LIKO tatizo, ndani ya Chama Cha Mapinzudi (CCM). Tatizo hili ni la usiri katika kila jambo. Tatizo hili pia liko serikalini na haina shaka chanzo chake ni viongozi wakuu wa CCM ambao ndio wale wale wanaoongoza serikali.
Hili ni la kifo cha Amina Chifupa, ambaye wakati akiugua kuliwa na viji-maneno maneno kuhusu kuugua kwake na hata alifariki, uvumi ulizidi kusambaa kuwa kifo chake kina mkono wa baadhi ya viongozi wa CCM na serikali.
Kauli ya baba yake Amina, Mzee Hamis Chifupa mara tu baada ya kufariki kwa mwanae kuwa kifo hicho kisihusishwe na mambo ya kishirikiana au wauza mihadarati, kwa sababu kimetokana na mapenzi ya Mungu, nayo ilipokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya watu na hata baadhi ya vyombo vya habari ambavyo pengine kwa kutokubaliana naye, viliendelea kuandika habari za utata kuhusu kifo hicho.
Lakini kauli ya karibuni kabisa ya mzee Chifupa, ambayo inatofautina na ile aliyoitoa awali, imezidisha maswali kuhusu usiri uliopo katika kifo cha Amina.
Mzee Chifupa sasa anadai kuwa kifo cha Amina kilisababishwa na ugonjwa wa Kiswahili na kisukari, na kwamba kabla ya kifo chake, alikuwa akiwataja sana baadhi ya viongozi kadhaa.
Ni mzee Chifupa aliyewatangazia Watanzania kuwa amemzuia binti yake kujitokeza hadharani kulipua bomu lililosababisha ndoa yake kuvunjika, na kuwataja watu waliokuwa wakimuandama katika maisha yake. Haina shaka huu ni mlolongo wa kile kinachoitwa usiri, tukizingatia kuwa Mzee Chifupa ni kada wa siku nyingi wa CCM.
Hivyo Amina amekufa na siri nzito moyoni mwake, ambayo kama angepata nafasi ya kuiweka hadharani, huenda leo hii mambo yangekuwa tofauti na ilivyo sasa, kwa sababu wangejua ni nani bingwa wa fitina na majungu ndani ya CCM na serikali.
Ili kuondoa utata wa kifo hiki, tunaishauri serikali, ichukue hatua kukichunguza na viongozi wanaotajwa tajwa kuhusika nacho wawekwe bayana ili nao waeleze wanachokijua dhidi ya Amina.
Vinginevyo, hili la Amina lisipochunguzwa, sisi tunadhani litazidisha shaka ya wengi dhidi ya usiri katika mambo ya hatari na huenda CCM na serikali vikazidi kujiweka katika nafasi mbaya.
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/7/15/tahariri.php