Kithuku
Naeleweka mantiki ya hisia zako. Pole sana kama umeumizwa na huu mjadala. Na najua kuna watu wataumia zaidi. Na naamini kabisa Kikwete atavyofanya mabadiliko ya baraza la mawaziri hivi karibuni, mjadala tunaoufanya hivi sasa utakuwa ni moja ya mambo ambayo yatamgusa. Hatupaswi kufika mahali ambapo tukalipeleka taifa letu katika mazingira ambayo baadhi ya watanzania wenzetu watajilaumu kwa kuwa wachaga! Hili lazima tuliepuke. Bahati mbaya wewe kithuku pamoja na watanzania wengi hamkuamka kukumea hisia hizo wakati CCM ilipokuwa ikitangaza kwamba CHADEMA ni chama cha wachaga. Unadhani wachaga walioko CHADEMA ama wanaotaka kushika nafasi za uongozi kupitia CHADEMA wanajisikiaje katika mazingira hayo? Let the golden rule apply and not the law of the jungle.
CHADEMA tumejitahidi kutumia busara zote kuepuka kuwataja watu majina, na tuliwaonya CCM kuwa wasitufikishe mahali tukaanza kutaja, kumbuka tamko hili ambalo tuliotoa mwaka jana:
Utangulizi:
Mwishoni mwaka 2006 na mwanzoni mwaka huu shutuma kadhaa zimeelekezwa kwa CHADEMA na viongozi wake hususani Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe. Mwanzoni shutuma hizi zimekuwa zikitolewa na wanasiasa wanaojitoa kambi ya upinzani na kujiunga na CCM. Shutuma hizi ni pamoja na:
1. Kuwa CHADEMA awali kilianzishwa wakati wa ukoloni kikijulikana kama Chagga Development Manifesto (CHADEMA) ambacho bado kinaendelea na mwelekeo huo(Rejea Majira: 24/12/2006.;
2. CHADEMA ina mrundikano wa watu wa kabila la wachagga. Haipaswi kuwa chama cha demokrasia na maendeleo badala yake inapaswa kuitwa chagga development manifesto Rejea Mwananchi: 24/12/2006.(Hoja hii ilirudiwa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa wiki kadhaa mfululizo wakinukuliwa viongozi wachache waliojitoa kutoka upinzani).
Awali CHADEMA tulipuuza uzushi huu. Lakini kutokana na kauli hizi kurudiwa rudiwa mara kwa mara tunaamini kuwa uwongo na upotoshaji huu unaweza kugeuzwa na umma watanzania ukaaminishwa kuwa ndio ukweli. Aidha tunatoa taarifa hii kufuatia taarifa ya Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Aggrey Mwanri iliyochapwa katika vyombo mbalimbali vya habari 5 Januari 2007 ambapo CCM imetoa shutuma kadhaa kwa CHADEMA na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe. Pia taarifa hii imenatolewa kujibu shutuma kadhaa zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe kupitia maoni ya Mhariri wa gazeti la Mtanzania la tarehe 5 Januari 2007 yaliyokuwa na kichwa cha habari Wapinzani tafuteni njia bora za kukubalika.
SI KWELI KUWA CHADEMA NI CHAMA CHA WACHAGA KILICHOANZISHWA TOKA WAKATI WA KUDAI UHURU
Mtanzania yeyote mwenye ufahamu wa kawaida kabisa wa historia ya nchi yetu, atakubaliana nasi kuwa katika orodha ya vyama vya siasa vilivyokuwepo kabla ya uhuru, hakuna chama kilichoitwa CHADEMA. Ukweli ni kuwa CHADEMA ni chama kilichoanzishwa na kusajiliwa mara baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi. Hii inatufanya tubaki na maswali mengi kuhusu nia ya wanaosambaza uzushi huu.
SI KWELI KWAMBA CHADEMA IMEJAA WACHAGA
Kwa akili za kawaida, shutuma kwamba CHADEMA imejaa wachaga maana yake ni kwamba CHADEMA ina viongozi na wanachama wengi wachagga kuliko kabila lolote hapa Tanzania. Je ni kwa kiasi gani kauli hiyo ina ukweli?.
Katika safu ya juu ya uongozi wa kitaifa wa CHADEMA yenye viongozi sita: wenyeviti na makatibu mchaga ni mmoja tu-Mwenyekiti wa chama Taifa, Freeman Mbowe. Viongozi wengine wanatoka makabila mengine kama MuIraq, Myao, Mpemba na MuUnguja.
Aidha katika sekretariati ya chama taifa ambacho ndio chombo kinachosimamia utekelezaji wa kila siku wa shughuli za chama kikiwa na kurugenzi 9, kati ya wakurugenzi wake mchaga ni mmoja tu. Na wasukuma ni watatu. Kwa nini hawasemi kwamba CHADEMA ni chama cha wasukuma?
Kadhalika mpaka sasa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe ameteua wajumbe wanne wa kamati kuu, kati yao hakuna na mchaga hata mmoja na kati yao wawili ni wahaya, Profesa Mwesiga Baregu na Balozi Ngaiza. Kwa nini hawakusema kwamba CHADEMA ni chama cha wahaya?
