Mali bila daftari na vitabu vya fedha za umma vinavyoota miguu!
M. M. Mwanakijiji
Kuna msemo wa zamani unaosema kuwa ‘Mali bila daftari hupotea bila habari'.
Msemo huu ni miongoni mwa kanuni za mwanzo kabisa, mfanyabiashara na mtu yeyote mwenye kutumia fedha zake anatakiwa kujifunza.
Msemo huu ni somo kubwa la kusimamia fedha kwamba ili ujue fedha zinavyoingia na kutoka ni vizuri uwe na mahali ambapo unarekodi mapato na matumizi yako. Kwa kufanya hivyo utaweza kujua ni wapi unapata faida na ni wapi unapata hasara lakini vile vile unaweza kujua unatumiaje fedha zako.
Kutokana na nadharia hiyo ya zamani sana jamii zote ambazo zimekuwa na matumizi ya fedha zilijifunza mapema sana jinsi ya kutunza kumbukumbu ya matumizi ya fedha.
Hii inasaidia mtu kujua amenunua nini, kwa kiasi gani, wapi, na pia inasaidia kujua ni kwa kiasi gani bei ya vitu imebadilika na kumsaidia kulinganisha.
Kumbe zipo faida nyingi sana ambazo siyo lengo la makala yangu leo zinazohusiana na utunzani mzuri wa kumbukumbu za fedha.
Mimi mwenyewe nimejifunza umuhimu huu wa kutunza kumbukumbu baada ya kujikuta nalipia kitu kimoja mara mbili na kujitia hasara isiyo ya lazima. Nilifanya malipo ya huduma ya intaneti huku nikiwa nimetumia mfumo wa kibenki kuweka tarehe ambapo kampuni ingechukua fedha moja kwa moja kutoka kwa akaunti yangu lakini siku ya kulipia nilikuwa nimeshasahau kuwa niliweka kiasi na tarehe tayari kwa benki kufanya hivyo.
Badala yake nikawapigia simu kampuni na kuwaambia wachukua kiasi kingine cha fedha ili wasije kunikatia huduma.
Baada ya taarifa ya benki ya mwezi kunijia nikajikuta ndani ya siku moja moja nimefanya malipo mawili makubwa na nilikumbuka lile tu nililolipia kwa kupiga simu.
Nilipoamua kupitia daftari langu la benki ndipo nikakuta kuwa nilikuwa tayari nilikuwa nimewaagiza kampuni kuchukua fedha ya malipo. Bila daftari ningedhani kuna mtu kaniibia! True story.
Kanuni hii ya kutunza kumbukumbu haihusu taasisi binafsi tu bali pia serikali na taasisi zake vile vile.
Serikali inakusanya kodi kutoka kwa wananchi na kutoka kwenye huduma na bidhaa mbalimbali na vyanzo vingine vya ‘mapato'. Fedha hizi hutumiwa tena na serikali hiyo hiyo katika kulipa mishahara, kuleta huduma mbalimbali kwa wananchi n.k Hivyo, kanuni ya kutunza kumbukumbu inatakiwa kufuatwa vile vile.
Serikali haitakiwi hata kidogo kutumia fedha bila maelezo. Serikali ambayo inatumia fedha bila maelezo inawaibia wananchi!
Ni kutokana na hili basi serikali kama ya kwetu zina mtu anaitwa ‘Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu' ambaye amepewa jukumu la kuangalia ripoti mbalimbali za matumizi ya serikali na taasisi zake na kulinganisha taarifa hizo na vitu vilivyonunuliwa. Njia pekee Mkaguzi (CAG) anaweza kujua fedha zimeingia wapi, vipi na zimeenda wapi, vipi na kwa nini ni kwa kupitia vitabu au madaftari yenye kurekodi matumizi ya serikali.
Ni muhimu sana kwa vyombo vya umma na vyote vya serikali kuwa na utaratibu mzuri wa kutunza kumbukumbu. Bila ya kumbukumbu hatuwezi kujua jinsi gani fedha za umma zimepatikana na kutumika. Inapotokea taasisi au chombo cha umma kinashindwa kutoa taarifa za mapato na matumizi yake kwa kushindwa kuonesha vitabu vya risiti, au vitabu vya kihasibu kwa kisingizio chochote kila uwezekano ni kuwa kuna kitu kimejaribu kufishwa.
