DuaZaMama
JF-Expert Member
- Jun 2, 2025
- 1,882
- 4,153
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU UDANGANYIFU KWA KUTUMIA JINA LA BALOZI DKT. EMMANUEL JOHN NCHIMBI
Hivi karibuni kumekuwepo ongezeko la matukio ya udanganyifu yanayofanywa na watu wasiojulikana wanaotumia jina la Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kuwatapeli wananchi kupitia barua pepe, ujumbe mfupi wa simu, na mitandao ya kijamii.
Moja ya mifano ya udanganyifu huo ni barua pepe inayoadaiwa kutumwa na “EMMANUEL NCHIMBI” kupitia anwani ya barua pepe [email protected] ikidai kuwa kuna taarifa muhimu zinazohitajika kutoka kwa mpokeaji.
Umma wa Watanzania wote unataarifiwa kuwa, ujumbe huo si halali na hauhusiani kwa namna yoyote ile na Katibu Mkuu wa CCM wala taasisi yoyote rasmi ya Chama na Serikali.
Inasisitizwa kwamba:
- Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi hatumii barua pepe binafsi kwa masuala ya kitaasisi au ya chama.
- Viongozi wa Chama au Serikali hawatumi ujumbe wa siri kwa masuala ya kikazi kupitia barua pepe binafsi au njia zisizo rasmi kama hizo.
- Ni muhimu kuwa makini, kutilia shaka, kupuuza au kutoa taarifa kwa mamlaka pale unapopokea ujumbe unaokitaka utoe taarifa binafsi kwa haraka au kuchukua hatua bila uthibitisho rasmi.
Wito unatolewa kwa Watanzania na wananchi wote kwa ujumla kuwa waangalifu na kujiepusha na mawasiliano ya aina hiyo. Endapo utapokea ujumbe wa kutilia shaka, tafadhali ripoti kwa vyombo vya usalama au kwa uongozi wa CCM katika ngazi husika.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Aboubakary Liongo
Kaimu Katibu wa Habari wa Katibu Mkuu wa CCM
21/07/2025