Mkurugenzi wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), John Mnyika ameibuka na kuzungumzia tuhuma kwamba chama hicho ni cha wachaga. Mnyika ambaye katika uchaguzi uliopita alikuwa mgombea wa Ubunge katika jimbo la Ubungo mkoani Dar es salaam amezungumzia suala hili kutokana na hivi karibuni kujitokeza kwa wanachama wanaojitoa katika kambi ya upinzani na kuingia Chama cha Mapinduzi(CCM) ambao pamoja na mambo mengine kutoa shutuma kwamba CHADEMA ni chama cha wachaga.
Hivi karibuni, magazeti kadhaa ya kila siku(si gazeti hili) yamemnukuu aliyekuwa kiongozi wa chama cha wananchi CUF akiwa amezunguka vyama vya UMD, UDP, NCCR-Mageuzi, CHADEMA , na kuanzisha chama cha ULIMO bila mafanikio,Aman Nzugile Jidulamabambasi( maarufu kama Jidula ama Jidu), alirejea CCM, akitokea chama cha wananchi CUF ambapo alikuwa mgombea ubunge huku akitoa shutuma za hali ya juu kuhusu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari(MAELEZO).
Itakumbukwa kuwa baada ya kurejea CCM, Jidulamabambasi alidai na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa vyama vya upinzani havina mwelekeo na kwamba vinaubaguzi , huku akisisitiza kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ni chama cha kikabila na kwamba kimejaa wachagga na kuongeza kuwa CHADEMA kilianzishwa kabla ya uhuru kwa maslahi ya wachagga ambapo kilikuwa na jina la Chagga Development Manifesto(CHADEMA).
"Kwa hulka na tabia ya Jidula tunayemfahamu, tunaamini kuwa maneno haya hata yeye mwenyewe anaamini si ya kweli na pengine alishinikizwa na CCM aseme hivyo kwani propaganda za namna hii zimekuwa zikitumiwa na CCM kwa muda mrefu dhidi ya CHADEMA, amesema Mnyika.
Aidha Mnyika alisisitiza, "Na kwa mtu kama Jidula mwenye hulka ya kutafuta uongozi kwa udi na uvumba, sio ajabu kutamka maneno ambayo hata mwenyewe ama hayaamini au hayajui. Kwa hiyo namtaka Jidula athibitishe kauli yake kuwa CHADEMA ni chama cha wachagga kilichikuwepo kabla ya uhuru wa Tanganyika, kwa upande mmoja. Lakini pia kupinga kauli hiyo ya upotoshaji ya Jidula kwa upande wa pili".
Akizumgumzia shutuma kwamba CHADEMA ni chama si siasa kilichoanzishwa kabla ya uhuru kikiitwa Chaga Development Manifesto Mnyika alisema " kwa mtanzania yeyote mwenye ufahamu wa historia walau ya kiwango cha shule ya msingi, atakubaliana nasi kuwa katika orodha ya vyama vya siasa vilivyokuwepo kabla ya uhuru, hakuna chama kilichoitwa CHADEMA"
Kwa msomi wa kiwango cha Jidula kushindwa kung'amua vitu vidogo kama hivi, kunazua maswali mengi kuliko majibu hasa kuhusu uhalali na usahihi wa elimu yake kwa upande mmoja kama ni kweli amepotosha kwa kutojua. Lakini pia kunazua maswali kuhusu kiwango cha uzalendo wa Jidula anapokuwa anatafuta nafasi ya uongozi kama kweli alikuwa anajua lakini ameamua kuupotosha umma wa watanzania kwa malengo yake ya kisiasa katika chama hicho.
Kwa upande mwingine akijibu shutuma ya kwamba CHADEMA imejaa wa wachaga, Mnyika, "Pengine hatuna hakika na uwezo wa Jidula wa lugha ya kiswahili, labda pengine anatumia maneno asiyoyajua maana yake. Kwa mfano Jidulla anaposema CHADEMA imejaa wachagga maana yake nini?. Kwa akili za kawaida, maana yake ni kwamba CHADEMA ina viongozi na wanachama wengi wachagga kuliko kabila lolote hapa Tanzania. Kama Jidula alikuwa na ujumbe huo!, Je ni kwa kiasi gani kauli hiyo ina ukweli?"
