GE2025 CHADEMA: Tangu Oktoba 1 hadi 25, wametekwa watu 52

GE2025 CHADEMA: Tangu Oktoba 1 hadi 25, wametekwa watu 52

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Mwanamwana

Platinum Member
Joined
Aug 1, 2011
Posts
9,604
Reaction score
22,722
TAARIFA YA UTEKAJI
​
Chadema tumeendelea kufuatilia kwa karibu matukio mbalimbali ya utekaji wa watu yaliyotokea nchini ndani ya siku ishirini na tano kuanzia tarehe 01 hadi 25 Oktoba 2025. Katika kipindi hiki, jumla ya watu 52 wametekwa, wengi wao ni viongozi na wanachama wa Chadema, pamoja na baadhi ya wanachama wa vyama vingine vya siasa na wananchi wa kawaida. Matukio haya yamezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii kuhusu usalama na uhuru wa raia. Matukio hayo ni kama yafuatayo:

RODRICK KAKWAYA
Mnamo usiku wa kuamkia tarehe 01 Oktoba 2025, Mwalimu Rodrick Kakwaya wa shule ya sekondari Usevya mkoani Katavi alitekwa nyumbani kwake mbele ya familia yake. Kakwaya, aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Shule, alijulikana kama mtetezi wa haki za binadamu na mkosoaji wa mfumo kupitia makundi ya WhatsApp. Ndugu na jamaa wamethibitisha kutoweka kwake baada ya kutembelea vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio ya kumpata.

LOBEZI KULILO MASANYIWA
Mnamo tarehe 01 Oktoba 2025, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Chadema Wilaya ya Busega alitekwa na watu wasiojulikana akiwa kazini kwake Nyamikoma. Mashuhuda wameripoti kuwa alitishiwa kwa bunduki na kulazimishwa kuingia kwenye gari na watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao, kisha kuondoka naye kuelekea Barabara ya Mwanza. Hadi sasa hajulikani alipo.

ISSA HAMISI KAUDO
Mnamo tarehe 03 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Ikungi alitekwa na watu wasiojulikana baada ya kupokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama mfanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, aliyemwomba afike kwa ajili ya kazi ya kuchomelea. Alipofika eneo la miadi, alilazimishwa kuingia kwenye gari aina ya Land Cruiser na kuondoka nao kusikojulikana. Tangu wakati huo, hajulikani alipo.

PAUL VESLAS
Mnamo tarehe 03 Oktoba 2025, dereva bodaboda alitekwa baada ya kuchukuliwa na Issa Hamisi Kaudo kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, akielezwa kuwa kuna kazi ya kufanya. Alipofika kwenye eneo hilo, waliokuwepo walimuingiza kwa nguvu kwenye gari aina ya Land Cruiser na kuondoka naye kusikojulikana. Hadi sasa hajulikani alipo.

EVARIST JAMES RAMADHANI
Mnamo tarehe 03 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Bavicha Jimbo la Ikungi alitekwa akiwa nyumbani kwake
baada ya kupigiwa simu na kuambiwa atoke nje. Tangu alipotoka, hajarejea nyumbani na hajulikani alipo hadi sasa.

ARON JONAS MASSAWE NA KELVIN INDIG MUSHI
Mnamo tarehe 3 Oktoba 2025, walitekwa baada ya kupeleka simu kwa mteja aliyekuwa amefika katika maeneo ya Kanisa la KKKT Kariakoo. Hadi sasa, hawajulikani walipo.

AMOS PAMBALA
Mnamo tarehe 04 Oktoba 2025, Katibu Mwenezi wa CHADEMA Kata ya Mafisa, Jimbo la Morogoro Mjini alitekwa baada ya kupokea simu na kuitikia wito. Tangu wakati huo, amepotea na hajulikani alipo hadi sasa.

