Na Maregesi Paul
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeendelea kukishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisema chama hicho hakina nia ya dhati ya kuwakomboa wananchi kwa vile viongozi wake hawana historia nzuri ya kutetea wananchi.
Akihutubia mkutano wa hadhara Manzese jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF, Ismail Jusa, alisema ingawa viongozi wa Chadema wanawaambia Watanzania, kwamba chama chao ndicho kinachowajali zaidi, kauli hizo siyo sahihi kwa vile viongozi hao hawana historia ya kitaifa.
Chadema walikuwa hapa jana, Mbowe alisema mengi sana katika mkutano wake huo, lakini ukweli ni kwamba, chama hicho hakina jipya kwa sababu viongozi wake hawana cha maana ukilinganisha na viongozi wa CUF, alisema Jusa.
Alisema wakati CUF kinaanzishwa mwaka 1992, viongozi wa chama hicho walidhani wangeweza kushirkiana na vyama vingine vya upinzani kuiondoa CCM madarakani, lakini kutokana na sababu ambazo haziko wazi, chama hicho cha upinzani kimegeuka na kukidharau CUF ingawa CUF kina wanachama wengi katika maeneo yote ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, alisema njama za kuihujumu CUF zinazofanywa na viongozi wa Chadema hazitafanikiwa kwa vile chama hicho kinaheshimika kutokana na kazi nzuri zinazofanywa na viongozi wa chama hicho.
Chadema wanataka kutumaliza bila sababu za msingi kwa sababu siku hizi kila wanapopanda majukwaani, ajenda yao kubwa ni kutusema vibaya kadiri wanavyoweza. Lakini, ukweli ni kwamba, hawatatuweza na kama wanataka kujua nguvu tuliyonayo, basi wakawaulize CCM kwani ndiyo wanaotujua vizuri kuliko chama kingine chochote hapa nchini, alisema.
Akizungumzia majigambo ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kwamba viongozi wa Chadema ndiyo vinara wa kupambana na ufisadi, Jusa aliwabeza viongozi hao na kutaka waeleze historia zao katika kipindi chote walichokaa bungeni kwa nyakati tofauti.
Mbowe anajidai yeye ni bingwa wa kupambana na mafisadi, sasa atuambie katika kipindi chote alichokuwa Mbunge alifanya nini na pia Dk. Slaa aseme alikuwa wapi kusema anayosema sasa kabla hajashinda tena kiti cha ubunge wa Karatu mwaka 2005, alihoji Jusa .
Awali, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho, Abdul Kambaya, alisema baada ya Chadema kuonyesha kuwa hawataki siasa za kweli, hivi sasa chama chake kinawahesabu kuwa ndiyo maadui zao namba moja pamoja na CCM.