John Mrema ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (
CHADEMA) ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa maawasiliano na mambo ya nje, katika chama hicho.
Hivi karibuni
kumeibuka kundi la wanachama wa CHADEMA linalojulikana kama G55, ambao walikuwa ni wagombea 2020 na watia nia wa ubunge kupitia chama hicho wametoa msimamo wao kuelekea uchaguzi mkuu wakipinga msimamo wa chama kuzuia uchaguzi (No Reforms, No Election) badala yake wakihimiza kushiriki Uchaguzi.
Aidha kundi hilo lilifanya
mkutano na waandishi wa habari ukiongozwa na John Mrema ambapo ulikuwa na dhumuni la kufafanua na kuelezea kwa kina waraka walioutuma kwa katibu mkuu wa chama hicho kupinga msimamo wa chama wa kuzuia uchaguzi.
Madai
Mara baada ya mkutano huo kumekuwapo na taarifa inayosambaa mtandaoni kuwa Kamati kuu ya CHADEMA imemfuta uanachama John Mrema kwa kutokuwa na nia njema na Chama hicho akihusishwa na kundi la G55
Uhalisia wa madai hayo
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia maneno muhimu (Key Word Search) umebaini kuwa taarifa hiyo haijatolewa na
CHADEMA, kwani haijachapishwa katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya chama hicho.
Aidha JamiiCheck imebaini mapungufu kadhaa katika taarifa hiyo yanayodhihirisha kuwa ni ya kutengenezwa, sehemu ya mapungufu hayo ni pamoja na matumizi ya aina ya mwandiko (fonts) ambao hautumiwi katika taarifa rasmi za chama hicho.
Hata hivyo mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho
Godbless Lema kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X ameikanusha taarifa hiyo na kuwa si ya kweli. Pia
John Mrema mwenyewe amesema taarifa hiyo ipuuzwe kwa si ya kweli.