IBRAHIM MUHIDIN MFANGAVO NA VIJANA WENGINE WATATU
Mnamo tarehe 04 Oktoba 2025, katika Kijiji cha Kakola, Kata ya Bulyanhulu, Wilaya ya Kahama, vijana wanne walitekwa na watu wasiojulikana. Wa kwanza kutekwa alikuwa Ibrahim Muhidin Mfangavo, aliyetekwa nyumbani kwao mbele ya baba yake mzazi, Mzee Muhidin Mfarangavo. Vijana wengine watatu walitekwa walipokuwa wakifuatilia kwa bodaboda waliomteka Ibrahim, wakijaribu kuwafuatilia na kusaidia, lakini nao wakakamatwa na kuondoka nao kusikojulikana.

ABEDNEGO SANGA
Mnamo tarehe 04 Oktoba 2025, Katibu wa Bavicha Jimbo la Lupembe alitekwa akiwa kazini kwake katika duka la dawa. Watekaji waliwasili kwa gari aina ya Land Cruiser lisilo na namba za usajili, wakiwa na silaha za moto, wakaingia ndani ya duka na kumwondoa kwa nguvu, kisha kuondoka naye kusikojulikana.

ISAYA WILLIAM OUMA NA GIMASE JOSEPH
Mnamo Jumamosi, tarehe 4 Oktoba 2025, Isaya William Ouma, mwenyeji wa Sirari, alikodi gari dogo aina ya Toyota Probox kuelekea Mwanza, akiwa na dereva wake, Gimase Joseph, ambaye pia ni mkazi wa Sirari. Waliondoka asubuhi, lakini kufikia saa tisa alasiri simu zao hazikupatikana tena. Kwa mujibu wa mashuhuda, gari hilo liliendeshwa hadi eneo la MT Hotel, Tarime, huku likisindikizwa na gari jingine aina ya Land Cruiser. Baada ya kufika, Probox hiyo ilitelekezwa, na waliokuwamo walionekana wakipanda kwenye Land Cruiser na kuondoka kusikojulikana. Tangu wakati huo, Isaya na dereva wake hawajulikani walipo, na mawasiliano yao yamekatika kabisa.

ELIAS SAMWELI DOMISIANI
Mnamo tarehe 04 Oktoba 2025, mchungaji wa kanisa la Highway of Holiness Church (H.H.C) lililopo Mtaa wa Manyuki, Kata ya Lukobe, Morogoro, ametekwa na watu waliomwita kwa simu wakimhitaji kufungiwa solar. Baada ya kumuaga mke wake na kuondoka, hajarudi hadi leo. Aidha, mchungaji huyo pia ni mfanyabiashara wa solar.

HUMPHREY POLEPOLE
Mwanasiasa na mwanadiplomasia maarufu wa Tanzania ametekwa kuanzia usiku wa tarehe 6 Oktoba
2025, baada ya watu wasiojulikana kuvamia makazi yake mjini Dar es Salaam.

NTIHAKANIGWA KIBA
Mnamo tarehe 06 Oktoba 2025, alitekwa Tabora Mjini, Cheyo B, karibu na Mwanga Shop, kando ya Barabara ya Kitoma. Mpaka leo hajulikani alipo.

ROGERS YOHANA LUDOVICK
Mnamo tarehe 07 Oktoba 2025, mfanyabiasha wa miamala ya simu alitekwa katika eneo la Dumila. Gari nyeupe aina ya Land Cruiser yenye namba za usajili T324 ELK ilifika ofisini kwake majira ya saa 7 mchana ikiwa na watu wanne. Baada ya kufika, walishuka, wakamchukua kwa nguvu na kuondoka naye kusikojulikana.

RAMSO
Mnamo tarehe 07 Oktoba 2025, mtengenezaji wa maudhui mtandaoni kupitia Tik Tok, ambaye amekuwa msoaji wa utawala wa Rais Samia tangu mwaka 2024, alitekwa akiwa nyumbani kwake. Mpaka sasa hajaripotiwa kama amepatikana.

