Bunge lapitisha Bajeti ya Trilioni 2.74 kwa Wizara ya Uchukuzi 2025/26

Bunge lapitisha Bajeti ya Trilioni 2.74 kwa Wizara ya Uchukuzi 2025/26

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 leo tarehe 15 Mei, 2025 Bungeni Jijini Dodoma.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam kwa kukamilisha upembuzi yakinifu wa Gati namba 8–15 na kuanza ujenzi wa miundombinu ya kupokelea mafuta na matanki 15 yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000 (asilimia 25 ya ujenzi imekamilika).

Pia, maboresho yanaendelea katika Bandari ya Tanga kwa kuongeza kina cha bandari hadi mita 13 na kupanua eneo la meli kuingia, kutoka na kugeuza.

Serikali kupitia TPA inatekeleza mradi wa ujenzi wa gati na Conveyer Belt Bandari ya Mgao kwa ajili ya shehena chafu, huku usanifu wa bandari hiyo ukiwa umekamilika.

Vilevile, upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa Bandari ya kimkakati ya Mbegani–Bagamoyo umekamilika, ikitarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara katika Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Bagamoyo.

==

Bunge la Tanzania limepitisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya Shilingi Trilioni mbili, Bilioni mia saba arobaini na sita, Milioni mia nne themanini na tano na kumi na nane elfu (2,746,485,018,000) kwaajili ya matumizi ya mwaka 2025/26.

Wakati wa hitimisho la Mjadala wa Bajeti hiyo, Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewashukuru Wabunge wote 15 waliochangia Mjadala wa Bajeti hiyo kwa njia ya kuzungumza na maandishi, akiahidi kwamba Wizara yake itayafanyia kazi maoni, mapendekezo na ushauri uliotolewa, ikiwemo kuondoa tatizo la kuchelewa kwa safari za ndege zenye kuendeshwa na Shirika la ndege la Tanzania ATCL.

Awali Wizara hiyo pia imebainisha kwamba kwa mwaka ujao wa fedha, pamoja na mambo mengine itaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa SGR katika ushoroba wa kati, kununua vitendea kazi pamoja na kuboresha reli zilizopo, kuifanyia maboresho ATCL, kuboresha miundombinu na huduma za bandari pamoja na kuendeleza ujenzi wa meli mpya na maboresho ya viwanja vya ndege na Meli zilizopo.

Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson ameipongeza Wizara hiyo kwa wasilisho na majukumu ambayo wamekuwa wakiyatekeleza, akimtakia Waziri na Naibu Waziri wake kila lenye kheri katika kutimiza yale yaliyomo kwenye mipango ya Wizara kwa mwaka ujao wa fedha.
 
Back
Top Bottom