Saleh Jembe kaandika;
Mfano mzuri ni picha hii inayomuonyesha mzazi wa mwanasoka maarufu zaidi nchini Mbwana Samatta akiwa amekaa kwenye ngazi za uwanja wa ndege kumsubiri mwanaye awasili.
Ally Samatta alikuwa na furaha ya mwanaye kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wanaocheza Afrika. Aliwasili saa nane usiku, lakini mzee alikuwa pale.
Kila mmoja anajua juhudi binafsi za mzee huyo kumsaidia mwanaye kufikia hapo alipo. Wengi tumemjua baada yam zee huyo na familia yake kupambana tokea mwanzo, mimi ninaamini anastahili heshima kubwa ya mzazi na mlezi bora kabisa.
Hakuna kiongozi wa Fat, TFF, Simba au kwingine aliyewahi kumsaidia wakati akipambana kwa ajili ya Mbwana.
Ameleta heshima kubwa kwa taifa kupitia mwanaye, lakini leo anafikia kwenye ngazi ambazo nadiriki kusema alikaa chini uwanja wa ndege.
Hoja yangu iko hivi, kweli Mzee Samatta hasitahili kutumia sehemu ya VIP ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere?
Nauliza tena, unawajua wangapi waliorejea nchini na kuitumia sehemu hiyo wakiwa hawana kubwa walilotoa kwa ajili ya taifa letu. Kungekuwa na ubaya gani Mzee Samatta angekaa kule wakati akimsubiri mwanaye, halafu wangeungana na watu wengine wakati akitoka nje?
Mara ya mwisho, niliona wakienda kumpokea Kocha Mart Nooij upande wa VIP ambao waliomba ili afikie wakati anawasili. Vipi Baba Samatta na familia yake waonekane hawafai na kwenda kukaa chini?
Hata kama wanatokea Uswahilini kwetu, lakini heshima yao wanastahili kupewa. Viongozi wa TFF wanaonekana hawajali, waliona ni jambo la kawaida tu.