IBRAHIM RICHARD
Mnamo tarehe 8 Oktoba 2025, katika eneo la Magu, alitekwa na watu watano waliokuwa wamevalia kiraia. Walimchukua kwa nguvu na kumpakiza kwenye gari aina ya Land Cruiser, kisha wakaondoka naye kusikojulikana.

PADRE CAMILLUS NIKATA
Mnamo tarehe 8 Oktoba 2025, Padre Camillus Nikata wa Jimbo Kuu la Songea, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza, alitarajiwa kusafiri kuelekea Mwanza kwa basi la Superfeo baada ya kununua tiketi. Hata hivyo, tangu siku hiyo hajulikani alipo. Mizigo yake ilibaki chumbani kwake katika Seminari ya Mtakatifu Vianney, Songea, na simu yake haipatikani. Hatimae tarehe 18 Oktoba 2025 alipatikana katika mashamba ya Kijiji cha Mawa, Kata ya Hanga, Wilaya ya Namtumbo.

JERISON KERALIYO
Mnamo tarehe 09 Oktoba 2025, katika Mtaa wa Kishiri B, Nyamagana, karibu na banda la mkaa eneo la Kishiri Center karibu na Hoteli Kasanda, alitekwa na watu wanne waliotoka kwenye gari aina ya Land Cruiser nyeupe. Watu hao walimlazimisha kuingia kwenye gari kisha wakaondoka naye.

AYUBU JUMA
Mnamo tarehe 09 Oktoba 2025, dereva wa bodaboda alitekwa baada ya kuchukuliwa na wasichana wawili waliokuwa wanahitaji kupelekwa katika mgodi wa Matongo, ulio katika Kitongoji cha Matongo, Kata ya Ikungi, Wilaya ya Ikungi. Tarehe 12 Oktoba, mwili wake umeokotwa porini ukiwa umeuawa.

YAHAYA OMARY LIHUPA
Mnamo tarehe 09 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Chadema tawi la Lumemo, kutoka Kata ya Lumemo
jimbo la Kilombero, alitekwa baada ya kuwabeba wanawake watatu kwenda katika mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mahutanga, Kata ya Lumemo. Hadi sasa hajulikani alipo.

WAKILI DASTAN MUJAKI
Mnamo tarehe 10 Oktoba 2025, saa 2 asubuhi, alichukuliwa ofisini kwake Bukoba na watu walijitambulisha kuwa ni Jeshi la Polisi bila kueleza sababu. Baada ya muda, mawakili wenzake walifika Kituo cha Polisi Bukoba na kuthibitishiwa kuwa yupo, lakini hawakuruhusiwa kuonana naye. Baadaye ilidaiwa kuwa amepelekwa Geita na kikosi maalumu cha Jeshi hilo. Hata hivyo, ufuatiliaji uliofanywa Geita haukuthibitisha kuwepo kwake. Mpaka sasa, hajulikani alipo.

CHIEF KALUMNA
Mnamo tarehe 12 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Bukoba, alichukuliwa nyumbani kwake na watu waliodai kuwa maafisa wa Jeshi la Polisi waliowasili kwa magari mawili na kumueleza kuwa anahitajika kituo cha polisi. Baada ya viongozi wa chama kufika kituoni kufuatilia taarifa hizo, waliambiwa kuwa hayupo, na baadhi yao pia walikamatwa. Baadaye, Jeshi la Polisi lilithibitisha kuwa linamshikilia Chief Kalumna.

BAZIRI WAZIRI
Mnamo tarehe 14 Oktoba 2025, Katibu wa Chadema wa Jimbo la Kyerwa alitekwa na watu sita wenye silaha akiwa katika eneo la biashara yake lililopo Kata ya Nkwenda, Wilaya ya Kyerwa. Watu hao walimchukua kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari aina ya Land Cruiser kisha kuondoka naye kusikojulikana. Hatimae tarehe 17 Oktoba 2025 Jeshi la Polisi limekiri kumshikilia.

