Waziri wa zamani kwenye Wizara mbalimbali Geoffrey Idelphonce Mwambe amefungua kesi kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam dhidi ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kesi ambayo inasikilizwa leo, Jumanne Januari 20.2026
Kesi hiyo namba 488 ya mwaka 2026 inayotarajiwa kusikilizwa majira ya saa 03:00 asubuhi, imefunguliwa kwa hati ya dharura, na imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji David Ngunyale,
Inaelezwa kuwa, msingi wa kufunguliwa kwa kesi hiyo ni kwamba Geoffrey Mwambe ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kilichokuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na pia Mbunge wa zamani wa Jimbo la Masasi, mkoani Mtwara (CCM) anapinga kitendo cha Idara ya Uhamiaji kumnyang'anya 'passport' yake ya kusafiria kinyume na taratibu
"Mwambe ni mgonjwa, mgonjwa kabisa serious, sasa hivi karibuni alipanga kusafiri nje ya nchi kwaajili ya matibabu, sasa jambo la kushangaza ni kwamba alipofika kwenye mpaka wa Namanga akiwa ameambatana na mke wake na watoto wake wote walinyang'anywa 'passport' zao na kuzuiliwa kutoka nje ya nchi bila kupewa maelezo ya zuio lao limetokana na nini", kilieleza chanzo cha kuaminika kilichopo karibu na familia hiyo
Licha ya kwamba haijafahamika mara moja sababu za kushikiliwa kwa 'passport' hizo, lakini itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwaka uliopita (Desemba 2025) Mwambe alishikiliwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kwa makosa ya jinai lakini baadae aliachiwa kwa dhamana
Taarifa iliyokuwa imetolewa na Wakili wa Mwambe, Hekima Mwasipu kwa Waandishi wa Habari wakati huo haikueleza kama mteja wake amepatiwa masharti ya dhamana yanayomzuia kusafiri nje ya nchi au la.