Dodoma. Taasisi isiyokuwa
ya kiserikali ya Mwalimu
Nyerere Idealogy
Conservation Society ya jijini
Tanga, imefungua Kesi
Mahakama Kuu ikitaka
kuzuia mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba.
Taasisi hiyo inapinga
mchakato huo wa Katiba
kwa kile inachodai kuwa ni
kasoro zilizojitokeza,
ikiwamo wananchi kukosa
uwakilishi uliotokana na
ridhaa yao, posho kubwa
wanayolipwa wajumbe na
gharama kubwa zilizotumika
katika maandalizi ya Bunge
hilo.
Kesi hiyo ya madai namba
02/2014, ilifunguliwa
Februari 17, mwaka huu
katika Mahakama Kuu Kanda
ya Tanga na mwenyekiti wa
taasisi hiyo, Dk. Muzzammil
Mussa Kalokola.
Washtakiwa katika kesi hiyo
iliyofunguliwa kwa
stakabadhi ya malipo ya
Serikali namba 49803745, ni
Waziri wa Sheria na Katiba,
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), (kwa sasa ni
Frederick Werema) na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo Mwenyekiti wake ni
Jaji Mstaafu, Joseph
Warioba.
Hata hivyo Jaji Werema na
Jaji Warioba wamesema
hawana taarifa za kesi hiyo.
Dk. Kalokola alisema katika
hati yake ya madai kuwa
anataka mchakato huo wa
Katiba usitishwe kwa kuwa
umevunja Katiba iliyopo.
Amesema Katiba ya sasa
imekiukwa katika Muundo
wa Bunge la Katiba na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba
katika utekelezaji wa
majukumu na wajibu wake
wa kukusanya maoni na
kutengeneza Rasimu ya
Madadiliko ya Katiba ibara
ya 98.
Vilevile imeshindwa
kuzingatia hadidu za rejea
kama zilivyoainishwa na
Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba Sura ya 83, alisema
Dk Kalokola.
Dk. Kalokola alifafanua kuwa
Katiba ya sasa imeweka
masharti kadhaa, ikiwamo
utaratibu wa namna ya
kuibadilisha na sheria
nyingine ambazo
zimeanishwa katika ibara ya
98 na Sheria ya mwaka 1984
Na.15 ib.14.
Ibara ya 98 (1) Bunge
laweza kutunga sheria kwa
ajili ya kubadilisha masharti
yoyote ya Katiba hii kwa
kufuata kanuni zifuatazo,
alisema huku akiinukuu
ibara hiyo na kuendelea:
Muswada wa Sheria kwa
ajili ya kubadilisha masharti
yoyote ya Katiba hii
(isipokuwa yale
yanayohusika na aya ya (b)
ya ibara hii ndogo) au
masharti yoyote ya sheria
yoyote iliyotajwa katika
orodha ya Kwanza kwenye
Nyongeza ya Pili utaungwa
mkono kwa kura za wabunge
ambao idadi yao haipungui
theluthi mbili ya wabunge
wote.
Muswada wa sheria kwa
ajili ya kubadilisha masharti
yoyote ya Katiba hii au
masharti yoyote ya sheria
yoyote yanayohusika na
jambo lolote kati ya mambo
yaliyotajwa katika Orodha ya
Pili kwenye Nyongeza ya Pili
iliyoko mwishoni mwa
Katiba hii, utapitishwa tu
iwapo utaungwa mkono kwa
kura za wabunge ambao
idadi yao haipungui theluthi
mbili ya wabunge wote
kutoka Tanzania Bara na
theluthi mbili ya wabunge
wote kutoka Tanzania
Zanzibar. Alisema kwa madhumuni ya
ufafanuzi wa masharti ya
ibara ndogo ya (1)
kubadilisha masharti ya
Katiba hii au masharti ya
sheria maana yake ni
pamoja na kurekebisha au
kusahihisha masharti haya
au kufuta na kuweka
masharti mengine badala
yake au kusisitiza au
kubadilisha matumizi ya
masharti hayo.
Pingamizi limepelekwa
mahakamani kutokana na
tume kushindwa kuzingatia
masharti ya Katiba
yaliyowekwa na ibara hii,
ibara ya 98. Vilevile tume
imeshindwa kuzingatia
masharti ya hadidu za rejea
yaliyowekwa na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba sura
83, alisema.
Kwa mujibu wa Dk Kalokola,
katika kutunga sheria ya
kuunda Bunge la Katiba
Serikali imelipotosha Bunge
kwa kuunda sheria ambayo
haikuzingatia masharti ya
uhalali wa uwakilishi kama
yalivyowekwa na Katiba
hususan ibara ya 21.
Kwa mujibu wa uhalali wa
uwakilishi, Katiba inaweka
masharti kuwa wawakilishi
halali watakuwa ni wale
waliochaguliwa na wananchi
kwa hiari yao, kwa haki na
uhuru kabisa kwa kuzingatia
utaratibu uliowekwa na
sheria au kwa mujibu wa
sheria, ameeleza katika hati
hiyo na kuendelea;
Baya zaidi Mheshimiwa Rais
aliahidi kuwa kwa mujibu wa
sheria uteuzi utalenga
kutengeneza Bunge la Katiba
lenye sura ya utaifa kwa
kuzingatia mahali
wanapoishi wajumbe
walioteuliwa. Kwa uhalisia
wajumbe kutoka Tanzania
Bara, zaidi ya asilimia 75
wanaishi Dar es Salaam.