Akitoa takwimu kuhusu idadi ya wachaga katika CHADEMA Mnyika ameweka wazi kuwa, "Katika safu ya juu ya uongozi wa kitaifa wa CHADEMA yenye viongozi sita: wenyeviti na makatibu mchaga ni mmoja tu-Mwenyekiti wa chama Taifa, Freeman Mbowe. Wazanzibari ni wengi zaidi kati ya hao viongozi sita. Kwa nini Jidula hakusema kwamba CHADEMA ni chama ambacho kimejaa wazanzibari?
Aidha katika sekretariati ya chama taifa ambacho ndio chombo kinachosimamia utekelezaji wa kila siku wa shughuli za chama kikiwa na kurugenzi 9, kati ya wakurugenzi wake mchaga ni mmoja tu. Na wasukuma kabila la Jidula ni watatu?. Kwa nini Jidula hakusema kwamba CHADEMA ni chama cha wasukuma?
Kadhalika mpaka sasa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe ameteua wajumbe wanne wa kamati kuu, kati yao hakuna na mchaga hata mmoja na kati yao wawili ni wahaya, Profesa Mwesiga Baregu na Balozi Ngaiza. Kwa nini hakusema kwamba CHADEMA ni chama cha wahaya?
Kwa upande mwingine kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi uliopita, jimbo ambalo CHADEMA iliongoza kwa uwingi mkubwa zaidi wa kura ni Tarime ikiwa asilimia zaidi ya 64. Kama CHADEMA ni chama cha wachaga kwa nini jimbo la kwanza lisingekuwa la mkoa wa Kilimanjaro? Kati ya majimbo kumi ambayo CHADEMA ilifanya vizuri zaidi, jimbo la Kilimanjaro ni moja tu la Moshi mjini huku mikoa kama Kigoma, Rukwa ikiwa na majimbo mawili ambayo CHADEMA imefanya vizuri zaidi. Kama CHADEMA ingekuwa chama cha wachaga si ingefanya vizuri zaidi katika majimbo ya Kilimanjaro? Je, Jidula anataka kutuambia kuwa Mara, Kigoma, Rukwa na mikoa mingine ambayo CHADEMA imefanya vizuri kote kumejaa wachaga?
Kwa mantiki hiyo basi, si kweli kwamba CHADEMA ni chama kilichojaa wachaga. CHADEMA ni chama cha kitaifa. Kinachojumuisha wanachama na wapenzi wa asili na hali mbalimbali.
Zaidi ya hayo namshangaa Jidula akitoa hoja kwamba CHADEMA imejaa wachaga. Lakini namshangaa zaidi Jidula kwa kuwa hatukumsikia akisema chochote pale Rais Kikwete alipoteua wachaga wengi zaidi katika baraza la mawaziri. Je, kwa mantiki ya Jidula serikali ya Kikwete ni ya wachaga? Je, kwa kuwa wachaga ndio kabila lenye wabunge wengi zaidi kati ya wabunge wa viti maalumu wa CCM na CHADEMA, Je kwa kigezo hiki tu tuseme kwamba CCM na CHADEMA ni vyama vya wachaga? Je, kwa CCM kuwa na wabunge wa viti maalum wachaga hata katika mikoa mingine ya nchi yetu zaidi ya Kilimanjaro wanapotoka wachaga je, kwa uchambuzi wa mtu kama Jidula anaweza kusema kwamba CCM ni chama cha wachaga?
Nimeamua kujibu shutuma hizo kwa sababu suala la ukabila ni nyeti sana kwa mustakabali wa nchi yetu. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kuasa kwamba kufanya dhambi ya ubaguzi ni kama kula nyama ya mtu, ukianza huwezi kuacha. Naamini kauli za watu kama Jidula zinapandikiza mbegu ya ubaguzi miongoni mwa watanzania na kuwashawishi watu kutazamana kwa misingi ya makabila yao. Tukiwaruhusu watu kama hawa tutaweka mashakani mshikamano na amani yetu hapa nchini.
Mwalimu Nyerere aliwahi tena kusema kwamba katika kutafuta uongozi kuna watu wanaweza kutumia vigezo vya kijinga kama udini na ukabila kujihalalisha ili kufikia malengo yao na ndivyo wanavyofanya watu jamii ya Jidula.