LICHA ya baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuipinga kwa kauli nzito na kejeli hotuba ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2009/2010, imepitishwa kwa kishindo na wabunge wa chama hicho tawala.
Baada ya kutishwa na spika kwamba kwa mujibu wa ibara ya 90, kifungu kidogo cha 2(b) ya katiba ya nchi, rais hataweza kulivunja Bunge isipokuwa kama wabunge watakataa kupitisha bajeti ya serikali , wabunge 221, wote wa CCM, waliipitisha kwa kuitikia ‘Ndiyo', wabunge 33 wa kambi ya upinzani waliipinga kwa kusema ‘Hapana', huku wabunge wawili kutoka Chama cha Wananchi (CUF), wakipiga kura ya kutokuwa upande wowote.
Kupitishwa kwa bajeti hiyo kwa kishindo, kunaweza kuibua maswali mengi kwani tangu kuanza kwa mjadala wa bajeti hiyo, baadhi ya wabunge wa CCM, walionyesha dhahiri kuikamia kwa kutoa kauli nzito na kuapa kwamba kama haitafanyiwa mabadiliko makubwa, hawataipitisha.