Changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi inaendelea kuleta madhara makubwa kwa jamii za Kenya, iwe ni mafuriko wakati wa mvua kubwa, au ukosefu wa chakula baada ya mafuriko kuathiri uzalishaji wa chakula, na hata ukosefu wa umeme baada ya miundombinu ya usambazaji wa umeme kuharibiwa kwenye mafuriko. Bwawa la Thwake lililojengwa na China linatajwa kuwa moja ya masuluhisho muhimu kwa changamoto hizo, na changamoto nyingine kubwa zinazowasumbua watu wa Kenya.
Ujenzi wa Bwawa la Thwake ulioanza mwaka wa 2018 na kukamilika mwaka huu kutoa maji kwa ajili ya kunywa, kutumika kwa ajili ya umwagiliaji, na kuzalisha megawati 20 za umeme. Kutokana na China kuwa na uzoefu mkubwa katika kukabiliana na changamoto za mafuriko katika eneo lake la kusini, na ukame katika eneo lake la kaskazini, kuichagua kampuni ya China kutekeleza ujenzi wa bwawa la Thwake, ulikuwa ni uamuzi wa busara wa serikali ya Kenya. Mabadiliko ya tabia nchi yameleta matatizo mengi kwa Kenya, na changamoto kubwa zaidi imeonekana kwenye hali ya usalama wa chakula na watu kupoteza maisha na mali zao kutokana na mafuriko. Bwana hilo limejengwa ili kuipatia uwezo Kenya kukabiliana na changamoto za mafuriko, na kufanya maji ambayo yangeleta madhara kwa jamii kutumika kwa njia zenye manufaa.
Kwa muda mrefu sasa wakulima wa Kenya kama ilivyo kwa wakulima wengi wa Afrika, kilimo kimekuwa kikitegemea zaidi mvua, lakini wingi wa mvua kupita kiasi, na ukame wa muda mrefu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, vimeathiri sana uzalishaji wa chakula. Hali hii imezusha msukosuko wa usalama wa chakula kwa Kenya, kiasi kwamba katika wakati mmoja, Kenya ililazimika kuagiza cha mahindi kutoka nchi jirani ili kufidia upungufu nchini Kenya.
Ofisa wa kilimo katika kaunti ya Makueni ya Kenya, amesema kwa sasa wana ekari 1,500 zilizo katika hatua mbalimbali kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Kufuatia kukamilika kwa Bwawa la Thwake, kutakuwa na ekari nyingine 100,000 zitakazoendesha kilimo cha umwagiliaji.
Mradi huo uliojengwa na Kampuni ya China Ghezhouba, na kugharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika na serikali ya Kenya, sio tu umejengwa kwa gharama nafuu ilikinganishwa na manufaa yake kwa Kenya, bali pia umekidhi vigezo vya hali ya juu vya uhandisi, na pia unaendana na moyo wa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika kwenye ujenzi wa miundo mbinu. Lakini pia unaendana na ahadi iliyotolewa mwezi Novemba 2022 na Rais William Ruto, aliyeahidi kuwa serikali itajenga mabwawa 1,000 kote nchini Kenya ili kuimarisha sekta ya kilimo na usalama wa chakula.
Mradi huu ni ushahidi mwingine kuwa kati ya wadau mbalimbali wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi duniani, kuna wale wanaotoa ahadi na kauli nyingi kuhusu kuzisaidia nchi za Afrika kuzoea mabadiliko ya tabia nchi. Nchi za magharibi ambazo zimekuwa zikieleza vizuri hatari na changamoto hizo, na kwamba ni nchi hizo ndio chanzo cha tatizo hilo, lakini ziko nyuma au hazitoi mchango wowote kivitendo kwenye kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na matokeo ya tatizo hilo. Bwawa la Thwake ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya China na Afrika, na kati ya China na Kenya katika kukabiliana kivitendo na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.