KATIBA INARUHUSU LAKINI NI NGUMU SANA BUNGE KUMWONDOA RAIS MADARAKANI
Nawasalimu kwa jina la Chama Cha Mapinduzi,
Leo nimeona nije na hili jambo la kusisimua lililopo kwenye katiba yetu lakini lisilotekelezeka. Halitekelezeki kwa sababu CCM haijawahi teua mgombea mwenye matatizo yasiyo ya kawaida kufikia hatua ya kufikiria kumwondoa madarakani. Lakini kwa upande mwingine tuchangamshe akili zetu na kuona jinsi gani hili suala lilivyo gumu kutekelezeka hasa nyakati hizi CCM ikiwa inaongoza.
Katiba kupitia ibara ya 46A imeweka wazi taratibu za kufuatwa. Imeandikwa hivi;
Ibara ya 46A.-(1) Bila ya kujali masharti ya ibara ya 46 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.
(2) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, hoja yoyote ya kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama inadaiwa kwamba Rais.
(a) ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(b) ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya Katiba, au
(c) amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano, na haitatolewa hoja ya namna hiyo ndani ya miezi kumi na miwili tangu hoja kama hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge.
Baada ya hili azimio la bunge kuna taratibu zimeelezwa hadi kufikia hatua ya Rais kuondolewa. Ugumu uko wapi? Ni kwenye kofia ya pili ya Rais kama mwenyekiti wa CCM. Hapa namaanisha baada ya rais kuondolewa madarakani atabaki na uenyekiti wa chama. Kama aliondolewa kwa fitna basi hao wabunge ambao pia ni wanachama wa CCM watakuwa katika wakati mgumu sana kulikwepa rungu la mwenyekiti.... uwezekano mkubwa ni wengi wao kufukuzwa uanachama. Ikumbukwe mojawapo ya hatua kwenye utekelezaji wa azimio hilo ni uwepo wa taarifa ya maandishi yenye sahihi za wabunge wanaounga mkono. Hakuna kujificha kwa waliohusika. Ila Tukumbuke ibara hii;
67.-(1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo-
(b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa;
Kwahiyo hakuna mbunge atapenda kujiingiza kwenye matatizo ya kuhatarisha ubunge wake kwa kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wake wa chama. Mwisho wa siku hiyo ibara itaendelea kutotumika. Binafsi nawapongeza sana viongozi wa CCM walioamua rais pia awe mwenyekiti wa CCM. Kuvaa hizi kofia mbili kwa mpigo imezuia hatari nyingi sana.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.