Hivi, si hawa hawa wanafamilia waliotuma barua Bungeni ati habari za kifo cha mtoto wao zisiandikwe magazetini, halafu wakati huo huo wanaenda maelezo kuelezea mambo ya ushirikina? Something is very wrong.... Angalia habari hizi ambazo zote ziko kwenye gazeti moja:
1. 2007-07-12 22:02:07 (Nipashe)
Na Mwanaidi Swedi, Dodoma
Familia ya aliyekuwa Mbunge wa Viti- Maalum kupitia Umoja wa Vijana wa CCM, Marehemu Amina Chifupa, imekuja juu ikitaka mpendwa wao asiendelee kuandikwa kwenye vyombo vya habari.
Katika kuhakikisha hilo linatekelezwa, familia hiyo imetuma ujumbe maalum Bungeni, uliosomwa na mmoja wa waheshimiwa wabunge.
Salam hizo za wana familia ziliwasilishwa Bungeni na Mbunge wa Mbinga Magharibi, CCM, Kapten (Mstaafu) John Komba.
Wakati anatoa salam hizo ilikuwa jana yapata saa moja hivi usiku.
Kapteni Komba alifikisha ujumbe huo wakati alipopewa nafasi ya kutoa mchango wake kwenye bajeti ya Wizara ya Miundombinu.
Akasema kuendelea kuamuandika Marehemu Amina Chifupa wakati akiwa tayari ameshatangulia mbele ya haki, ni sawa na kuwakumbusha machungu ndugu na jamaa zake.
Mheshimiwa Amina Chifupa alifariki Juni 26 mwaka huu katika hospitali ya Jeshi Lugalo ambako alilazwa tangu Juni 8 mwaka huu.
Halafu siku moja baadaye,
2007-07-13 10:44:20
Na Lucy Lyatuu
Mzazi wa aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Vijana (CCM), Marehemu Amina Chifupa, ameishauri serikali kuwataja viongozi wanaoshiriki katika sakata la dawa za kulevya ikiwa ni njia mojawapo ya kumuenzi mtoto wao.
Baba wa Amina, Bw. Khamis Chifupa alitoa rai hiyo, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam jana.
Alikuwa akitoa shukrani zake kwa watu walioshiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha msiba wa mtoto wake.
Mapema kabla ya kuanza mkutano huo, waandishi wa habari walisimama kwa dakika moja na kusali na kutoa heshima kwa marehemu ambaye kitaaluma alikuwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa radio.
Alisema familia yake iko tayari kusikia taarifa zozote zinazohusiana na viongozi wanaojihusisha kwa njia moja au nyingine katika sakata la dawa za kulevya na akaiomba serikali kutokuwa na kigugumizi kuwataja wahusika bila kujali nyadhifa zao kisiasa au kijamii.
Hata hivyo, aliishukuru serikali kwa mchango wake ilioutoa katika kipindi chote cha majonzi.
``Tunamshukuru sana Rais Jakaya Kikwete kwa mchango wake alioutoa ikiwa ni pamoja na kutoa ndege yake kwa ajili ya kusafirisha mwili wa marehemu hadi kijijini Ihanjo wilayani Njombe. Hatuna cha kuwalipa ila tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu,`` alisema Bw. Chifupa.
Alisema familia yake haiwezi kusema serikali ichunguze kifo hicho ila kama kuna mtu mwenye taarifa au anayejua mazingira ya kifo hicho anaweza kutoa taarifa kwa serikali ili wanaohusika wachukuliwe hatua.
``Ninatoa kauli hii kwa kuwa wapo wanaosema kifo cha Amina kinahusishwa na kupewa sumu, wengine uchawi kutokana na kupiga vita dawa za kulevya, jambo ambalo hatuna uhakika nalo,`` alisema.
Hata hivyo, alisema katika kumuenzi mtoto wake, familia itaendeleza mfuko wa Amina Foundation na kuwataka watu wote waliokuwa na mapenzi mema na Amina kuuchangia ili uweze kutekeleza ahadi zote alizokuwa amewaahidi.
``Amina Foundation itaongozwa na mjomba wake, Bw. Solomon Mmbanga, akishirikiana na wajumbe wengine kutoka Bungeni na kamati iliyokuwa ikiandaa msiba wake.
Bw. Chifupa alisema yeyote anayetaka kuuchangia mfuko huo atumie akaunti iliyoko katika tawi la CRDB Kijitonyama yenye namba 01J1014153400.
Alisema marehemu Amina alianza kuumwa Mei 8 mwaka huu mara baada ya kwenda nyumbani kwake akitokea kwa aliyekuwa mume wake, Bw. Mohamed Mpakanjia.
Aliongeza kuwa mwanae aliugua maradhi ya ajabu ambapo alikuwa akitaja baadhi ya viongozi kuwa ndio waliomsababishia tatizo la kuugua.
Hata hivyo, kwa kipindi chote Amina alikuwa hali chakula chochote ndipo tulipojua kuwa yalikuwa mambo ya Kiswahili hivyo ikabidi kumhudumia Kiswahili.
Bw. Chifupa alisema baada ya kumpeleka hospitali kuu ya Jeshi ya Lugalo aligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari kilichofikia 400 kikichanganyikana na homa, ambavyo vyote kwa pamoja vilikuwa havishuki.
``Akiwa hospitalini Amina alizungumza maneno mengi (hakuyataja) ya ajabu na mazito mengine yakiashiria kifo chake,`` alisema.
Katika hatua nyingine, Bw. Chifupa alimetoa ruksa kwa wote wanaoendelea kumuandika mtoto wake lakini waandike yaliyo ya kweli peke yake.
Marehemu Amina alikufa Juni 26, mwaka huu saa 8:45 usiku akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo na kuzikwa kijijini Ihanjo wilaya ya Njombe mkoa wa Iringa.