RASHADI HAMZA
Mnamo tarehe 13 Oktoba 2025, mwanachama wa Chadema alitekwa na watu wasiojulikana katika eneo lake la kazi kwenye karakana ambapo hujihusisha na kazi za useremala. Watu hao walimchukua kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari aina ya Land Cruiser kisha kuondoka naye kusikojulikana. Tukio hilo lilitokea Kata ya Nkwenda, Wilaya ya Kyerwa.

ALBANI PETER MWALLO
Mnamo saa kumi jioni tarehe 15 Oktoba, mfanyabiashara wa mtaa wa Gogo na Narung'ombe, Kariakoo, alikamatwa na watu wanaosadikiwa kuwa askari wa kikosi maalumu na kupelekwa kusikojulikana. Alidaiwa kupelekwa kituo cha polisi Msimbazi lakini hakuingizwa, bali alipakiwa kwenye gari aina ya Land Cruiser Hard Top na watu waliovaa kiraia. Hadi sasa haijulikani yupo wapi.

NYAMALWA FIMBO NA WENZAKE 11
Mnamo tarehe 15 Oktoba 2025, alitekwa akiwa kazini katika ofisi ya BM Printing, iliyopo barabara ya tisa Dodoma Mjini Dodoma. Watekaji hao walimchukua yeye, mmiliki wa ofisi hiyo, pamoja na wafanyakazi wengine 10, na kufanya jumla ya watu 12 waliotekwa katika ofisi hiyo. Mpaka sasa, haijulikani walikopelekwa wala hali zao.

KIMASA PASTORY MWIKA
Mnamo tarehe 17 Oktoba 2025, majira ya saa tatu usiku, dereva katika kampuni ya Dangote Cement Mtwara, alitekwa na kundi la watu zaidi ya watatu waliokuwa wakitumia gari aina ya Land Cruiser. Mashuhuda wanasema kuwa wakati wa tukio hilo, Kimasa alikuwa ameketi katika kituo cha kusubiri daladala pamoja na wenzake wa kazini, ndipo walipofika watu waliodai kuwa askari wa Jeshi la Polisi na kumchukua kwa gari hilo. Tangu siku hiyo hadi sasa, haijulikani alipo.

REGAN DOMINIK KAILA
Mnamo tarehe 19 Oktoba 2025, Regan Dominik Kaila, mkazi wa mkoa wa Simiyu anayejihusisha na shughuli za udalali, aliripotiwa kutekwa na watu waliodai kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi akiwa mitaani. Ndugu na jamaa zake walifanya jitihada za kumtafuta kwa kutembelea vituo mbalimbali vya polisi, lakini waliambiwa kuwa hayupo mikononi mwao. Hata hivyo, baada ya siku saba kupita, Jeshi la Polisi lilithibitisha kwamba linamshikilia.

ABDALAH ABUBAKARI MKUKI
Mnamo tarehe 21 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Bavicha Kata ya Kikio, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, alitekwa na watu waliokuwa na silaha za moto. Tukio hilo lilitokea mchana, ambapo watekaji hao waliokuwa wakitumia gari aina ya Land Cruiser walimchukua kwa nguvu na kuondoka naye kuelekea kusikojulikana. Mpaka sasa, haijulikani alikopelekwa.

NICKOSON MUYEMBA
Mnamo tarehe 20 Oktoba 2025, Muyemba, ambaye aliwahi kuwa mgombea udiwani wa Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2020 jimbo la Mwibara, alitekwa akiwa katika stendi mpya ya Nyegezi jijini Mwanza. Mpaka sasa, haijulikani alikopelekwa.

JUMA IDD
Mnamo tarehe 21 Oktoba 2025, mfanyabiashara ambaye ni mwanachama wa CCM kutoka Sirari, alitekwa na watu wasiojulikana waliotumia risasi za moto kutawanya wananchi waliokuwa eneo la tukio. Hata hivyo, wananchi kwa ushirikiano na madereva wa bodaboda walifuatilia gari la watekaji, wakalizuia kwa kufunga barabara na kulilazimisha kuelekea kituo cha polisi.

