beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,880
- 6,368
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, amesema kuna haja kwa wanataaluma nchini kuanza kuzungumzia mchakato wa katiba mpya kuliko kukaa kimya, kwani ulitumia fedha nyingi.
Aliyasema hayo jana, wakati wa kumbukizi ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliondaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa chuo hicho (Udasa).
“Lazima wanataaluma waendelee kuzungumza kuhusu mchakato wa katiba mpya, zoezi lilikuwa kubwa na lilitumia fedha nyingi, lakini wanataaluma tumekaa kimya, tena nasikitika kusema kuwa mojawapo wa watu waliokuwapo katika mchakato huo ni mimi na mzee Warioba, leo tukipita mitaani tunatemewa mate na kuonwa hatuna jipya,” alisema Butiku.
Butiku ambaye alikuwa akizungumzia mada isemayo ‘mchango wa wanataaluma katika ujenzi wa taifa’, pia alisema wanataaluma wanapaswa kuwa watu wa kutafuta ukweli, kuwa wajasiri na kutambua nchi ilipotoka na inapokwenda.
“Kutafuta ukweli ni wajibu wa kwanza wa wanataaluma, pia wanapaswa kuwa wajasiri wa mioyo na ubongo, hatutaki mtu anakuja kusoma hapa UDSM anakuwa muoga, anapaswa kuwa jasiri,” alisema Butiku, ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kuhusu ajira, Butiku alishangazwa na idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini, lakini upatikanaji wa ajira unakuwa mdogo.
Alisema kila mwaka kunakuwa na idadi kubwa ya wahitimu katika vyuo vikuu, lakini wengi wao wanaishia mitaani, huku wengine wanakuwa wababaishaji.
“Kwa nini wanataaluma mnaandaa wanataaluma wasioweza kujiajiri?” Alihoji na kuendelea:
Tunatoa wahitimu kila mwaka, wanavaa majoho na kofia wanazipeperusha, lakini mmewahi kujiuliza wanakwenda wapi? “Wengi wanakwenda kuishia mitaani bila ajira.”
Butiku aliwataka wanataaluma nchini kuzungumza na kukemea masuala yanayotokea katika uchaguzi nchini, na kueleza kuwa kukaa kimya kutasababisha kasoro hizo kuendelea kutokea kila mwaka.
Naye mwanazuoni kutoka UDSM, Prof. Issa Shivji, akiwasilisha mada ya ‘Nafasi ya wanataaluma katika maendeleo ya taifa: Enzi zilizopita na zilizopo’, alisema enzi za zamani kulikuwa na uhuru wa kitaaluma, walimu walikuwa wanapata ajira, utawala wa chuo ulikuwa unaheshimu wanataaluma, watawala walikuwa wanawalinda wanataaluma, lakini zama za sasa imekuwa kinyume.
Chanzo: IPP Media