Ataka tume huru iundwe kuchunguza wizi wa kura
na Salehe Mohamed, Dodoma
HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa tamko zito la kutomtambua Rais Jakaya Kikwete, kwa madai kuwa ameingia madarakani kwa wizi wa kura (uchakachuaji).
Msimamo huo ulitangazwa jana mkoani hapa na viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, ambapo walisema utakuwa ni unafiki kumhalalisha kiongozi aliyeingia madarakani kwa uchakachuaji wa kura.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Slaa, ambaye alikuwa mgombea urais wa CHADEMA, alisema wakati wa utangazaji wa matokeo, CHADEMA waliiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwataka kusitisha zoezi hilo, kwa sababu lilikuwa na kasoro nyingi, ikiwamo ya wizi wa kura, lakini NEC haikuwasikiliza.
Alibainisha kuwa NEC ilifanya kazi kwa uzembe na usiri na ilishiriki kuiba kura zake na kubadilisha matokeo kwa lengo la kumsaidia mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kikwete kupata ushindi mwembamba wa asilimia 61.
Alisema wananchi wamekoseshwa fursa ya kuongozwa na kiongozi waliyemtaka, kwa sababu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu haukuwa huru na wa haki, hivyo hawaoni sababu ya kumtambua kiongozi aliyetokana na matokeo ya uchakachuaji.
Nawashukuru Watanzania kwa kunipa kura zile zilizotangazwa na NEC, lakini leo napenda kuutangazia umma kuwa simtambui Rais Jakaya Kikwete kwa sababu kura zilizompa ushindi zilipatikana kwa msaada wa wizi na si matakwa ya wananchi, alisema.
Dk. Slaa ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuzungumza na vyombo vya habari tangu kutangazwa kwa matokeo ya urais, alisema lengo la demokrasia ni kupatikana kwa kiongozi aliyetokana na matakwa ya wananchi, lakini NEC na vyombo vya usalama viliamua kumpendelea mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Alibainisha kuwa wamefikia hatua ya kutomtambua Rais Kikwete, kwa sababu utaratibu uliopo hivi sasa wa kisheria na kikatiba, hautoi nafasi kupinga matokeo ya uchaguzi katika mahakama au chombo kingine kinachoundwa kikatiba.
Alisema NEC inalindwa kisheria na hata kama inachakachua matokeo ya uchaguzi kwa makusudi kwa lengo la kumnufaisha Rais Kikwete na chama chake.
Alibainisha kuwa katika mazingira hayo ya kisheria na kikatiba, njia pekee waliyonayo kuonyesha kutoridhika na ukiukwaji wa makusudi wa nguzo kuu za uchaguzi huru na wa haki, ni kuheshimu dhamiri zao kwa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na NEC hivi karibuni.
Aidha, alisema Usalama wa Taifa ni mafisadi wa kutumia rasilimali za taifa kwa kusaidia wizi wa kura kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Alisema anao ushahidi wa kutosha kuwa Usalama wa Taifa walifanya kazi hiyo ili kumnufaisha mgombea wa CCM, Kikwete ambaye alitangazwa mshindi katika nafasi ya urais kwa kupata kura milioni tano.
Dk. Slaa alisema matokeo ya uchaguzi yalibadilishwa kwa lengo la kumbeba Kikwete na kuongeza kuwa ushahidi huo hawezi kuupeleka Usalama wa Taifa kama alivyotakiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jacky Zoka, bali ataupeleka mahakamani kama akifunguliwa kesi ya kuikashifu idara hiyo nyeti.
Alibainisha kuwa hawezi kuupeleka ushahidi huo kwa chombo hicho kwa sababu chenyewe ndicho kilichoshiriki kufifisha demokrasia kwa kuchakachua matokeo ya urais, ili Kikwete aibuke na ushindi dhidi ya yeye (Slaa).
Wanataka niwapelekee ushahidi, nifanye hivyo kwa nini wakati wao ndio ninao watuhumu? Wasijidanganye kuwa nitafanya wanachokitaka, kama wanaona wao si mafisadi, wakanishitaki mahakamani, huko ndiko nitawaonyesha, alisema.