HILDA MBINDA
Mnamo tarehe 21 Oktoba 2025, Bi. Hilda, mwalimu wa shule ya msingi katika kijiji cha Idibo, wilaya ya Gairo, aliripotiwa kutekwa nyumbani kwake akiwa na mtoto mdogo aliyekuwa naye, ambapo mashuhuda wanasema mtoto huyo ni mgonjwa. Tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, na mamlaka husika zimearifiwa kuhusu hali hiyo.

GIDO MBELE
Tarehe 22 Oktoba 2025, mwenyekiti wa Bavicha Jimbo la Kawe, aliripotiwa kutekwa katika eneo la Sinza Kivulini. Inadaiwa kuwa alitekwa na watu sita waliokuwa na silaha za moto wakiwa wamepanda gari aina ya Land Cruiser. Tukio hilo lilitokea katika ofisi ya mawakili alipokuwa Gido, ambapo watu hao walimchukua kwa nguvu na kuondoka naye kuelekea kusikojulikana.

ALBERT MACHUMU
Mnamo tarehe 24 Oktoba 2025, Albert Machumu alitekwa akiwa ofisini kwake na watu waliokuwa wakitumia gari aina ya Land Cruiser. Machumu amewahi kuwa mgombea katika uchaguzi wa Serikali za Mtaa wa Katoma kupitia Chadema, na pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Geita, hadi sasa hajulikani alipo.

MCHUNGAJI ELETH ELIAWAHA MTAITA
Mnamo usiku wa tarehe 24 Oktoba 2025, watu wasiojulikana wakiwa na silaha walivamia nyumba ya Mchungaji Eleth Eliawaha Mtaita wa Kanisa la KKKT, Usharika wa Buay, lililopo Babati Vijijini, mkoani Manyara, na kuvunja mlango kabla ya kumchukua Mchungaji kwa nguvu. Watu hao walitumia silaha kuwatisha wanafamilia wa Mchungaji Mtaita kabla ya kumwingiza kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser isiyo na namba za usajili, kisha wakaondoka kwa kasi. Baada ya siku moja Jeshi la Polisi limekiri kumshikilia.

MANJALE MAGAMBO
Mnamo saa tatu usiku tarehe 24 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita na mtia nia wa ubunge wa Jimbo la Geita Mjini, Manjale Magambo, alitekwa nyumbani kwake katika eneo la Bombambili. Gari lililotumika katika utekaji huo lilionekana likiwa na namba za usajili za Toyota Vanguard, ingawa kwa uhalisia ni Toyota Hilux. Gari hilo linadaiwa kusoma jina la Brian Paul Bayo, mwenye namba ya simu 0710 909 491, na mmiliki wake anaripotiwa kuwa mkazi wa Arusha. Hadi sasa hajulikani alipo.

JUSTAN JUMA KANANDI
Mnamo usiku wa tarehe 25 Oktoba 2025, watu waliodai kuwa ni askari polisi walivamia nyumbani kwa mwanachama wa Chadema, Justan Juma Kanandi, katika kijiji cha Ishinga, kata ya Swaya, Jimbo la Rungwe, mkoani Mbeya, na kuondoka naye bila kutoa maelezo yoyote. Hadi sasa, Kanandi hajulikani alipo.

Tunatoa wito kwa Serikali na vyombo husika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa raia wote bila kujali Vyama itikadi za Vyama vya Siasa. Tunawahimiza wananchi kujilinda na kuwa makini katika kipindi hiki kigumu ambapo matukio ya utekaji yamekidhiri.

Imetolewa leo Jumapili, tarehe 26 Oktoba 2025
Brenda Rupia
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi

c1.jpg
c2.jpg
c3.jpg
c4.jpg
C5.jpg
c6.jpg
 
Ila wanawake mna nguvu aisee. Naomba nisifafanue zaidi kwa leo. Ila nguvu mnazo, siyo mchezo hata kidogo.
 
Back
Top Bottom