•Wabunge CCM: Tutakufa na mtu
Waitahadharisha Serikali kuhusu Richmond
Na John Daniel, Dodoma
WABUNGE wa CCM wamezidi kukasirishwa na vitendo vya kifisadi na kuitumia Serikali salamu za tahadhari, kwamba watakufa na mtu iwapo hawatapata taarifa ya kina kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu hatua kali dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa Richmond.
Katika hali isiyotarajiwa, wabunge hao wameonya kwamba hawatakuwa na huruma wala kulindana kichama, juu ya suala hilo zito kwa maelezo, kwamba hivi Sasa Watanzania wasio na hatia wanaumia kwa kukabiliwa na ugumu wa maisha, kutokana na mabilioni ya fedha kutumika kulipa kampuni hewa bila kuzalisha umeme kama ilivyotarajiwa.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Bunge jana, wabunge hao walisema ili kuepuka lawama na kuhakikisha kwamba wanatekeleza azma yao ya kusafisha Serikali ya CCM dhidi ya ufisadi, walipanga kuwasilisha mapendezo yao katika kikao cha wabunge wa CCM kilichopangwa kufanyika jana jioni.
"Tunatarajia taarifa iliyokamilika na ya kina kuhusu hatua kali zilizochukuliwa dhidi ya mafisadi wote, wengine walishaachia ngazi, lakini wengine bado wapo wanaendelea na kazi zao serikalini.
"Tunataka kujua wamechukuliwa hatua gani na kwa nini wao hawajakaa pembeni, hapa hakuna kulindana wala kufichana ukweli, lazima haki itendeke," alisema Mbunge machachari wa CCM kutoka Kaskazini.
Alipoulizwa iwapo taarifa hiyo haitawagusa wanaoendelea na kazi zao serikalini na kusomwa jumla jumla kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa, Mbunge huyo alisema:
"Unajua, katika hili hakuna mchezo, kuna kitu ambacho nikisema sasa hivi wanaweza kutafuta njia ya kukwepa au ... tutakufa na mtu yeyote anayeleta mchezo, ili Serikali ijue kwamba tumeamua, mimi mwenyewe nitawasilisha mapendekezo yangu katika kikao cha wabunge wa Chama leo (jana) jioni." alisisitiza.
Naye Mbunge mwingine kutoka Tanga, alisema yeye na wabunge wengine wanatarajia kwamba Serikali itatoa majibu yanayojitosheleza na yenye kujibu maswali magumu ya Watanzania wote bila kuogopa mtu, wala kuoneana haya.
"Bunge lilifanya kazi yake, sasa tunasubiri Serikali ijibu na tunaamini majibu yatakuwa mazuri tu, hata wale ambao hakuwajibika kuacha kazi zao, lazima hatma yao itakuwa katika majibu ya Serikali katika Bunge hili, kama Serikali haitafanya hivyo, basi tutaanzia hapo, subiri tu, utaona muda ukifika, japo hatujui ni lini taarifa hiyo itawasilishwa," alisema Mbunge huyo.
Wabunge wengine waliozungumza na Majira walionesha nia ya dhati ya kutaka mabadiliko, huku wengi wao wakitaka viongozi wa Serikali waliokabidhiwa madaraka ya umma kubadilika na kutambua kwamba makosa yao madogo ni mateso kwa Watanzania zaidi ya milioni 30.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu jana asubuhi, Spika Bw. Samwel Sitta, alitangaza kwamba wabunge wote wa CCM wangekutana katika kikao cha chama hicho jioni katika ukumbi wa Pius Msekwa.
Kikao hicho kilitarajiwa hata hivyo kutanguliwa na kile cha uongozi wa chama hicho ambacho jana saa 5 asubuhi.
Kwa upande wao wananchi waliozungumza na Majira walidai kwamba majibu ya hatua dhidi ya watuhumiwa wa Richmond ni mtihani wa pili kwa Rais Jakaya Kikwete na ni mtihani wa kwanza kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na kwamba iwapo watashindwa kusema ukweli, itakuwa ni dosari kwao.
Katika Kikao cha 11 cha Bunge Aprili mwaka huu, Bw. Pinda, aliahidi Serikali kutoa majibu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa Richmond, huku akisisitiza kwamba suala hilo linahitaji umakini wa hali ya juu kwa kuwa linagusa maisha na maslahi ya watu moja kwa moja.
Katika mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge yaliyowasilishwa bungeni mwaka huu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Kamati hiyo ilitoa jumla ya mapendekezo 23 ikiitaka Serikali kuyatekeleza na kutoa jibu ndani ya Bunge.
Moja ya mapendekezo hayo ni kuwachukulia hatua kali wote waliohusika, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani, kuwafukuza kazi watumishi wa Serikali akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Johnson Mwanyika na wote waliohusika kwa njia moja au nyingine na kashfa hiyo.