Mafisadi wabanwa kuwania ubunge
Martha Mtangoo, Dodoma
Daily News; Sunday,March 08, 2009 @19:17
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuanzia sasa kuwa wagombea wa ubunge, Baraza la Wawakilishi na madiwani, watakuwa wakipigiwa kura za maoni na kila mwanachama badala ya utaratibu wa zamani uliokuwa ukiruhusu wajumbe wachache kupitia mikutano mikuu ya majimbo.
Uamuzi huo umepitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, kwenye kikao chake kilichofanyika juzi mjini hapa. Utaratibu huo unafuta uliokuwepo ambao kura za maoni zilikuwa zikipigwa na wajumbe wachache kupitia mikutano mikuu ya majimbo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati alisema kuwa utaratibu huo utaondoa tabia mbaya iliyojitokeza katika siku zilizopita kwa baadhi ya wagombea kutoa rushwa kwa wapiga kura ili kujipatia ushindi kwa kuwa chini ya utaratibu mpya, haitakuwa rahisi kuwahonga wanachama katika matawi yote jimboni bila ya kubainika.
Chiligati alisema leo kwamba uamuzi huo ni azma ya kupanua demokrasia ndani ya chama, na kuwashirikisha wanachama katika kupiga kura za maoni. Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Chiligati alisema utaratibu huo utaanza kutumika katika uchaguzi mkuu ujao.
Chini ya utaratibu huo mpya, kabla ya kura za maoni, wagombea watapata fursa ya kutembelea matawi yote na kukutana na wanachama wa CCM kwa lengo la kujitambulisha na kuomba kura. Alisema ziara hizo zitaandaliwa na CCM ngazi ya Wilaya na wagombea watasafiri kwa pamoja kwa usafiri ulioandaliwa na kugharimiwa na chama, hatua ambayo ina lengo la kutoa haki sawa kwa kila mgombea kutembelea matawi yote na kujitambulisha.
Aidha, Chiligati alisema baada ya ziara ya kujitambulisha kukamilika, itapangwa siku moja ambayo wanachama wote watapiga kura kwenye matawi yao. Upigaji kura utaanza saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana na kamati ya siasa ya tawi itaweka utaratibu wa kuhakiki kazi hiyo.
Alisema kura zitahesabiwa katika kituo husika na matokeo kutangazwa siku hiyohiyo na nakala ya matokeo hayo itabandikwa hadharani nje ya ofisi ya tawi au mahali ambapo kura zitapigiwa ili yawe wazi. Alisema kila mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kusimamia upigaji kura na kazi ya kuhesabu huku wilaya ikiweka wasimamizi wa uchaguzi katika kila tawi.
Katibu huyo wa itikadi na uenezi, alieleza kuwa katika utaratibu huo baada ya kura kuhesabiwa katika kituo na matokeo kutangazwa, msimamizi wa kituo atatakiwa kupeleka matokeo hayo haraka kwa Katibu wa Chama wa Wilaya. Alisema baada ya matokeo kutoka katika matawi yote na kufika wilayani, Katibu wa chama atajumuisha kura za kila mgombea na kwamba kila mgombea atakuwa na haki ya kuwepo mwenyewe au mwakilishi wake.
Kwa mujibu wa Chiligati, baada ya kazi hiyo kukamilika, vikao vya ngazi ya wilaya, mkoa na taifa vitakaa kuchambua kwa undani zaidi juu ya sifa za wagombea na kuzingatia kura za maoni walizopata na hatimaye yatawasilishwa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na ratiba ya tume ya uchaguzi.
Alisema kuwa NEC inaamini kuwa utaratibu huo utatoa nafasi kwa kila mwanachama kushirikishwa katika mchakato wa kuwapata wagombea na pia watashiriki kuwaunga mkono wagombea wa CCM kupata ushindi katika uchaguzi mkuu. Aidha alisema halmashauri kuu imeagiza kamati za usalama na maadili katika ngazi zote kuwa macho wakati wa kura za maoni ili kubaini vitendo vya rushwa.
Alisema atakayebainika kukiuka kanuni za uchaguzi ataenguliwa katika kugombea na iwapo atajihusisha na rushwa atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Wakati huo huo, Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zimeelekezwa kubadili katiba na sheria ya uchaguzi ili kuweka ukomo wa idadi ya wabunge na wawakilishi kufikia idadi inayohitajika.
Chiligati alisema NEC imeelekeza ukomo wa idadi ya wabunge katika Bunge la Muungano kuwa 360 na idadi ya Wawakilishi kuwa 86. Serikali hizo zimetakiwa pia kuhalalisha kisheria utaratibu mpya wa kuwapata wabunge wanawake kupitia viti maalumu.
Imeshauriwa Katiba ya SMZ ifanyiwe marekebisho ili kumwezesha Rais kuteua wanawake wasiopungua watano katika nafasi 10 alizonazo kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar. Alisema utaratibu wowote wa kuongeza idadi ya wabunge wanawake lazima izingatie ukomo huo na kuongeza kuwa utaratibu uliopo wa kuwapata wabunge na wawakilishi wanawake wa viti maalumu, utaendelea isipokuwa idadi yao katika kila chombo itapatikana kutokana na asilimia 50 ya wabunge wote wa majimbo 232.
Iwapo Bunge litakuwa na ukomo wa viti 360 wakati idadi ya majimbo yaliyopo sasa ni 232, wabunge wanawake watakaopatikana watakuwa 116 ambayo ni sawa na asilimia 50 ya wabunge wote wa majimbo. Hata hivyo, katibu huyo alifafanua kuwa kuna wabunge wanawake saba ambao watapatikana kwa mujibu wa katiba ambapo kwa utaratibu huo, wanawake 109 ndio watakaopatikana kupitia viti maalumu.
Chiligati alisema kuwa katika kuandaa orodha ya wagombea wanawake kwa nafasi 109 za Bunge na nafasi 20 za uwakilishi zitakazogombewa, NEC imependekeza wapigiwe kura na vikao vya Umoja wa Wanawake (UWT). Alisema kupitia utaratibu huo, wagombea ubunge na uwakilishi watapigiwa kura na mkutano mkuu wa UWT mkoa huku kwa upande wa wagombea udiwani viti maalumu, wanawake watapigiwa kura na mkutano mkuu wa wilaya.