Baada ya kupitia ripoti ya CAG ya mwaka 2009/2010 na kulinganisha na ripoti nyingine za miaka iliyopita nimegundua kuwa kuna tabia ambayo imekubaliwa na inatarajiwa kuwa kwa namna fulani kuwa vitabu vya hesabu vinaweza kupotea kiana na watu bado wakaendelea kuwa katika kazi zao kama kawaida na kuendelea kupokea mishahara kana kwamba hilo si jambo kubwa.
Hebu tuangalie ripoti hizo na tuone jinsi gani Watanzania kama taifa wanachukuliwa kama mazoba ambao hawana uwezo wa kuhoji, kufikiri wala kudai watu wawajibishwe.
Tunapozungumzia ufisadi si lazima watu wawe kwenye Kamati Kuu ya CCM kujulikana kuwa ni mafisadi. Ufisadi mwingine ni huu wa kupoteza vitabu vya hesabu na kwa makusudi kuficha wakaguzi kinachoendelea.
Kwa sababu vitabu haviwezi kuota mbawa au miguu na kutoweka vyenyewe. Bado haijawahi kutokea kwamba kwenye ofisi fulani ati vitabu ‘havionekani' au vimeshindwa kupatikana.
Hivi vitabu vinavyoota miguu ni vya aina gani hivi? Vitabu ambavyo vinashindwa kupatikana ati kwa sababu ‘vimeshindwa kupelekwa' vimetengenezwa wapi? Inashangaza serikali ya CCM na viongozi wake wanaisoma ripoti hii na hawasikii hasira.
Na tatizo siyo tu kutopatikana vitabu wakati mwingine vitabu vinapatikana lakini taarifa za matumizi au mapato yake hazipo wakati watu wote serikalini wanajua kabisa huwezi kutumia mali za umma bila kuweka rekodi lakini viongozi hawa hawa tuliowarudisha madarakani wanavumilia mtindo wa taasisi na idara mbalimbali za serikali kusema kuwa wametumia fedha hivi au vile lakini bila kuonesha risiti au kurekodi mahali popote pale.
Tuangalie mifano michache ya vitabu vya serikali yetu vinavyoota mbawa na viongozi wake bado wakiwa madarakani wakilindwa na serikali ile ile.
Kwenye Serikali za Mitaa
Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 pamoja na mabadiliko yake Halmashauri zote nchini zinatakiwa kuwa na kutunza vitabu vya mahesabu.
Ripoti inatutaarifu kuwa: 948 vya kukusanyia mapato katika Halmashauri 48 havikuweza kutolewa kwa wakaguzi kwa ajili ya uhakiki, hivyo kupelekea wakaguzi kushindwa kuthibitisha kiasi cha mapato kilichokusanywa kupitia vitabu hivyo. Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro iliongoza kwa kuwa na vitabu 168 ambavyo havikuwasilishwa ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi yenye idadi ya vitabu 101.
Mtu mwenye akili timamu anatakiwa kujiuliza hivi, vitabu hivyo ‘havikuweza kutolewa kwa wakaguzi' kwa sababu gani? Havikuwepo, havikuweza kupatikana, vilihamishwa, vilifichwa, viliazimwa au viligeuka mvuke vilipoona wakaguzi wanafika basi vikatoweka hewani!?
Mniruhusu niangalie kwa undani kidogo sakata la vitabu vyenye mbawa kwenye Halmashauri zetu: Nanukuu moja kwa moja kutoka kwenye ripoti ya CAG.
Wilaya ya Mwanga
Vitabu 8 vya wazi vya kukusanyia mapato (HW5) na vitabu 28 vyenye thamani ya Sh 8,000,000 havikupatikana wakati wa ukaguzi.
Mapato yaliyokusanywa kwa kutumia vitabu hayakuweza kuthibitishwa ndani ya vitabu hivyo.
Wilaya ya Kilwa
Vitabu 101 vya kukusanyia mapato havikupatikana wakati wa ukaguzi, kwa hali hiyo mapato yaliyokusanywa kwa kutumia vitabu hivyo hayakuweza kuthibitishwa.
