Rais Kikwete awakuna
wapambanaji wa ufisadi
*Kilango:Ametupa faraja kupambana zaidi
*Shellukindo:Ameweka sawa ya Richmond
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuhutubia Taifa na kufafanua juu ya masuala mbalimbali mazito ya kisiasa na kitaifa hususan vita vya ufisadi nchini, wabunge mbalimbali wa CCM hasa walio mstari wa mbele kupambana na ufisadi, wameipokea hotuba hiyo kuwa ni dira mpya.
Mbunge wa Same Mashariki-CCM, Anne Kilango Malecela, amelazimika kuzungumza akiwa ughaibuni kusisitiza kuwa msimamo wa Rais Jakaya Kikwete, kuhusiana na mapambano dhidi ya ufisadi hasa ahadi yake ya kuruhusu Serikali kukosolewa kwa nia ya kusahihisha makosa, umewapa faraja wabunge wanaopambana katika vita hivyo.
Akizungumza kwa simu kutoka Iowa, Marekani aliko kikazi, Kilango ambaye ni mmoja wa wabunge wachache ndani ya CCM wenye msimamo usioyumba, alisema Rais Kikwete ameonyesha ujasiri na kwamba wabunge makini wako nyuma yake.
Kwa kweli tunampongeza sana Rais Kikwete kwa msimamo wake kuhusiana na ufisadi. Nimepata taarifa kupitia kwenye mtandao na kuwasiliana na wenzangu Tanzania, kwa kweli tumefarijika sana na msimamo wake ambao tunaufahamu siku zote, alisema. Kilango alisema vita dhidi ya ufisadi ni vita vyenye changamoto nyingi ambazo wamekuwa wakipambana nazo na kwamba hata Rais Kikwete naye amekuwa akikumbana na changamoto nyingi, lakini ameonyesha ujasiri wa hali ya juu kubaki na msimamo wa kutounga mkono uhujumu wa fedha za wananchi.
Tuko nyuma yake kwa moyo mmoja. Hatutapunguza kasi katika kutafuta mabadiliko ya dhati na yenye nia ya kukiimarisha chama chetu cha CCM (Chama Cha Mapinduzi) na Rais wetu asikate tamaa, tuko pamoja naye, alisema. Alisema kutokana na furaha aliyoipata kutokana na kauli ya Rais Kikwete, Kilango anasema kwamba kwa sasa bado yuko katika maombolezo ya msiba wa ndugu yake lakini amelazimika kuzungumza hadharani kuonyesha furaha aliyoipata kutokana na msimamo wa Rais.
Alisema amekuwa kimya kwa muda mrefu, lakini Watanzania watarajie kishindo kikubwa mara atapoamua kuzungumza tena hadharani kutokana na kujiandaa kikamilifu kuitetea nchi yake. Wasione nimekaa kimya, mimi nitajitokeza na kuibua mambo mazito kama Tsunami na watu najua mtatikisika na waandishi mtapata mambo ya kuzungumza, aliahidi.
Kilango ambaye alitunukiwa tuzo ya mwanamke jasiri kutokana na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa, alisema Rais Kikwete amekipa uhai mpya Chama Cha Mapinduzi na kwamba sasa chama kinazidi kuwa na nguvu kubwa. Kwa kuimarisha chama, tunamhakikishia Rais Kikwete kwamba tutamsaidia kwa nguvu zetu zote bila kuchoka wala kuogopa misukosuko. Amegusa nyoyo zetu, alisema.
Katika mazungumzo yake ya juzi usiku, Rais Kikwete alibainisha wazi kwamba katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na aina zote za uhalifu hana mchezo. Hata alipoulizwa swali kwamba kuna watu wanalindwa kwa kuwa amekuwa na mahusiano nao, Rais alionekana kuwa jasiri kwa kusema wazi kwamba katika ufisadi hana rafiki wala ndugu na kwamba wahusika wanalifahamu hilo.
Mbunge wa Bumbuli-CCM, William Shellukindo yeye aliguswa na ahadi ya Kikwete kulimaliza suala la Richmond.
Nampongeza sana Rais kwanza ametuthibitishia kwamba anafahamu kuwa Serikali inalazimika kuleta majibu kuhusu maazimio ya Bunge mwezi Novemba. Na serikali ikituletea majibu ya kuridhisha sisi tutafurahi sana maana suala hilo litakuwa limefikia mwisho ili tuweze kuendelea na mambo mengine....Sisi katika kamati yetu (Nishati na Madini) tuliazimia na tumesema tutaendelea kusimamia haki hadi mwisho.
Akizungumzia suala la wabunge wa CCM kutoelewana, Shellukindo alisema hilo ni suala la afya kwa chama tofauti na watu wanavyoona ni tatizo.
Hiyo ni afya ya kisiasa maana katika wabunge zaidi ya 200 wa CCM huwezi kuwa na wabunge wote wenye mawazo yanayofanana. Sasa hili la kuwepo kwa msigano ni tatizo la baadhi ya wabunge wasiofahamu kutofautisha hoja na mahusiano. Mbunge anaweza kuwa na hoja na sisi mara zote hatuzungumzii mtu binafsi tunazungumzia hoja.
Kwa mfano kama suala la Richmond lilikuwa ni azimio la bunge na wote wa CCM na wapinzani tulikubaliana katika hilo. Sasa lazima tujue kwamba wale waliochukuliwa hatua wana wabunge marafiki zao na wao wanaweza kuwa na hoja tofauti na mtazamo tofauti. Hili ni suala la kawaida na siyo tatizo wala mgawanyiko hasa kwa wale tunaoelewa.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, CCM, Godfrey Zambi, mmoja wa walioshikia bango sakata la Ticts, alisema hotuba ya Kikwete imewaweka sawa:
Labda niseme kwamba siku zote sisi wabunge tumechaguliwa ili kutetea maslahi ya umma. Kazi hii haiwezi kuwa ya wapinzani peke yao ni kazi ya wabunge wote. Kama mimi ningekuwa mroho wa madaraka ningekwenda upinzani tangu mwaka 2000, lakini niliamini kwamba ni vyema kuikosoa serikali nikiwa ndani ya chama changu CCM. Lazima katika hili tuelewane na ninashukuru kwamba Rais ameliweka vizuri.
Mmoja wa wabunge vinara wa sakata la Richmond, Lucas Selelii-CCM Nzega, alimsifu Kikwete kwa kutangaza msimamo wa kutowaonea haya mafisadi. Tunamshukuru sana Rais ameutangazia umma wa Watanzania msimamo wake na wa serikali yake. Lazima kama viongozi wa CCM na viongozi wa wananchi tujifunze kusoma ishara za nyakati. Naamini Rais hilo analijua na ndiyo maana kauli yake mmeisikia naamini ametuwekea njia na mwelekeo wa tunakokwenda, alisema.
Source: Kulikoni 12/9/2009.