Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatajwa katika Ibara ya 125 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano ya Mwaka 1977.
Mahakama Maalum ya Katiba inaundwa na nusu ya jumla ya wajumbe watakao teuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na nusu nyingine ya jumla hiyowatakaoteuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Katiba haijataja ni nani Mamlaka ya Uteuzi wa wajumbe) .
Mamlaka yake: Kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake, kutoa uamuzi wa usuluhishi, juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Ibara ya 126).
Katika kutekeleza kazi yake, Mahakama Maalum ya Katiba haitakuwa na mamlaka ya kuchunguza au kubadilisha uamuzi wa Mahakama Kuu au uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliotolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara za 83 na ibara ya 117 ya Katiba. Ibara ya 83 inahusu uamuzi kama mtu ni mbunge halali au sivyo na Ibara ya 117 inahusu mamalaka ya jumla ya Mahakama ya Rufani.
Katiba haipo wazi iwapo Mahakama Maalum ya Katiba inaweza au haiwezi kubadilisha uamuzi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kuhusu jambo lolote.
Ibara ya 128(4) inaeleza yafuatayo ambayo ni masuala magumu kuyatafsiri kwani hayajatekelezwa na Bunge mapka sasa:
" (4) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu utaratibu wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa
Mahakama Maalum ya Katiba, utartibu wa kupeleka shauri mbele ya Mahakama hiyo, utaratibu wa kuendesha shauri katika Mahakama na utaratibu wa kuwasilisha Serikalini uamuzi wa Mahakama Maalum ya Katiba:
Isipokuwa kwamba iwapo shauri lolote litafikishwa mbele ya Mahakama Maalum ya Katiba wakati hakuna sheria yoyote ya aina iliyoelezwa katika ibara hii ndogo, basi shauri litasikilizwa na kuamuliwa kwa kufuata utaratibu utakaowekwa na Mahakama yenyewe kabla ya kuanza kusikiliza shauri, au iwapo Wajumbe wa Mahakama watashindwa kukubaliana juu ya utaratibu huo, basi shauri litasikilizwa na kuamuliwa kwa kufuata utaratibu utakaoamuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar.
Japo zipo kero za wazi za muungano, Mahakama hii haijawahi kuundwa tokea kufikiwa kwa makubaliano ya Muungano. Inaonekana kuwa, , kuundwa kwa Mahakama hii ni kama kuruhusu uwezekano wa wazi wa kuvunjika kwa muungano. Serikali imekuwa ikijiadhari sana kutojaribu kutenda kosa hili la kuwa na Mahakama ya Katiba hapa nchini.
Maoni:
Kwa mujibu wa ibara ya 125 ya Katiba, si kweli kuwa Mahakama ya Katiba ndio iliyopaswa kusikiliza kesi ya aina kama iliyofunguliwa na Mtikila kuhusu suala la Mgombea Binafsi. Kesi hii haihusu tafsri ya Katiba kama Ibara ya 125 inavyoeleza kuhusu majukumu ya Mahakama ya Katiba.
Aidha, Ibara ya 30 (3), (4) NA (5) za Katiba zabainisha:
(3) Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika Sehemu hii ya Sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au
wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano, anawezakufungua shauri katika Mahakama Kuu.
" (4) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii, Mahakama Kuu itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kwa mara ya kwanza na kuamua shauri lolote lililoletwa mbele yake kwa kufuata ibara hii;.........."
5) Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 12 hadi 29 za Katiba hii, na Mahakama Kuu inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni batili au kinyume cha Katiba basi Mahakama Kuu ikiona kuwa yafaa au hali au masilahi ya jamii yahitaji hivyo, badala ya kutamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili, itakuwa na uwezo wa kuamua kutoa fursa kwa ajili ya Serikali au mamlaka nyingine yoyote inayohusika kurekebisha hitilafu iliyopo katika sheria inayotuhumiwa au hatua inayohusika katika muda na kwa jinsi itakavyotajwa na Mahakama Kuu, na sheria hiyo au hatua inayohusika itaendelea kuhesabiwa kuwa ni halali hadi ama marekebisho yatakapofanywa au muda uliowekwa na Mahakama Kuu utakapokwisha, mradi muda mfupi zaidi ndio uzingatiwe" .
Katiba ya saa ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa utangulizi wake ina tamka kuwa
" KWA HIYO, BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BUNGE MAALUM LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, kwa niaba ya Wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.
Kwa maana nyingine ni kusema kuwa, Bunge hili la Kawaida haliwezi kuchukua madaraka "BUNGE MAALUM" kutunga katiba.Haijatajwa ndani ya Katiba, hilo Bunge Maalum ni Bunge gani, linakutanaje na wajumbe wake ni akina nani.
Aidha, ukisoma ibara za Katiba unaona kuwa mamlaka makuu ya BUNGE ni kutunga sheria na si Katiba. Bunge limekuwa likiifanyia kazi hiyo kwa kuweka vilaka katika Katiba kwa utaratibu wa marekebisho ya sheria ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 inayosomeka.
98-(1) Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata Kanuni zifuatazo:-
(a) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na
aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa katika Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote;
(b) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya Sheria
yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya
Pili iliyoko mwishoni wa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao
idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.
Ibara ya 62 ya Katiba inaeleza bayana kuwa:
" 62-(1) Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo litakuwa na sehemu mbili, yaani Rais na Wabunge.
Kwa maana ya kumuhusisha Rais katika Muundo wake, Bunge siku zote haliwezi kuwa huru juu ya maamuzi yake dhidi ya Serikali, achilia mbali Mahakama ambayo watendaji wake ni watumishi wa Serikali kwa uteuzi wa Rais.