Chama cha Demokrasia na Maendeleo hakina ubavu wa kuwakataa hawa wabunge wao.
Kwanza, kuna viashiria kila mahali kwamba wako bungeni kufuatia nia, mchakato, na baraka za chama.
Pili, itaibuka hoja tunapoelekea kwenye ngwe za uchaguzi mwakani, kwamba kama walipokelewa mapapa wa mafisadi kama akina Lowassa, Sumaye na Lazaro Nyalandu, wakasafishwa, wakasifiwa na kugombea, seuze akina Halima Mdee?
Hii hoja moja tu inatosha kutuliza hali ya hewa na kuleta mtangamano Chademani.
Isitoshe, mwenyekiti atadai, kama anavyodaigi kila mwaka, kwamba hii ni fursa ya pekee kuunganisha nguvu zote za peponi na motoni za wafuasi watiifu na wasaliti ili kuingia Ikulu kwa kishindo, au kama wao waitavyo - mafuriko!
Mwisho, siasa hainaga maadui wala marafiki wa kudumu. Ndiyo maana juzi Zitto Kamwe alikuwa Msisiemu, jana akatimkia Chadema, leo yuko siti ya mbele kabisa Eisitii, na, nani ajuaye, huenda kesho akapokelewa kwenye chama cha Republican Marekani!