SoC02 Busara za Babu na Safari ya mjukuu

SoC02 Busara za Babu na Safari ya mjukuu

Stories of Change - 2022 Competition

ChengulaJr

New Member
Joined
Jul 29, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Nilimkuta amejikunyata ndani ya blanketi lake lililokuwa na rangi ya udhurungi, macho yake hafifu yalikua yakilitazama jua, ambalo lilikuwa likitoka huko mafichoni lilikokuwa ili kuja kuungaza ulimwengu, katikati ya mapengo yake ya mbele, alikua amekibananisha kiko chake vilivyo ili moshi wa tumbaku iliyokuwa ikichomeka mbele ya kiko chake, ukafanye kazi iliyokusudiwa mapafuni pasi na kupotea katika ombwe la dunia hii hadaa.

Starehe tulivu ya joto maridhawa la jua la asubuhi lililokuwa likiipasha moto ngozi yake iliyokuwa imegubikwa na makunyanzi, ilisitishwa ghafla na sauti za mlio wa viatu vyangu vya matairi pindi nikaribiapo eneo lile alilokuwa amekaa babu yangu, kabla hata ya salamu za kilugha kuchukua nafasi baina yetu, sauti yenye mikwaruzo iliyoambatana moshi wa tumbaku ilitoka kwenye kona kinywa cha babu yangu na kuuliza "ni wewe mjukuu wangu?", "ni mimi babu", nilijibu huku nikikaa juu ya kichuguu kilichokuwa kando na babu yangu.

Niliamua kuuweka mfuko wangu kuu kuu, uliokuwa na nguo zangu kadhaa zenye viraka vingi pembeni yangu, kwani ukiweka kando busara ambazo nilikuwa nikifunzwa na babu yangu, nguo hizo ndio kilikua kitu pekee nilichokua nikimiliki kwenye maisha yangu.

Baada sauti za ndege mwitu waliokuwa wakikatiza angani kutulia, ulikua ni muda sahihi sasa wa salamu kuchukua nafasi baina yetu. "Kamwene"?, alinisalimu babu kwa kilugha, "kamwene babu, unogage?", nilijibu "..... aaaaah!! ndim'nofu-ela", babu alijibu huku akikitoa kiko chake mdomoni, kama ishara kuu ya kuanza mazungumzo yetu, yaliyokuwa ni tiketi mahbibu ya safari ndefu iliyokuwa mbele yangu. Pasi na kupoteza muda, babu yangu akaanza kuyatanabaisha yaliyokuwa yameujaza moyo wake, huku masikio yangu nayo yakiwa chonjo kwa ajili ya kuanza kupokea busara adhimu ambazo ulimwengu wa sasa umekua ukizipiga teke.

Mjukuu wangu, nakushukuru kwa kuutii wito wangu, nakuja kunisikiliza, nina machache ya kutaka kukueleza mimi kama babu yako, ili usije ukamezwa na ya dunia hii. Tangu ulipoondokewa na wazazi wako, nimekuwa nikikulea, na kwa kudra za yule aliyetuumba, na binafsi ninajivunia kuwa sasa unaiendea safari halisi ya huko dunia iendako, kuwa makini mjukuu wangu kuna mengi sana huko, babu alisema kwa sauti ya upole, kisha babu akaendelea kusema, nimeyaskia mengi yaikumbayo dunia hii mjukuu wangu, nimeyasikia mengi yanayoifanya dunia hii kuwaya waya, nimeyasikia yote mjukuu wangu na kisha nimeyatafakari sana.

Pindi uianzapo safari hii ya kuelekea huko duniani, katu usisahau kuwa dunia imebadilika sana mjukuu wangu na vilivyomo ndani yake vimebadilika pia. Watu wengi utakaowakuta huko wapo kwa ajili ya kuyapigania matumbo yao, hivyo ukifika huko kamwe usiiweke tamaa mbele, utautia aibu ukoo mjukuu wangu.

Hakikisha kuna uhusiano mzuri wa kinywa chako na ufahamu wako, ili usije ukaongea yasiyo na mantiki, utadharaulika mjukuu wangu.

Nimeskia huko uendako kuna taharuki kuu sana, kile chungu kilichokuwa kimehifadhi ile dawa ambayo hapo awali ilikuwa ikidhaniwa ni tiba ya baadhi ya maradhi sugu ya ulimwengu kama wengi walivyokuwa wakidhani, kimepasuka na baadhi ya dawa ile imwemwagika. Endapo kama utapata bahati ya kufika pahala pale kilipo chungu hicho, chonde chonde mjukuu wangu hakikisha haudhuriki na ile harufu itokanayo na dawa ile iliyomwagika, kwani itakulevya na kisha yaweza kuyaharibu maisha yako pasi na kujiuliza mara mbili.

