Dingswayo
JF-Expert Member
- May 26, 2009
- 4,019
- 2,925
NAJUA ni maeno ya kuudhi, lakini sina budi kuyasema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina dhamira ya dhati kuwapatia Watanzania katiba mpya waitakayo.
Kinachofanyika sasa ni kutafuta sifa ya kuingizwa kwenye rekodi kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ndiyo iliandika katiba mpya, lakini ukweli ni kwamba tunaandaa katiba mbaya zaidi ya hii iliyopo.
CCM haiwezi kusimamia na ikaandika katiba mpya wakati mawazo hayo haikuwa nayo kwenye ilani yake ya uchaguzi, badala yake kutokana na shinikizo la wapinzani walikurupuka bila kujiandaa kifikra na kisaikolojia.
Kwa viongozi wengi wa serikali na CCM, ukizungumza katiba mpya kila mmoja anapata hofu kuwa cheo chake kinaondoka. Bila shaka tuliwaona Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema na Celina Kombani wakati huo akiwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Hawa walitamka wazi kuwa katiba iliyopo inakidhi na wala Watanzania hawahitaji mpya. Na huo ndiyo ulikuwa msimamo wa CCM.
Katika maajabu hayo hayo rais akakubali kubeba ilani ya wapinzani kuandika katiba mpya halafu mchakato ukaanza kwa kutayarisha muswada wa sheria ambao ulisimamiwa na viongozi wale wale; Jaji Werema na Kombani ambao walishautangazia umma kuwa katiba ya sasa inatosha.
Serikali ya CCM mbali na kubeba ilani ya upinzani pengine hata kwa nia njema, lakini walitakiwa kwanza kujipa muda wa kujiandaa kisaikolojia na kifikra kukubali kwa dhati mabadiliko ya katiba.
Badala yake Serikali ya CCM iliichukua ajenda ya katiba mpya kama sehemu ya kujitafutia umaarufu, lakini kama ilivyotarajiwa tangu mwanzo, wameshindwa kusimamia mchakato huo na kuufanya uendeshwe kisiasa.
Nilimsikiliza vizuri Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, wakati akizungumzia mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba.
Kama wadau mbalimbali walivyoulalamikia uchaguzi huo kuwa uliendeshwa kisiasa na kutawaliwa na vitendo vya rushwa, Jaji Wariba na tume yake naye alikiri hilo lakini hataki kabisa uchaguzi huo urudiwe.
Hii ndiyo taswira niliyoiona tena bungeni kwa wabunge wa CCM na mawaziri wakijaribu kuwazima wapinzani katika hoja ya uchaguzi huo wa mabaraza.
Hawa wanasifu mchakato mbovu na kutamba kuwa CCM ilipaswa kuchukua wajumbe wengi kwa kuwa ina wafuasi wengi katika ngazi hizo. Hoja ikaja kumbe nao wanakiri kuwa kilichofanyika ni ushabiki wa kisiasa wala si uchaguzi.
Niliwatazama mawaziri, nikawatazama wabunge wa CCM kisha nikamtazama Mwanasheria Mkuu wa Serikali nilijifunza kitu kimoja kuwa kutawala ni upofu. Hata vile ambavyo wengine wanaviona, watawala wao wanajipofusha.
Tatizo linaanzia hapa, na kwa kweli hadi kesho namlaani aliyeondoa Ahadi 10 za TANU kuacha kufundishwa shuleni sambamba na wale waliolizika Azimio la Arusha.
Ahadi hizi 10 za TANU ukizisoma vizuri, kama wewe ni kiongozi usiye na uzalendo kwa taifa lako, lazima utajionea aibu mwenyewe. Yafaa tukaziweka kwenye katiba mpya.
Ahadi hizo ni:
- Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
- Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote
- Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.
- Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa.
- Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.
- Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.
- Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu.
- Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.
- Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika.
- Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.
Wabunge wa CCM na mawaziri wao wamekataa kukubali hoja ya uchaguzi wa mabaraza ya katiba urudiwe. Furaha yao ni kuona chama kimevuna wajumbe wengi wa kukiwakilisha kwenye mabaraza hayo.
Endapo sasa wananchi watakataa kushiriki kujadili rasimu ya katiba kwa kuwa mabaraza hayo hawakuyachagua wao, CCM itatengeneza katiba ipi ambayo wanakimbia mbio iwe imekamilika Aprili 26, 2014?
Hawa viongozi wa serikali na CCM waliisoma vizuri ahadi ya saba ya TANU? Kama kweli wameisoma na wanaizingatia ni kwanini huwa hawataki kujishusha kidogo kupokea maoni kutoka upande mwingine?
Ni kwa ubabe kama huo, wabunge hao hao walipitisha muswada mbovu wa kutungwa kwa sheria ya kuanzisha mchakato wa katiba mpya, hatua iliyowasukuma wabunge wa CHADEMA kususia Bunge na baadaye kwenda kukutana na rais.
Baada ya rais kupokea maoni ya CHADEMA, pia alikutana na vyama vingine vyenye wabunge na wadau kisha ukapelekwa muswada wa marekebisho ya sheria hiyo bungeni.
Hili pia ndilo ninaloliona kwenye hatua hii ya uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza. Kama Tume itaendelea kuabudu mawazo ya CCM na kuwapuuza Watanzania, hakika mchakato huu hautafika mbali. Tafakari!