Mnamo mwezi Aprili 2026 Umoja wa Pamoja wa Vyama Vikuu vya Korosho nchini (KCJE) na Bodi ya Korosho Tanzani walieleza kuwa wanatarajia kusambaza zaidi ya tani elfu 50 za Viuatilifu vya unga (Sulphur) msimu wa kilimo 2026/2027 kwa wakulima wa korosho nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa tarehe 26 Aprili 2026 Mkoani Mtwara, ilizinukuu KCJE na CBT zikieleza kuwa tayari kulikuwa na viuatili ambavyo vipo nchini huku vingine vikiwa vinatarajiwa kuendelea kuingia, ikiwa ni pamoja na tani elfu 30 za Salfa ya Unga.
Hata hivyo, taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali wakiwepo wakulima wa Korosho zinaeleza kuwa mpaka sasa kiasi cha viuatilifu viliyofika hasa Salfa ya unga ni vichache ilikinganishwa na maelezo yaliyokuwa yametolewa awali.
Maswali ya kujiuliza ni je, ni kweli kulikuwa Salfa ya unga iliyokuwa imebaki? Ilikuwa kiasi gani? Ilisambazwa wapi? Kuna kiasi gani ambacho kimeingizwa nchini mpaka sasa? Kiasi ambacho hakijaagizwa fedha zake ziko wapi?
MADAI YA KUFUNGWA KWA KIZUIZI CHA MKURANGA ILI KUPITISHA KOROSHO KIHOLELA
Kuna taarifa zinaeleza kuwa mwanzoni mwa mwaka 2026, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania akishirikiana na Mkurugenzi Mkuu walitumia nafasi zao kuagiza kufungwa kwa Kizuizi cha Mkuranga Mkoani Pwani, ambacho kilikuwa kimewekwa na Bodi ya Korosho Tanzania kwa lengo la kudhibiti usafirishaji wa korosho zilizobanguliwa bila vibali na bila kulipiwa tozo zinazozotambulika kisheria.
Inadaiwa kuwa Mwenyekiti alimwelekeza Mkurugenzi Mkuu kufunga kizuizi hicho kwa madai kwamba maafisa waliokuwa wanasimamia walikuwa wakila rushwa kupitisha mizigo ya wafanyabiashara jambo ambalo lilihitaji kufanyiwa uchunguzi.
Katika misimu ya Korosho 2024/2025 na 2025/2026, inadaiwa kuwa Mwenyekiti alikuwa akitumia baadhi ya vijana kununua na kusafirisha korosho zilizobanguliwa bila kuwa na vibali vinavyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania ambayo anaisimamia yeye.
Inadaiwa kuwa kupitia watu hao, mizigo ya korosho yenye uzito kati ya kilo 500 hadi kilo 800, na wakati mwingine kufikia takribani tani 1.5, kila siku ilikuwa ikisafirishwa bila kufuata taratibu zinazohitajika.
Zipo taratibu zinazotakiwa kutumika katika usafirishaji wa korosho zilizobanguliwa, ambapo msafirishaji anapaswa kulipa tozo zinazohusika, ikiwemo tozo ya Halmashauri inayokadiriwa kuwa shilingi 300 kwa kila kilo, na kuwasilisha risiti husika kama sehemu ya nyaraka za kuombea kibali kutoka Bodi ya Korosho Tanzania.
Hata hivyo, inasemekana kuwa utaratibu huo haukuzingatiwa katika mizigo iliyosafirishwa kutoka Mtwara Kwenda Dar Es Salaam, hali ambayo inawezekana kuwa imesababisha upotevu wa mapato ya Serikali za Mitaa na Serikali kwa ujumla, pamoja na kuathiri usawa wa ushindani miongoni mwa wafanyabiashara wanaofuata taratibu zilizowekwa.
Kuhusu kizuizi cha Mkuranga ni kwamba, kabla ya kufungwa kulikuwa na maafisa wa Bodi ya Korosho Tanzania waliokuwa wakifanya kazi katika eneo hilo kwa kushirikiana na maafisa wa Polisi wa Wilaya ya Mkuranga katika ukaguzi wa mizigo inayopita katika eneo hilo.
Inadaiwa kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, maafisa hao walikuwa wakikamata mizigo ya korosho iliyokutwa haina vibali vinavyohitajika na kuchukua hatua stahiki, ikiwemo kutoza faini kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za Bodi ya Korosho Tanzania.
Hata hivyo baadhi ya mizigo iliyokamatwa ilikuwa ikihusishwa na watu waliokuwa wakifanya kazi kwa niaba ya Mwenyekiti, na baada ya taarifa za kukamatwa kwa mizigo hiyo kuwafikia wahusika, inadaiwa kuwa Mwenyekiti alichukua hatua za kuagiza kufungwa kwa kizuizi hicho, jambo ambalo liliondoa utaratibu wa udhibiti uliokuwa umewekwa ili kuzuia usafirishaji wa korosho bila vibali.
Kwa kuzingatia uzito wa madai hayo, yafuatayo yanahitaji kufanyiwa uchunguzi na mamlaka husika:
Uthibitisho wa umiliki wa mizigo ya korosho iliyokamatwa katika Kizuizi cha Mkuranga na maeneo mengine.
Rekodi za vibali vya usafirishaji vilivyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania katika misimu ya 2024/2025 na 2025/2026.
Rekodi za malipo ya tozo za Halmashauri na Serikali zinazohusiana na mizigo hiyo.
Rekodi za mizigo iliyokamatwa na kutozwa faini katika Kizuizi cha Mkuranga.
Taarifa za maafisa wa Bodi na Polisi waliokuwa wakifanya kazi katika kizuizi hicho.
Maelekezo au mawasiliano yaliyotolewa kuhusu kufungwa kwa Kizuizi cha Mkuranga, ikiwemo sababu rasmi za uamuzi huo.
Uhusiano kati ya Mwenyekiti na watu waliodaiwa kununua au kusafirisha korosho kwa niaba yake.
Kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini kama kulikuwa na mgongano wa maslahi, matumizi mabaya ya madaraka au ukiukwaji wa taratibu za biashara ya korosho.
Hata hivyo kwa kuwa madai yaliyotajwa hapo juu ni mazito na yanahusu uadilifu wa uongozi, usimamizi wa Sekta ya Korosho na ulinzi wa mapato ya Serikali,yanapaswa kuchunguzwa na kuthibitishwa kwa ushahidi wa nyaraka, kumbukumbu za biashara, taarifa za maafisa waliohusika na uchunguzi huru wa mamlaka husika kabla ya kufikia hitimisho kuhusu uwajibikaji wa mtu yeyote.
Kwa hiyo, ni jukumu la mamlaka yenye dhamana ifanye uchunguzi wa kina na wa haki kuhusu madai haya, hususan kuhusu umiliki wa mizigo, vibali, malipo ya tozo, mizigo iliyokamatwa na mazingira ya kufungwa kwa Kizuizi cha Mkuranga, ili kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu.