Mwaka 1962, Mwalimu Nyerere aliandika kitabu kidogo cha kurasa 20 kinaitwa TUJISAHIHISHE. Kwa maoni yangu wana CCM ni vema tukajikumbusha maudhui yake ili tulisaidie taifa.
Katika kitabu hiki Mwalimu Nyerere anasema "Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, n.k., matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi." Ni jambo lililo wazi kuwa ubinafsi wetu katika michakato ya uchaguzi ndio umetufikisha hapa. Picha tuliyoijenga ni kuwa nafasi zote tunataka ziwe zetu CCM, iwe tumechaguliwa au hatukuchaguliwa? Hata chache wanazopata wapinzani kwa haki, tunawapora.
Tutafakari ikiwa wagombea wa CCM wakikatwa nchi nzima, tukaambiwa hawajui kusoma na kuandika, sisi kama wana CCM tutajisikiaje? Au wagombea wetu wanapoenda kurudisha fomu wawe wanapigwa chenga na wakurugenzi mpaka muda wa kurudisha fomu unaisha halafu waambiwe wameshachelewa hivyo fomu zao hazitapokelewa? Au mawakala wa wagombea wetu wafanyiwe mizengwe kuingia kwenye vituo vya kupigua kura? Sisi wana CCM, tukitendewa mambo kama hayo tutakubaliana nayo?
Katika kitabu chake Mwalimu anasisitiza kuwa: “Makosa ni makosa bila kujali ni nani ameyafanya. Muhimu ni kuyajua makosa hayo na kujisahihisha.” Tujiulize, fomu za wagombea wa upinzani zingekuwa zinapokelewa bila mizengwe, wanateuliwa kugombea bila mizengwe, mawakala wao wanaruhusiwa kusimamia kura za wagombea wao bila mizengwe na pale wanaposhinda wanatangazwa bila mizengwe, Je, tungekuwa na No reform, No election?
Mwalimu alisema "hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujifanya hayapo" Yanayolalamikiwa na CHADEMA, yanaakisi kauli za Ndugu Nape za halali, nusu halali na halamu, pamoja na zile za DC Ng'umbi wa Longido kuhusu walichofanya 2020. Wenye wasiwasi na utendekaji wa haki kwenye chaguzi zetu sio CHADEMA tu, hata Prof. Assad CAG mstaafu naye anasema hata piga kura mpaka reform zifanyike. Madai ya reform sasa hivi yamekuwa ni ya watu wetu, na Mwalimu anatuasa "Chama cha siasa hakina budi kujishughulisha na shida za watu."
Mwalimu alitufundisha “Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi. Ukiniona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa!”
Tumeaswa na baba wa Taifa kuwa "Watu walio hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu." Hakutakuwa na ubawa kuyafanyia kazi maoni ya wazee wetu akina Butiku na Warioba. Haswa ukizingatia hata viongozi wa dini nao wameshauri mazungumzo yafanyike. Kasoro zinazowezekana kurekebishika zirekebishwe, twende kwenye uchaguzi October tukiwa wamoja kama Taifa.
“Tujisahihishe. Tujitazame. Tujikague. Tujione. Tujirekebishe.” Mwl Nyerere 1966.