Alibainisha kuwa kitendo cha Usalama wa Taifa kuwasambaza vijana wao mikoani kwa lengo la kuisaidia CCM na mgombea wake ni kosa la jinai, kwa sababu wao wamepewa jukumu la kuangalia usalama wa raia wote na wala si kutetea masilahi ya chama fulani.
Aliongeza kuwa CHADEMA haimuogopi yeyote, hivyo Usalama wa Taifa wasijidanganye kuwa wanao uwezo wa kuwatisha, ili wasiibue vitendo viovu vinavyofanywa na taasisi za umma kwa lengo la kulinda masilahi ya watu fulani.
Alisema CHADEMA walishawahi kutangaza orodha ya mafisadi ambayo ilikuwa na vigogo kadhaa wa CCM na serikali, akiwamo Rais Kikwete, hivyo hawawezi kuogopa kuwataja watendaji wa Usalama wa Taifa walioshiriki kwenye vitendo vya wizi wa kura.
Alisema katika wizi wa EPA, walizitaja baadhi ya kampuni zinazomilikiwa na watendaji wa Usalama wa Taifa ambao walitishia kwenda mahakamani lakini hadi sasa hawajakwenda.
Hivi karibuni Dk. Slaa, alitoa malalamiko kuwa Usalama wa Taifa walishiriki kuiba kura ili kumsaidia Rais Kikwete, lakini madai hayo yalipingwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Jack Zoka.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema msimamo wao hauwezi kubadilisha matokeo hayo wala kumzuia aliyetangazwa na kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya kazi zake lakini hawapo tayari kuhalalisha matokeo yaliyotokana na ukiukwaji wa makusudi wa katiba, sheria za uchaguzi na kanuni za uchaguzi huru na wa haki.
Alisema hivi sasa CHADEMA inataka iundwe tume ya uchunguzi wa mchakato mzima wa uchaguzi pamoja na kutaka kuwapo kwa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, ambayo haitapendelea chama chochote cha siasa.
Aliongeza kuwa watapeleka hoja bungeni kutaka mabadiliko ya katiba na wanaamini hoja hiyo itapata uungwaji mkono na wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani, kwa sababu haitakuwa ikisimamia masilahi ya chama bali inalenga kustawisha maendeleo ya nchi.
Hatudai mambo haya kwa nguvu, vurugu na fujo, kwani tukifanya hivyo tutakuwa tunaathiri amani na utulivu tulionao, sisi ni wadumisha amani, tutalitumia Bunge na majukwaa mbalimbali kudai tume huru ya uchaguzi pamoja na katiba mpya, alisema.
Alisema pamoja na kutomtambua Rais Kikwete, wabunge, madiwani na watendaji kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini, hawataacha kazi zao, bali wataendeleza utumishi wa umma ndani ya vyombo husika huku wakitanguliza mbele masilahi ya taifa, ikiwamo kupambana na ufisadi.
Alisema hata kama wabunge wake watateuliwa na rais, CHADEMA haitakuwa tayari kuingia serikalini, kwani yenyewe inajiandaa kuongoza serikali ijayo.
Mbowe alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania na waandishi wa habari kutolazimisha ndoa ya wapinzani na wanasiasa, bali walazimishe fikra zinazokubaliana kushirikiana.
Alisema vipo vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa vikivaa ngozi ya kondoo wakati vyenyewe ni chui ambao hawapendi kuona maendeleo ya CHADEMA.
Sisi tupo tayari kushirikiana na chama chochote makini, nasisitiza makini kwa sababu kuna vingine ni wakala wa CCM. Leo hii kuna vyama vya siasa vimetupeleka mahakamani vikitaka tuvilipe fidia na wabunge wetu wavuliwe nyadhifa zao, sasa unataka tushirikiane navyo? alihoji.
Alisema CHADEMA iliwasiliana na Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu kuunganisha nguvu na kuunda kambi ya upinzani lakini kwa bahati mbaya walipewa jibu kuwa chenyewe kimejiunga na vingine kuanzisha kambi ndogo.