Hati za malipo zenye jumla ya sh 144,994,981 hazikupatikana wakati wa ukaguzi kwa hiyo uhalali wa malipo hayawezi kuthibitishwa.
Wilaya ya Kilosa
Vitabu vya kukusanyia mapato vipatavyo 394 havikuwasilishwa kwa wakaguzi vilipohitajika.
Mifano hiyo ni kidogo tu ya kile ambacho kinaonekana kuwemo kwenye zoezi hili la watendaji kuvipatia miguu vitabu vya mapato na matumizi. Mkaguzi Mkuu anasema hivi kama hitimisho lake kuhusu suala la vitabu kutoonekana:
"Kwa kuwa vitabu hivi vilikusudiwa kukusanya mapato ya halmashauri, sikuweza kujua mara moja ni kiasi gani kilikusanywa kwa kutumia vitabu hivyo" na anagongelea msumari kwa kututaarifu kuwa "kuna uwezekano mkubwa wa wizi wa mapato ya halmashauri na kupotosha makisio ya mapato ya halmashauri'.
Unaweza kufikiria tatizo hili la vitabu kuota mbawa ni la halmashauri peke yake.
Serikali Kuu
Ofisi ya Rais jumla ya sh 11,870,000 zililipwa kwa watu mbalimbali bila kuwa na nyaraka timilifu.
Wizara ya Fedha
Wizara ilihamisha kiasi ya sh 70,000,000,000 (bilioni 70) kwa kipindi kilichoishia Juni 30, 2010 kwenda TIB kwa ajili ya kubadilisha TIB kuwa taasisi ya Maendeleo ya Fedha na pia kufungua benki kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Kwenye hili Mkaguzi aliomba nyaraka zifuatazo na nyaraka hizo hakupewa. Nyaraka zingemsaidia kujua fedha bilioni 70 za Watanzania zimetumiwa vipi:
- Taarifa ya akaunti ya benki kwa kipindi kilichoishia Juni 2010.
- Dondoo za ripoti ya fedha kuonyesha mapokezi yote, malipo na urari wa mfuko huo.
- Hatua zilizochukuliwa ili kuzuia uwezekano wa mfuko huo kuanguka kutokana na ukweli kuwa mkataba hauwabani TIB kuwajibika waliochukua mikopo wanaposhindwa kulipa.
- Kibali cha baraza la mawaziri kuanzisha taasisi hizi mbili. Yaani taarifa hizo zilishindwa kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu!
Wizara ya Mambo ya Ndani
Malipo ya sh 423,183,545 yalifanywa kwa watu wengine, lakini hayakuonyeshwa katika vitabu vya fedha kinyume na viwango vya kimataifa vya uhasibu (IPSAS).
Katika hili CAG anasema kuhusu wizara hiyo "Kulikuwa na udhaifu katika usimamizi wa mikataba vilevile nyaraka muhimu za mikataba hazikuletwa kwa uhakiki."
RAS Tabora
Mali na vifaa visivyohamishika vyenye thamani ya sh 12,233,800 ikiwa ni pamoja na jenereta, kompyuta, samani na friji, hazikuingizwa katika kumbukumbu za vitabu vya mali za kudumu.
Taarifa za kifedha zimeandaliwa pungufu kwa kiasi cha sh 12,233,800 (inawezekana kuna mtu katumia fedha za umma kujinunulia vitu vyake mwenyewe)?
Vifaa vyenye thamani ya sh 19,693,560 vilinunuliwa lakini havikuingizwa vitabuni. Hatukuthibitisha kama vifaa hivyo vilipokewa na kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mkaguzi akatudokeza hali ilivyo katika kusimamia fedha za Watanzania:
Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2010, serikali ilikuwa na madeni yasiyotarajiwa yaliyofikia kiasi cha sh 26,276,785,317 yaliyohusisha mafungu kumi na mawili ambayo asili yake haikuonyeshwa kwenye vitabu. (Yaani kuna madeni ambayo tunajua ni madeni lakini hakuna ushahidi wa maandishi ya kwanini tunadaiwa!)
