Mtani Komba umekwenda kweli? Jina lako lilikuwa kubwa sana. Lilikuwa kubwa kwenye CCM kwa jitihada zako za kutusi, kusimanga na kuwasigina kwa maneno mazito mazito wapinzani wa kisiasa hasa CHADEMA. Ukavuka mipaka ukatukana mpaka wazazi, mzee Warioba ni miongoni mwao. Ulikuwa shujaa mtani katika kutusi na masimango dhidi ya wote usiowataka.
Umaarufu wako ulienda zaidi kwa wale visura. Wengine walistaajabu kwa nini uwadake visura wa namna ile. Mtani wako sina ushahidi wa hawa visura, ni habari za kusikia tu. Ila kuropoka dhidi ya wazee wenye hekima kama Warioba, hakika nilikusikia mwenyewe kweupe kwa masikio yangu. Na yale maneno yako bungeni dhidi ya CHADEMA kuwa wanasema kama wanajamba jamba, hayo nayo niliyasikia.
Umaarufu wako katika kuimba, na sauti nzuri isiyoendana na umbile lako, hakika katika hilo mimi ni shahidi.
Mtani hakika nimesikitika sana kuondoka mtani wangu muda kama huu. Nilitaka uwe hai ili ushuhudie tunavyokuangusha ubunge kule jimboni mwezi wa Oktoba. Nilitaka mtani ushuhudie tunavyokidondosha chama chako, na tukuoneshe wewe na chama chako jinsi nchi inavyotakiwa kuongozwa. Maana raha ya ushindi ni kumshinda mshindani wako akiwa mzima na mwenye afya njema na awepo ili ashuhudie ushindi wako.
Mtani umetutoka, na ndugu zangu waliopo Dar na Songea wana kazi kubwa ya kulibeba jeneza lako na kuliweka kwenye nyumba yako ya milele. Uzito wako siyo mchezo, lazima karibia kilo 200. Maana naamini ule utamaduni wetu ni lazima utafuatwa na CCM na serikali itabidi wasiuvuruge. Maiti lazima ioshe na watani zake. Chakula, mahema, kaburi, sanda na maziko ni lazima watani wasimamie na kutekeleza kikamilifu.
Mtani nikuage namna gani? Komba kwa heri, tena kwa heri ya milele. Hatujui tukuimbie wimbo gani, ziandaliwe nyimbo nyingine au tupige nyimbo zako mwenyewe!
Kwa watoto, ndugu, marafiki na wangoni wote poleni kwa msiba wa mtani Komba. Baba yenu jina lake lilikuwa kubwa, kauli yake kuwa ataingia msituni ilikuwa ndiyo kauli yake nzito ya mwisho ambayo haikueleweka. Matusi yake hatuyakumbuki leo, kejeni na masimango yake hatuyakumbuki leo, madeni yake hatuyakumbuki sisi labda hao CRDB, sisi letu ni moja tunaungana kuomboleza kifo cha mtani Komba, mimi mtani wake ambaye hatukuwahi kukaribiana wala kusogeleana katika itikadi lakini niliposikia kifo chako, moyo ulishtuka kwa mshangao mkubwa.
Poleni sana familia ya Komba. Nguvu yenu ya kustahimili msiba huu ipo mikononi mwa Bwana aliyetumba vyote maana ndiye ajuaye kila mmoja siku ya kuitwa kwake. Bwana alitoa na Bwana alitwaa, jina lake lihimidiwe.