Badala ya wachangiaji kutoa madukuduku yao ya kisiasa na ya kibinafsi, ni vyema kujiuliza iwapo hii ni mara ya kwanza kwa Rais mpya wa CAF kujua juu ya uanachama wa Zanzibar, tujiulize iwapo kulikuwa kuna upinzani wowote kwenye Kikao cha CAF kilichoipa Zanzibar uanachama, tujiulize iwapo uanachama wa Zanzibar ndani ya CAF ilikuwa ni ajenda mojawapo ya Kikao cha Morocco, tujiulize iwapo Tanzania yenyewe imeilalamikia CAF juu ya Zanzibar kupewa uanachama wa CAF. Ikiwa jawabu ya yote hayo ni hapana (na ndivyo ilivyo) tujiulize basi kulikoni? Natamani tungekuwa na waandishi mahiri wa makala za uchunguzi, wakaanza kazi huku Zanzibar kujua kinachoendelea baada ya Zanzibar kupewa uanachama wa CAF. Kumekuwa na kuwindana baina ya viongozi wa ZFA kiasi cha wengine kufungiwa maisha kijishughulisha na maswala ya soka, kumekuwa na ukaidi wa kurekebisha Katiba ya ZFA ili iendane na matakwa ya CAF, kumekuwa na Utawala usioridhisha wa fedha zinazotoka CAF kiasi cha viongozi kutofautiana, kumekuwa na siasa kwenye ushiriki wa Ligi Kuu ya huku unaolazimisha kila kisiwa (baina ya Unguja na Pemba) kuwe na uwakilishi wa timu, imefikia uamuzi wa kupunguza timu kutoka 40 za mfumo huo wa kisiasa hadi 12 mwafaka na Ligi za CAF umefikiwa kwa kupiga kura, sita kwa kila kisiwa............ Timu kadhaa zilizoathiriwa na maamuzi hayo na kujikuta zikishuka daraja kabla hata ya msimu kuanza hazikuridhika na hilo. Nina taarifa za uhakika kwamba angalau mbili kati ya hizo zimepeleka malalamiko yao CAF.
Sasa kwa kuzingatia hayo, na kwa CAF kubaini kwamba imedanganywa na ZFA (kwa kuwatumia Katiba nzuri ilhali siyo wanayoitumia), na kwa kuzingatia kwamba tangu awali uanachama wa Zanzibar ulikuwa ni hisani zaidi kuliko haki yao, mtu angetegemea CAF ifanye nini kama si kukata mzizi wa fitina? Na baada ya kufanya hivyo mtu ungetegemea CAF itoe sababu zote hizo zitazoonesha udhaifu wake yenyewe ilhali sababu rahisi na ya msingi ipo? Wa kulaumiwa kwa hili ni ZFA yenyewe, na Serikali ya Zanzibar kwa kukubali kudanganywa na ZFA na kwa hivyo isichukue hatua stahiki za kuondoa kasoro zote hizo. Hapo kusingekuwa na swala la Serikali kuingilia soka, bali la Serikali kuitaka soka iendeshwe ki-FIFA na ki-CAF.