Sheria haitakiwi kudhamini deni la chombo chochote kwa zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazokopwa. Mkaguzi Mkuu anatudokeza kuwa hii serikali ya CCM ikiongozwa na watu wale wale imefanya yafuatayo:
Serikali ilidhamini kampuni tatu zaidi ya kiwango cha mkopo kwa sh 60,864,285,978 kinyume na sheria.
Mkaguzi akatuambia kitu kingine hapa:
Kama nilivyobainisha katika Sura ya IV, kwa ujumla mali za serikali zimeongezeka kwa asilimia 13 kutoka mwaka 2008-09 hadi mwaka 2009-10 (kufikia thamani ya karibu shilingi trilioni 8).
Hata hivyo, serikali haina rejista ya mali za taifa kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za mali.
Kwa maneno mengine ni kuwa tunaambiwa tuna mali yenye thamani ya trilioni 8 lakini tukiiuliza serikali unaweza kutuambia ni mali gani ya taifa hili haiwezi kwani haina rekodi ya mali zetu zote. Kutokana na hilo Mkaguzi anatoa ushauri huu "Ninaishauri serikali kuweka mali za taifa katika daftari au rejista, kufanya usuluhishi mara kwa mara wa kumbukumbu za mali katika taarifa za fedha jumuifu za taifa. Ikumbukwe kwamba mali bila daftari hupotea bila ya habari."
Mashirika ya umma
Kama unafikiria tatizo la utunzaji kumbu ni tatizo la serikali za mitaa au serikali kuu peke yake na haliko kwenye mashirika ya umma utakosea na kupaisha kama yule jamaa wa Ghana alivyopaisha kwenye Kombe la Dunia mwaka jana.
Kwenye mashirika yetu ya umma ambayo mengine viongozi wake wanachukuliwa kuwa ni makini na wana weledi wa hali ya juu. Je, na wao wanajua umuhimu wa kanuni hii ya ‘mali bila daftari'?
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
shilingi milioni 40 - malipo ya simu za mikononi na posho za simu kwa wajumbe wa bodi, kwa viwango vilivyopitishwa vya dola za marekani 600 na posho ya simu dola 350 kwa Mwenyekiti wa Bodi,dola 300 kwa Makamu Mwenyekiti na dola 250 kwa wajumbe wengine wa bodi, hii ni kinyume na taratibu zilizokubalika za utawala bora.
(Wenzetu wanajilipa kwa viwango vya dola wakati wengine kwenye serikali ile ile labda hata taasisi hiyo hiyo wanalipwa kwa viwango vya madafu!)
Mamlaka ya Maji Safi na Taka (Tanga) shilingi milioni 30 - Vifaa vya ujenzi vilivyonunuliwa lakini haikuthibitika kama vilipokewa eneo la ujenzi.
Mkaguzi Mkuu anatuambia kuwa "Baadhi ya mashirika yameonekana kuwa na kawaida ya kuwa na udhaifu mkubwa katika kutunza kumbukumbu za manunuzi unaosababishwa na ukosefu wa taaluma katika kutunza kumbukumbu, ukosefu wa nafasi katika ofisi za vitengo vya manunuzi na kupoteza nyaraka bila sababu za msingi.
Madhara ya hali hiyo ni kuwa na manunuzi yasiyofuata sheria, udokozi wa mali na kupotea kwa mali za umma."
Na akaongeza kuwa "Tulibaini pia kutoweka bayana mapato na matumizi kama inavyotakiwa na matakwa ya viwango vya kihasibu hali ambayo inaweza kusababisha vitendo vya ubadhirifu.
Kwa upande wa matumizi, tumegundua udhaifu katika mifumo ya ndani ya udhibiti wa malipo, kutokuwepo kwa nyaraka za kuthibitisha malipo"
Sasa hii yote ni mifano michache tu ya jinsi gani tuna tatizo kubwa sana katika usimamizi wa fedha zetu lakini zaidi tatizo la viongozi ambao wanavumilia tabia hii miaka nenda rudi. Mapendekezo yaliyotolewa na CAG mwaka huu kuhusu utunzaji wa kumbukumbu hayana tofauti na mapendekezo yake ya miaka 5 iliyopita.
Lakini tufanye nini? Tuendelee kusubiri mwaka mwingine tuone kama tumejifunza somo la ‘mali bila daftari'. Au tuendelee kusubiri viongozi wa upinzani waje na orodha nyingine ya ‘mafisadi'?
Ndugu zangu, wanaosema ‘wamejivua gamba' wanatutania. Huwezi kujivua gamba wakati chini ya gamba kuna gamba lenye gamba.
Huwezi kujivua gamba kwa kuwaondoa watu wanne kwenye chama wakati kuna maelfu ya watendaji serikali ambao wanafanya gamba lisiwe gamba tu iwe ni gamba sugu. Gamba hili halivuki kwa kutambulisha viongozi wapya au kwa kubeza watu.
Gamba linavuliwa kwa kuvunja vunja mfumo wa utawala wa kifisadi ambao niliandika habari zake zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Nilisema hivi katika makala yangu ya Septemba 2009 Kuuelewa mfumo wa Utawala wa Kifisadi "Ndiyo maana nimesema awali kuwa tatizo letu siyo Rostam, Lowassa, Chenge au Yona; hawa ni dalili tu ambazo tunaweza kuziondoa barabarani.
Tutakuwa hatuna hekima kama tunaamini kuwa tukiwaangusha hawa kutoka madarakani basi ufisadi utakwisha. Tusipobadilisha mfumo wa kiutawala wa ufisadi tutaendelea kuzalisha mafisadi tu. Haijalishi ni chama gani kiko madarakani."
Leo nilichohofia ndicho kimetokea; na wapo watu wanataka tuamini kuwa ati CCM imebadilika wakati sheria na mfumo wa sheria bado upo ule ule. Nilisema kuwa kama kiwanda kinatengeneza magari yenye hitilafu fulani haitoshi kuyaondoa magari hayo barabarani lakini pia kuangalia kiwanda kinachotengeneza na mitambo yake ikoje.
Ndugu zangu, matatizo haya niliyoyadokeza kwa haraka haraka ni dalili tu kuwa ufisadi si tendo la mtu mmoja ni utamaduni. Tunapozungumzia Katiba mpya kimsingi tunataka kubadilisha kabisa mfumo uliojenga utamaduni wa kifisadi.
Katiba mpya ni suluhisho kubwa la lazima la kuubomoa mfumo tuliojenga kwa karibu miaka hamsini. Wale wanaodhania Katiba mpya inahusu kuiondoa CCM madarakani hawajajua tunachogombania.
Tunagombania nafasi ya kujenga upya nchi yetu katika misingi ambayo itahakikisha kuwa ufisadi kweli unabakia ni vitendo vya watu wachache na siyo zao la mfumo uliopo.
Tunachotaka na kubadilisha kabisa jinsi gani tunatawaliwa, na jinsi gani tunawawajibisha watawala wetu.
Chini ya mfumo huo mpya watu wote wanaofanya mambo kama haya wanawajibishwa kuanzia mfagizi wa shule ya vidudu hadi mpigiwa saluti mkuu wa taifa letu.
Lakini hili halitofanikiwa hadi Watanzania tutakaposema ‘imetosha'. Mpaka tutakapoona madudu haya na kuyaona ni kero ya kweli. Tusipofanya hivyo tutaendelea kucheza kwenye hili tope na tusipoangalia tutawaridhisha na watoto wetu mfumo huu ambao unatia kinyaa.
Katika jitihada za kujivua gamba serikali iwasimamishe mara moja viongozi na watendaji wote ambao wamehusishwa na kuficha vitabu vya mapato na matumizi na ambao wameshindwa kutoa taarifa za fedha za Watanzania zinatumika vipi.
Wakishawasimamisha wafanye uchunguzi na wale ambao wataonekana wameshindwa kushika nafasi zao watimuliwe ili waingizwe Watanzania wengine.
Hakuna semina au warsha inayoweza kuwasaidia watu hawa kubadilika. Serikali ikifanya hivyo mara moja ndio tutaanza kuzungumzia kweli ‘kujivua gamba!'
Niandikie:
mwanakijiji@jamiiforums.com