Duru za karibu na rais Pierre Nkurunziza zimethibitisha kuwa kiongozi huyo wa Burundi amefariki baada ya kuambukizwa virusi vya corona.
BBC inatambua kwamba vyanzo vya karibu na rais Nkurunziza vimeuthibitishia mtandao wa habari wa SOS ambao unaendeshwa na wanahabari wa Kirundi kuwa rais huyo alikumbwa na corona.
SOS imekusanya matukio yote ya mwisho ya kiongozi huyo ambaye alidharau ukubwa na hatari wa janga la corona kwa kuruhusu kampeni na uchaguzi wa mrithi wake kinyume cha ushauri wa wataalamu wa afya.
Hivyo kwa mantiki hiyo kiongozi huyo anakuwa wa kwanza wa nchi kufariki kwa corona duniani. Hata hivyo, serikali ya Burundi imetangaza kuwa rais huyo alikufa kutokana na shinikizo la moyo.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, Pierre Nkurunziza aliripotiwa kuwa anatafuta msaada kutoka kwa madaktari wakubwa wa Burundi.
Wale ambao walikuwa karibu na marehemu kabla ya kifo chake, wamekiambia chombo cha habari cha SOS kuwa timu ya wauguzi ilikuwa haijajiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Covid 19.
Walimfanyia vipimo mara tu alipoanza kupata dalili.
Lakini kikosi cha wataalamu wa afya walikutana haraka baada ya hali yake ya afya ilipozorota. Walipambana kupeleka chombo cha kupumulia katika hospitali ya Karusi alipokuwa amelazwa lakini walikuwa wamechelewa tayari.
Mmoja wa wahudumu wa afya ambaye alikuwa anamhudumia rais Nkurunzinza ameripotiwa kuwa na virusi vya corona.
Vivyo hivyo kuna baadhi ya mawaziri walikuwa wanatibiwa ugonjwa huo wa corona katika wiki chache zilizopita.
Serikali ilipuuzia ushauri wa kiafya ambao ulikuwa unasisitizwa kote duniani .
Generali Evariste Ndayishimiye alishinda nafasi ya uraisi Mei 20 na alikuwa anaendelea kuonekana na rais katika mikusanyiko ya maombi na sala.
Lakini hajaonekana tena tangu rais Nkurunzinza atangazwe kuwa amefariki siku ya Jumatatu.
Rais huyo mteule anategemewa kuapishwa mwezi Agosti .
Haijawekwa wazi nani atachukua nafasi ya rais katika kipindi hiki cha mpito kwa sasa.
Katiba inaeleza wazi tu kuwa spika wa bunge ana haki ya kuchukua nafasi hiyo ya rais pale kiongozi anapofariki . Lakini hali inakuwaje kama tayari kuna rais alikuwa amechaguliwa tayari? Baraza la mawaziri limeachia mahakama kuamua.
Source: BBC
Pierre Nkurunziza:Duru za kuaminika zathibitisha kifo cha Rais wa Burundi kimetokana na Covid 19