihi hivyo hujikuta katika hatari zaidi ya kuambukizwa na kusambaza.
Kumekuwa na changamoto katika upimaji wa afya kwenye vituo husika, huku ikiripotiwa kuwa wanaume sio wengi wanaojitokeza kwa hiari huku wanawake wakilazimika kufanyiwa vipimo hasa kipindi wanapokuwa wajawazito na hata hao wanaolazimika kupima (ME/KE) inapotokea upenyo wengi wao hukimbia ‘majibu’ au huwa hawapo tayari kujua ukweli.
Sasa kwa sheria hii inaruhusu upatikanaji ‘holela’ wa vifaa vya kupimia VIRUSI, mtu kwa hiari yake ataweza kujipima na kujipa majibu akiwa amejifungia au akiwa na watu ambao mwenyewe karidhia kuwa nao, lakini je elimu inatosha juu ya kupokea matokeo ya vipimo?
Imeshawahi kunitokea mimi enzi za ujana wangu, japo ilikuwa kinyume na sheria ila nilifanikiwa kuwa na vipimio ndani na mara kadhaa nilikuwa naibuka mshindi kwa kutengeneza matokeo CHANYA kabla ya mechi, ila siku moja ikatokea mambo yakasoma ‘kekundu’ kwa huyu ‘mshirika’ ambaye umemshawishi na kumpima. Je, utakuwa katika nafasi gani kumfanya akubaliane?
Tunahitaji elimu, elimu, elimu.
UKIMWI upo, japo umepunguza sifa hivyo umetulia kama vile haupo ila takwimu ziko sahihi.
Pima. Jitambue. Ishi.