Ile dawa chache iliyosalia chunguni, ni nzuri pasi na shaka. Na watu kutoka pande mbalimbali za uliwengu wamekuwa wakiisifu kwa umashuhuri wake wa kuyaleta mapinduzi ya kitabibu katika nyanja mbalimbali tena kwa namna tofauti tofauti. Lakini mjukuu wangu, si unajua kama kila kilema huja na mwendo wake?, ila nimekuwa na mashaaka makuu na mwendo huu, kiasi kwamba nimeshtushwa na aina ya ulemavu wenyewe.
Mwanzoni nilikuwa na shaka na madhara ya harufu yatokanayo na dawa ile, ila kwa sasa nina mashaka makuu na maradhi ya walimwengu, na ukifika salama mjukuu wangu naomba usisahau kuwauliza walimwengu "kwani ni nani aliyewaroga?".

Nimearifiwa kuwa sasa hivi wanawake kuyaweka hadharani maumbile yao imekua si habari ya kilinge tena, ni dhahiri na ukiwaona hao, shituka mjukuu wangu ila hao usiwasemeshe, dunia itasema nao. Ila, kama jicho lako litafanikiwa kuwaona wale wanaume wavaao na kuenenda kama wanawake, hao usiwaache bure mjukuu wangu, waaambie kuwa "waendako watafika, ila kwa tabu sana".

Najua ukiwaambia hivyo watataka kujibizana nawe kama si kukupiga kwa maneno yao ya kebehi, basi kwa dhihaka kutoka kwenye chembe za mioyo yao midogo, wakifikia hatua hiyo usiwajibu mjukuu wangu, uuchote unyayo wako na kutokomea upesi.

Najua kutokana na chumvi niliyokula, uhusiano baina ya masikio yangu na uhafifu wake katika usikiaji unazidi kukua kwa kasi sana. Lakini hio haikuzuia mimi kusikia kuwa, hata wanandoa nao eti hawana tena muda na familia zao tena, ila wana muda kwa ajili ya familia za mitandaoni, tena siku hizi wameamua kutokuwalea watoto katika njia stahiki kama kutumia viboko wakati wakuwaonya, hawa wazazi ukikutana nao, waulize kuwa "kama na wao wangalilelewa hivyo, je, wangalikuwa hapo walipo leo?", najua hawa hawatakukasirikia, ila watainamisha vichwa vyao chini ili kujitafakari, pindi wajitafakaripo wewe uondoke mjukuu wangu ili ukajionee kundi kubwa la vijana linalotumia muda mwingi kupiga umbea na porojo za mitandaoni, pasi na kuzifikiria kesho zao. Ukibahatika kukutana na vijana hao, waambie babu kanituma niwaambie mambo mawili:-

1. Fainali ni uzeeni.
2. Mitaani kuna uhaba wa ajira, ila kazi zipo za kutosha.
Mjukuu wangu, vijana hawa mara nyingi huwa wanakuwa na hasira kali sana, hivyo hakikisha unakuwa mpole mbele yao ili usidhurike.

Maradhi ya wenyenyi wa huko uendako, ambayo yamesababishwa na ile dawa iliyomwagika kutoka chunguni, na kisha ikatoa harufu mbaya, katu hayatatibika kwa ile dawa iliyosalia chunguni, ila kwa dawa utakayowapelekea wewe, iitwayo ‘ukombozi wa ki-fikra’.

Hapo awali nilidhani dawa ile ingetibu kila kitu, ila la hasha, imetuongezea maradhi mengi sana kwa kizazi hiki cha umbea.

Lakini pia.....(sauti ya babu inakatizwa na mlio wa punda aliyekuwa akinisubiri kando ya zizi la mifugo ya babu kwa ajili ya safari iliyokuwa mbele yetu.), mlio wa punda yule,uliashiria kuiva kwa safari yangu na muda wa kwenda kuyashuhudia yaliyokuwa yakinenwa na babu ulikuwa umewadia.

Nilishuka kutoka kwenye kichuguu nilichokua nimeketi, na kumkumbatia babu yangu kama ishara ya kuagana naye, niliuokota mfuko wangu kuu kuu uliokuwa pale chini, na kuanza kuelekea lilipokuwapo gari lile, huku dani yangu nikijiuliza "KWANINI BABU KAYANENA YOTE HAYA?".

Kwaheri mjukuu wangu, alisema babu na kisha akaiwasha tena tumbaku iliyokuwa mbele ya kiko chake na kuendelea kuivuta.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom