Kilimanjaro Stars yawafariji Watanzania
Uganda mabingwa wa Chalenji 2009
Michael Momburi,Kampala
KILIMANJARO Stars jana jioni iliwafariji Watanzania baada ya kuifunga Burundi mabao 3-2 huku ikicheza soka lisilovutia na kuchukua ushindi wa tatu wa Kombe la Chalenji.
Stars ambayo ilikuwa na wachezaji wake wote tegemeo kama Shadrack Nsajigwa na Kelvin Yondani waliokosekana katika mechi iliyopita dhidi ya Kenya, ilicheza soka la kuonekana dakika 30 za mwisho.
Kiwango hicho kilionekana kupanda haswa baada ya kuingia kwa Nizar Khalfan na Mussa Hassan pamoja na kupata bao la kusawazisha na la ushindi.
Burundi ambayo ilikuwa ikishangiliwa sana na mashabiki wa Uganda ilitawala idara zote kwa takribani dakika 60 za mchezo huku wakipiga pasi nyingi kadri wanavyotaka.
Stars ambayo beki wake wa kushoto Juma Jabu alicheza chini ya kiwango, iliitumia dakika mbili kupata bao la kuongoza lililofungwa na Mrisho Ngassa ambaye aliunasa mpira na kuwachomoka mabeki wa Burundi waliokuwa wakijipanga.
Mpira huyo ulianza kwa kasi ya kawaida, lakini dakika ya nne Henry Joseph alizidiwa ujanja na kumkwatua mshambuliaji wa Burundi, Nahimana Claude na kusababisha penalti ambao ilifungwa kirahisi na Irambona Abdallah dakika ya tano.
Stars ambayo haikuwa ikipandisha mashambulizi ya haraka kama katika mchezo dhidi ya Rwanda na Zanzibar, ilitengeneza nafasi nzuri dakika tisa, lakini Mrwanda aliponasa pasi ya Henry Joseph akakokota na kupaisha.
Burundi ambao bado walionekana kutulia na kupanga mashabulizi ya hatari kimahesabu, walikuwa wakimiliki mpira kwa kiasi kikubwa lakini Nsajigwa aliwaponyoka dakika ya 16 na kupandisha shambulizi kali lakini shuti lake likapaa.
Warundi hao wakimtegemea zaidi mshambuliaji wao Nahimaha Claude mwenye mabao matatu, waliivamia ngome Stars mara kadhaa na kuitoa kijasho.
Nahimana alikokota mpira na kumvuka Henry Joseph na Kelvin Yondani, mashabiki wote wa Tanzania wakaweka mikono kichwani lakini kipa Shabaan Dihile akauwahi miguu kwa mchezaji huyo.
Burundi chini ya kocha wake Gilbert Younde ambae juzi alisema Tanzania haiponi, ilipata bao la pili dakika ya 42 kupitia kwa Jafari Jumapili aliyeunganisha krosi ya Nahimana.
Kipindi cha pili kilianza kwa Burundi kuingia kwa kasi na kukosa nafasitatu za wazi, lakini Stars ilijipanga na kusawazisha dakika 68 kupitia kwa Jerry Tegete ambae alipokea krosi Shadrack Nsajigwa,mchezaji mwenye umri mkubwa kwenye kikosi cha Stars.
Tanzania ilionyesha uhai baada ya kupata bao hilo ambapo walitulia na kupiga pasi fupi fupi huku Burundi wakiwa wamerudi kujilinda lakini wakawa wanapanga mashambulizi ya kushtukiza ambayo yalikuwa yakiwaweka kwenye wakati mgumu Yondani na Jabu.
Dakika ya 76 Danny Mrwanda ambae alikuwa akicheza huku akihisi maumivu kwenye enka ya kulia, aliifungia Stars bao la ushindi kwa shuti baada kunasa pande la Ngassa.
Mrwanda ambaye alifikisha mabao matatu katika mchezo huo, alionekana kuichachafya safu ulinzi ya Burundi sambamba na Ngassa lakini viungo walikuwa wakiwapandishia mipira ya juu ambayo mara nyingi haikuwa na madhara kwa Burundi.
Katika mchezo huo Burundi ilionekana kujiamini zaidi huku kocha wake Younde akiwa amesimama kwa dakika zote tisini kuhamasisha vijana wake ambao walilala uwanjani baada ya kipyenga cha mwisho cha mwamuzi Issa Kagambo wa Rwanda.
Kocha wa Stars, Marcio Maximo alisema vijana wake walipigana kufa kupona kusaka ushindi huo kwani Burundi ilimiliki sana hususani kipindi cha kwanza.
"Tulijipanga vizuri na wachezaji wangu wamecheza mpira mzuri kipindi cha pili, michezo hii imetusaidia kuelewa zaidi timu na ni maandalizi mazuri kwa michuano ya CHAN."
Kocha wa Burundi, Younde alilaumu safu yake ya ulinzi kwa kushindwa kulinda ushindi huku washambuliaji wakiwa na papara walipokuwa wakikaribia lango la Tanzania.
Kwa ushindi huo Stars imejinyakulia dola 10,000 tofauti na awali ilivyotuwa jijini hapa ambapo mashabiki walikuwa wakiipa nafasin kubwa ya kutwaa ubingwa.
Stars; Shabaan Dihile,Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Henry Joseph, Kiggi Makasi/Nizar Khalfan, Nurdin Bakar/Jerry Tegete, Danny Mrwanda/Mussa Mgosi, Mrisho Ngassa na Athuman Iddi.
Source:
Mwananchi Read News