Kama siyo ubinafsi wa watu fulani, Chadema ndio kingekuwa chama bora kabisa hapa nchini tangu mwaka 1995.
Baada ya kutoka CCMS, Mrema alikuwa tayari kujiunga na Chadema endapo angehakikishiwa nafasi ya kugombea Urais nafasi ambayo mzee Mtei alikuwa akiiwania pia. Hatimaye Mtei na Chadema wakakosa vyote - Mrema na kugombea Urais.
Ikumbukwe vizuri kuwa wakati huo chama kilichokuwa kimejipanga vizuri kiuongozi kilikuwa chadema chini ya akina Mzee Mtei, Bob Makani, Eric Mchata, Edward Barongo, Brown Ngwilulupi na wengineo pamoja na uwezo mzuri wa kiuchumi. NCCR Kilikuwa kimejipanga na timu ya wasomi ambao hawakuwa na nguvu za kiuchumi - Mrema aliamua kwenda huko na kukiongezea nguvu na umaarufu chama hicho. CUF walikuwa Zanzibar tu na nguvu kidogo kanda ya ziwa iliyojengwa na Mzee Mapalala. Hata Lipumba mwenyewe alikuwa bado hajulikani kabisa katika medani za kisiasa.
Bob Nyanga Makani pengine ndiye aliyepata kuwa kiongozi mwenye dhamira njema ndani ya Chadema. Mwaka 2000 alikubali Chadema isisimamishe mgombea na kukiunga mkono chama cha CUF katika ngazi ya Urais na kuachiana majimbo. Hata hivyo hili halikuwa na nguvu za kisheria bali makubaliano nyenye nia njema.
Ni muhimu kusema hapa kwamba tofauti ya kutosimamisha mgombea mwaka 1995 na 2000ni kuwa wakati mwanzoni Mzee Mtei alijiona hana uwezo wa kushinda kutokana na nguvu ya Mrema, Makani alifanya hivyo kwadhamira njema tu kwakuwa nguvu ya Lipumba haikuwa kubwa kiasi hicho. Mtei hakuacha kwa kupenda bali kulazimishwa na hali.
Unaweza kuishambulia CCM kwa njia ya Mbwa mwitu kwa Simba. Hili dude kubwa na sio rahisi kulishinda mara moja. Njia pekee ilikuwa ni kuachiana maeneo kwa chama chenye nguvu katika eneo husika.
Ilitia faraja katika chaguzi za Kiteto na Tarime kwamba angalau kulikuwa na kuachiana hata hivyo yaliyotokea Mbeya yanathibitisha usanii na unafiki wa wanasiasa wetu. Wasichokitambua Chadema ni kuwa kwa usanii wao wa Mbeya wamewasaliti wananchi sio vyama vingine vya upinzani.
Kosa kubwa walilofanya Chadema ni kujiona tayari wana nguvu kubwa wakati wana wabunge wakuchaguliwa wasiofika kumi kati ya wabunge mamia!
Kwa Mbowe kufuata ubinafsi wa mkwe wake amekinyima Chadema nafasi nyingine ya kuwa chama kinachokubalika zaidi hapa nchini.
NN