WAKATI mbunge wa jimbo la Maswa, John Shibuda akisisitiza nia yake ya kugombea urais, CCM mkoani kwake Shinyanga imeamua kumpuuza na kumtangaza Jakaya Kikwete kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa tiketi ya chama hicho tawala.
CCM Shinyanga pia imesema haimtambui mgombea mwingine yeyote wa nafasi hiyo kwa tiketi yake na hata kama atajitokeza haitamuunga mkono.
Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Mohamed Mbonde aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa chama hicho kuwa chama hakina ugomvi na mtu anayetaka kugombea nafasi ya urais bali azingatie taratibu za chama hicho.
"Sisi wana CCM tumejiwekea utaratibu kwamba kila rais atakayechukuwa madaraka kupitia chama hiki atakaa madarakani kwa muda wa miaka kumi na hata katiba ya chama chetu inasema hivyo na mwanachama kugombea lazima azingatie katiba inasemaje," alisema Mbonde.
Aliongeza kuwa chama hakijapokea taarifa rasmi za kuwepo mmoja wa wabunge anayetaka kugombea nafasi ya urais mbali ya kusikia kwenye vyombo vya habari tu na kusisitiza kuwa halmashauri kuu ya CCM mkoani inamuunga mkono mwenyekiti wa taifa, Kikwete kuwa ni mgombea pekee wa nafasi hiyo.
Alisema mmoja wa wabunge hao anayedaiwa kutaka kugombea urais ni mjumbe wa halmashauri ya CCM ya mkoa ambayo imetoa tamko la kumuunga mkono Kikwete kugombea urais peke yake kupitia chama hicho.
Pia halmashauri hiyo imewataka wanachama wa CCM wote kutomdhihaki Kikwete kwa kuwa ndiye anayesimamia ilani waliyoiweka wenyewe na kwamba kama wanayo maoni ama matatizo watumie vikao vya chama hicho.
Lakini Shibuda alisema hapingi vikundi vya watu kutamka hadharani kuwa vinamuunga mkono Rais Kikwete.
"Kwa mujibu wa taratibu za kidemokrasia, matamko ya namna hiyo ni ishara ya ukosefu wa elimu ya uraia kwa wanaoyatoa," alisema Shibuda, mmoja wa wabunge machachari ndani na nje ya Bunge.
Shibuda alisema kuwa hakuhudhuria kikao cha halmashauri kuu ya mkoa na wala hana taarifa za kufikiwa uamuzi wa kumtangaza Kikwete kuwa mgombea pekee wa urais.
CCM pia imeunga mkono hotuba ya rais ya kuuaga mwaka 2009 na kuukaribisha mwaka 2010 ambayo ilitahadharisha dhidi ya kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa na viongozi wa taasisi za kiraia, hasa za kidini, akisema kuwa zina mwelekeo wa kuligawa taifa.
Katibu huyo wa CCM mkoa alisema kauli za watu hao zinaonyesha kuwa ni vipofu wa macho na mioyo na kwamba kuna uwezekano mkubwa wakawa na chuki binafsi.
Katibu huyo alisema wanaccm wana amini kuwa kukosoa na kukosolewa kwa kufuata taratibu ni msingi wa kuimarishana lakini kudhalilishana na kubezana ni msingi wa kuvunjana moyo na kwamba vitendo hivyo vinaweza kusababisha viongozi wa awamu zote za serikali zikapimwa kwa kuangaliwa mtu na hivyo nchi kupoteza mwelekeo.