Kwa upande mwingine kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi uliopita, jimbo ambalo CHADEMA iliongoza kwa uwingi mkubwa zaidi wa kura ni Tarime ikiwa asilimia zaidi ya 64. Kama CHADEMA ni chama cha wachaga kwa nini jimbo la kwanza lisingekuwa la mkoa wa Kilimanjaro?
Kati ya majimbo kumi ambayo CHADEMA ilifanya vizuri zaidi, jimbo la Kilimanjaro ni moja tu la Moshi mjini huku mikoa kama Kigoma, Rukwa ikiwa na majimbo mawili ambayo CHADEMA imefanya vizuri zaidi. Kama CHADEMA ingekuwa chama cha wachaga si ingefanya vizuri zaidi katika majimbo ya Kilimanjaro?
Je, wanataka kutuambia kuwa Mara, Kigoma, Rukwa na mikoa mingine ambayo CHADEMA imefanya vizuri kote kumejaa wachaga?
Kwa mantiki hiyo basi, si kweli kwamba CHADEMA ni chama kilichojaa wachaga. CHADEMA ni chama cha kitaifa. Kinachojumuisha wanachama na wapenzi wa asili na hali mbalimbali. Lakini swali la kujiuliza ni je wachaga hawana haki ya kuwa sehemu ya viongozi katika taifa na wanachama wa CHADEMA?
Zaidi ya hayo tunawashangaa wakitoa hoja kwamba CHADEMA imejaa wachaga. Lakini tunawashangaa zaidi kwa kuwa hatukuwasikia akisema chochote pale Rais Kikwete alipoteua wachaga na watanzania wenye asili ya Kilimanjaro wengi zaidi katika baraza la mawaziri kuliko makabila mengine. Je, kwa mantiki ya wazushi kama hao serikali ya Kikwete ni ya wachaga? Je, kwa kuwa wachaga ndio kabila lenye wabunge wengi zaidi kati ya wabunge wa viti maalumu wa CCM na CHADEMA, Je kwa kigezo hiki tu tuseme kwamba CCM na CHADEMA ni vyama vya wachaga? Je, kwa CCM kuwa na wabunge wa viti maalum wachaga hata katika mikoa mingine ya nchi yetu zaidi ya Kilimanjaro wanapotoka wachaga je, kwa uchambuzi wa wazushi kama hao wanaweza kusema kwamba CCM ni chama cha wachaga?
Hatukupenda kujadili viongozi kwa kutazama makabila yao. Lakini tumeamua kutoa uchambuzi huu kwa sababu suala la ukabila ni nyeti sana kwa mustakabali wa nchi yetu na kwamba kwa kutoa mifano hai tutathibitisha wazi uzushi wa watu hawa. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kuasa kwamba kufanya dhambi ya ubaguzi ni kama kula nyama ya mtu, ukianza huwezi kuacha.
Sisi tunaamini kauli za wazushi kama hawa zinapandikiza mbegu ya ubaguzi miongoni mwa watanzania na kuwashawishi watu kutazamana kwa misingi ya makabila yao. Tukiwaruhusu watu kama hawa tutaweka mashakani mshikamano na amani yetu hapa nchini. Tunatoa mwito kwa watanzania kupuuza na kukumea kauli za viongozi kama hawa. CCM inaendelea kukumbatia wazushi hawa na uzushi wao, watanzania watakuwa na kosa gani wakianza kuamini kwamba chama tawala kinapandikiza mbegu za ubaguzi? Na kwa upande mwingine, tunatoa rai kwa vyombo vya habari kuchambua kwa kina kauli za watu kama hawa kwani uwongo ukisemwa sana wananchi wanaweza kuaminishwa kwamba ni ukweli.
Katika taarifa yake CCM imeinukuu shutuma ya wanaotoka upinzani ya kulalamikia tabia za ubabe na udini ndani ya CHADEMA? Ni ubabe upi huo? Ni udini upi huo ulioko katika CHADEMA? Hivi katika vyama vikuu vya siasa hapa nchini kuna chama ambacho safu yake ya kitaifa ina uwiano wa kidini kama CHADEMA? Mwalimu Nyerere aliwahi kusema pia kwamba katika kutafuta uongozi kuna watu wanaweza kutumia vigezo vya kijinga kama udini na ukabila kujihalalisha ili kufikia malengo yao na ndivyo wanavyofanya watu jamii hii.
Tamko linaendelea hapa:
http://www.chadema.net/tamko/2007/mwanri.php
CCM hawakusikia kabisa, kwa mjadala huu wa sasa naamini kabisa, hata CCM wakirudia tena kuanza kutaja kwa majina wachaga wachache walioko CHADEMA na kuita CHADEMA ni chama cha wachaga utakuwa wa kwanza kuwakemea.
CCM wamesema CHADEMA ni chama cha wachaga mpaka baadhi ya wananchi wakaanza kuamini. Njia pekee ni kuufanya umma kuamini kwamba wachaga kama watanzania wengine wowote wapo kila mahali ikiwemo CCM na wana haki hiyo kabisa. And that is the spirit of Mbowe's statement- inawezekana habari husika haijabeba sura hiyo kwa ukamilifu wake kwa kuwa kuna mengi aliyoyasema yameachwa lakini natumai ujumbe umefika.
Unaniruhusu niondoke?
JJ