Dk. Kalokola ameeleza pia
kuwa Serikali iliwapotosha
wabunge kutokana na
shinikizo la wanaharakati
kutunga sheria ambayo
inawapa nafasi wanaharakati
kushiriki katika uamuzi wa
Katiba ambayo wananchi
wangeipenda.
Ifahamike kuwa asasi zote
za wanaharakati zimeundwa
kwa malengo ya kushinikiza
Serikali kukubali matakwa ya
masilahi yao. Baya zaidi
wanaharakati wengine ni
mawakala wa wakoloni
mamboleo kutoka nchi za
nje, alisema.
Dk. Kalokola alieleza kuwa
kesi hiyo imefunguliwa
kupinga posho zilizoahidiwa
kwa wajumbe wa Bunge la
Katiba, kwa kuwa ni kubwa
mno ikilinganishwa kipato
cha taifa.
Tukumbuke kuwa Serikali
imepuuza kuwa ina dhima
kubwa kwa ustawi wa jamii,
na wafanyakazi wengine
kama walimu hawajalipwa
stahiki zao. Serikali
imefanya makosa kutumia
fedha kuwa silaha yetu ya
kupata Katiba Mpya.
Ifahamike kuwa Baba wa
Taifa alisema kuwa ni fikra
potofu kuchagua fedha kuwa
silaha yetu, silaha ambayo
hatuna. Mnyonge hawezi
kuchagua fedha kuwa silaha
yake, alisema.
Ombi mahakamani
Tumeiomba Mahakama itoe
tamko la kuwalazimisha
wahusika kuzingatia
masharti yaliyowekwa na
Katiba katika utekelezaji wa
majukumu na wajibu wao na
kusimamisha Bunge la
Katiba hadi hapo
litakapopatikana Bunge la
Katiba lenye uhalali wa
uwakilishi litakolokuwa
limechaguliwa na wananachi
wenyewe kwa hiari yao kwa
haki na uhuru kabisa,
alisema.
Dk. Kalokola alieleza kuwa
uongozi siyo kazi na Serikali
imekosea kupuuza uzalendo
na kutanguliza fedha. Amesema taasisi yake
inaamini kuwa uteuzi wa
Wajumbe wa Bunge la
Katiba, umelenga
kuwawezesha washikaji
kifedha bila kujali kuwa
wajumbe wa Bunge la Katiba
wanatakiwa wawe na weledi
na uzalendo, ili kufanikisha
Watanzania wanakuwa na
Katiba yenye lengo la ustawi
wa jamii na kujenga taifa
endelevu.
Kwa hiyo basi tumeiomba
Mahakama kutoa amri za
CIETORARI, MANDAMUS na
PROHIBITION (Kuzuia,
kulazimisha na kutekeleza
wajibu) kama ifuatavyo,
alisema na kuendelea;
Itoe tamko la
kuwalazimisha wahusika
kuzingatia masharti
yaliyowekwa na Katiba katika
utekelezaji wa majukumu na
wajibu wao, kusimamisha
Bunge la Katiba hadi hapo
litakapopatikana Bunge la
Katiba lenye uhalali wa
uwakilishi litakolokuwa
limechaguliwa na wanachi
wenyewe kwa hiari yao kwa
haki na uhuru kabisa.
Pia kuilazimisha Serikali
kurekebisha upungufu
uliodhihirika wa ukiukwaji
wa Katiba inayotumika kwa
masilahi ya taifa na
kuilazimisha Serikali
kuzingatia kuwa Rasimu
itakayopelekwa mbele ya
Bunge la Katiba iwe
imeandikwa kuzingatia
weledi na uzalendo bila
kutoa nafasi ya shinikizo
potofu kutoka kwa asasi za
kiraia, amesema.
Kwa kuwa asasi za kiraia
zote zina malengo ya
kushinikiza kufanikisha
masilahi yao, kwa
madhumuni ya kuepuka
mgongano wa masilahi wa
kuhalalisha masilahi ya
makundi kwa jinsi ya
ubaguzi, asasi zitakuwa na
haki ya uhuru wa maoni na
mawazo, lakini hazitakuwa
na haki ya uhalali wa
uwakilishi wa kuwawakilisha
watu ambao hawakutoa
ridhaa kwa asasi hizo kuwa
wawakilishi wao.
Ifahamike kuwa uhalali wa
wawakilishi unatokana na
haki ya wananchi kwa
mujibu wa Katiba kwa
kuchagua wawakilishi wao
kwa hiari yao kwa haki na
uhuru kabisa.
Kwa hiyo asasi za kiraia
hazina haki ya uhalali wa
uwakilishi wa Watanzania na
kutoa amri na maelekezo
mengineyo ambayo
Mahakama tukufu itaona
yanafaa.
Kesi hiyo sasa inasubiri
kupangiwa majaji wa
kuisikiliza.